NA LILIAN LUNDO – MAELEZO SERIKALI imefuta usajili wa vibali vya uzalishaji na Uingizaji wa aina 20 ya pombe kali z...
NA LILIAN LUNDO –
MAELEZO
SERIKALI imefuta usajili wa vibali vya uzalishaji na Uingizaji
wa aina 20 ya pombe kali za viroba zilizokuwa zimesajiliwa na Mamlaka ya
Chakula na Dawa (TFDA).
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Ummy
Mwalimu, (pichani juu), ameyasema hayo leo, Jijini Dar es Salaam kuhusu usitishaji wa
uzalishaji na uingizaji, uuzaji na matumizi ya pombe zilizofungwa katika mifuko
ya plastiki (Viroba).
“Tumefuta usajili wa vibali vya uzalishaji na uingizaji kutoka
nje, usambazaji, uuzaji na matumizi ya pombe kali zilizofungashwa katika mifuko
ya plastiki (viroba) chini ya ujazo wa milimita 200,” alifafanua Ummy Mwalimu.
Aliendelea kwa kusema kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa tamko la
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alilotoa Februari 02, 2017 la kusitisha uzalishaji,
uingizaji, usambazaji, uuzaji na matumizi ya pombe hiyo kali kuanzia Machi 01,
2017.
Ummy amesema kuwa usitishaji huo unazingatia kanuni za kukataza
uzalishaji, uingizaji na matumizi ya vifungashio vya plastiki kufungashia pombe
kali za mwaka 2017 (The Environmental Management (Prohibition of Manufacturing,
Important and Use of Plastic Sachets for Packakging Distilled and other
alcoholic beverages) Regulations 2017) imekatazwa kutumia vifungashio vya
plastiki kufungashia pombe kali. Badala yake wazalishaji watapaswa kufungasha
pombe kali hizo katika chupa zenye ujazo usiopungua mililita 200.
Aidha amesema kuwa uamuzi wa kupiga marufuku matumizi ya pombe
za aina hiyo unatokana na athari mbalimbali ikiwa ni pamoja na za kiafya na
kijamii.
Matumizi mabaya ya pombe hizo yamesababisha ajali
nyingi, vifo, ulemavu na mzigo mkubwa kwa Serikali wa kutoa huduma kwa wahanga
wa pombe hizo na ongezeko la
makosa ya jinai.
Ummy amesema kwamba Viroba vilivyokamatwa na kuzuiwa vinasubiri
maelekezo kutoka ofisi ya Waziri Mkuu namna ya kuviteketeza.
COMMENTS