Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO. Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wamenunua mtambo mpya wa kisasa unaojulikana kama ...
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Wakala
wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wamenunua mtambo mpya wa kisasa
unaojulikana kama ‘Energy Dispersive X-Ray Fluorescence Spectrometer’
(EDXRF) kwa ajili ya kurahisisha uchunguzi wa kimaabara.
Mtambo
huo uliogharimu kiasi cha shilingi 101,785,200 umesimikwa katika
Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya Nyanda za Juu Kusini mkoani
Mbeya kuanzia Februari 21 hadi 23 mwaka huu.
Hayo
yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na Mkemia Mkuu wa Serikali. Prof.
Samwel Manyele alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu
matumizi ya mtambo huo.
Prof.
Manyele amesema kuwa mtambo huo umesimikwa mkoani mbeya ikiwa ni moja
ya hatua za kuboresha maabara za Kanda zilizopo Arusha, Dodoma, Mbeya,
Mtwara na Mwanza, kusogeza shughuli za uchunguzi karibu na wananchi ili
kupunguza gharama za kusafirisha sampuli kuja mkoani Dar es Salaam kwa
ajili ya uchunguzi.
“Kuwepo
kwa mtambo huo ni suluhisho kwa Serikali, Wizara, Viwanda, Mashirika,
Wachimbaji wa madini, wajasiriamali na wananchi kwa ujumla ambao
walikuwa wanahitaji kufahamu ubora na usalama wa bidhaa mbalimbali za
viwandani na mashambani, kutambua uwepo wa madini ya thamani kwenye
udongo na bidhaa za vito pamoja na sampuli zinazohusiana na usalama wa
afya na mazingira,”alisema Prof. Manyele.
Ameyataja
matumizi mengine ya mtambo huo kuwa ni kufanya uchunguzi wa sampuli za
migodini, kupima bidhaa za mbao ili kubaini kiwango cha kemikali
zinazotumika kutibu mbao, kupima sampuli za mafuta ya kula kwa kuangalia
kiwango cha madini ya phosphorus, kupima sampuli za pembejeo za kilimo
pamoja na kufanya uchunguzi wa sampuli na vielelezo vinavyohusiana na
makosa ya jinai.
Prof.
Manyele amefafanua hoja zitakazojibiwa na matumizi ya mtambo huo
zikiwemo za kufahamu dhahabu kiasi gani ipo katika udongo unaohitaji
kuchenjuliwa, kufahamu mbogamboga zinazolimwa bondeni zina kiasi gani
cha madini yanayoathiri watumiaji, kufahamu kiasi cha uranium katika
ardhi na vyanzo vya maji pamoja na kufahamu athari za aina ya madini
yaliyopo katika maji ya visima virefu na vifupi kwa watumiaji.
Aidha,
Mkemia Mkuu amebainisha kuwa baada ya kuzinduliwa kwa mradi huo,
Maabara ya Nyanda za juu kusini itakua na majukumu ya kukusanya sampuli
za vinasaba vya binadamu (DNA) pamoja na kuwa kituo rasmi cha kukusanyia
sampuli nyingine mbalimbali.
Maabara
hiyo kwa sasa ipo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya ambapo kuanzia
mwezi Aprili mwaka huu itahamia katika eneo la Lwambi lililopo mkoani
humo.
Mkemia
Mkuu wa Serikali, Prof. Samwel Manyele (katikati) akizungumza na
waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dar es Salaam kuhusu
kuanza kazi kwa mtambo mpya wa kisasa wa Energy Dispersive X-Ray
Fluorescence (EDXRF) kwa ajili ya kufanyia uchunguzi wa kimaabara. Kutoka
(kulia) ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Huduma za Ubora wa Bidhaa,
Daniel Ndiyo, Mkurugenzi Idara ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali
Nchini, Sabanitho Mtega, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo
ya Biashara George Kasinga (kushoto) pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya
Sayansi Jinai na Huduma za Vinasaba, David Elias.
Baadhi
ya watumishi wa Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na
Waandishi wa Habari wakimsikiliza Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof. Samwel
Manyele (hayupo pichani) jijini Dar es Salaam wakati akizungumza
kuhusu kuanza kazi kwa mtambo mpya wa kisasa wa Energy Dispersive X Ray
Fluorescence (EDXRF) kwa ajili ya kufanyia uchunguzi wa kimaabara.
Mtambo huo umefungwa kwenye Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya
Nyanda za Juu Kusini, Mkoani Mbeya.
Mtambo
wa Energy Dispersive X– Ray Fluorescence (EDXRF) unaotumika
kupima sampuli mbalimbali zenye asili ya yabisi na vimiminika kama vile
vyakula, bidhaa za mafuta, maji, simenti, makaa ya mawe, bidhaa za chuma
ili kutambua kiwango cha madini kilichomo ndani ya sampuli hizo. Mtambo
huo umefungwa kwenye Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya Nyanda
za Juu Kusini, Mkoani Mbeya.
COMMENTS