Na Mwandishi wetu Washington Kila ifikapo tarehe 14 Februari nchini Marekani na sehemu nyengine Duniani husherehekewa...
Na Mwandishi wetu Washington
Kila ifikapo tarehe 14 Februari nchini Marekani na sehemu nyengine
Duniani husherehekewa Siku ya Wapendanao "Valentine's Day", au kama
ijulikanavyo kwa jina jingine "Siku ya Mtakatifu Valentine" (Saint
Valentine's Day). Katika miaka ya hivi karibuni siku hii pia imeanza
kusherehekewa katika maeneo ya Afrika Mashariki. Shukrani ziende kwa
enzi za utandawazi. Lakini je Siku Kuu hii ilianzia lini?
Asili yake
Hakuna chanzo cha uhakika kuhusu asili na chimbuko la Siku ya
Wapendanao. Hata hivyo inaaminika kuwa asili yake inarejea katika enzi
za Himaya ya Warumi, na baadaye Kanisa Katoliki kuingiza katika Ukristo.
Kuna watu watatu katika historia ya Kanisa Katoliki ambao
wanajulikana kama Mtakatifu Valentine au Valentinus, na wote inasadikiwa
walikufa kama mashahidi kwa mujibu wa itikadi za Kikatoliki, na kwa
hivyo Kanisa likaamua kuiadhimisha siku waliyonyongwa kama kuwaenzi
watumishi hao.
Kuna nganu inayodai kuwa Valentine alikuwa ni Mchungaji aliyehudumu
Roma katika karne ya tatu. Wakati huo, Mfalme Claudius Wa Tatu,
alipitisha amri ya kupiga marufuku ndoa kwa vijana wa Kiume kwa vile
alihisi kuwa wanaume wasio na wake au familia walikuwa askari bora zaidi
kuliko waliokuwa kwenye ndoa.
Mchungaji Valentine hakukubaliana na amri hiyo ya Mfalme na akawa
naendelea kufungisha watu ndoa kwa njia za siri. Mfalme Claudius
alipogundua mpango huo, aliamuru Valentine anyongwe.
Simulizi nyengine zinadai kuwa Valentine huenda alinyongwa kwa kosa
la kuwasaidia Wakristo kutoroka katika magereza ya Warumi ambako
walikuwa wakiteswa vibaya.
Inadaiwa kuwa Valentine ndiye aliyetuma maamkizi ya mwanzo ya mapenzi
(valentine) kumpelekea msichana aliyempenda ambaye alikuwa akimtembelea
wakti akiwa gerezani.
Inadaiwa kuwa kabla ya kifo chake, aliandika barua na kuisaini
"Kutoka kwa wako Valentine". Maneno hayo bado yanaendelea kutumika hadi
leo katika kadi za maamkizi ya siku ya Wapendanao.
Kwa upande mwengine, inasadikiwa kuwa kuanzia tarehe 13 hadi 15
Februari, Warumi walikuwa na desturi ya kusherehekea siku iliyojulikana
kwa jina la Lupercalia. Miongoni mwa ada za siku hii ilikuwa ni wanaume
kuwapiga wanawake.
Mnamo karne ya tano, Baba Mtakatifu Gelasius wa Pili, alikoroga mambo
kwa kuichanganya siku ya Mtakatifu Valentine pamoja na ile ya
Lupercalia kwa lengo la kuizika ada hiyo ya kipagani ya Warumi.
Kadiri miaka ilipozidi kusonga mbele ndivyo kadiri siku ya Wapendanao
ilivyozidi kusherehekewa, mpaka ikafikia enzi za Shakespeare na
Chaucer, ambao waliipamba siku hiyo katika kazi zao za sanaa na hivyo
kuipatia siku hii umaarufu zaidi. Katika karne za kati, kadi
zilizotengenezwa kwa mikono ndizo zilikuwa zikitamba.
Hatimaye, utamaduni huo ukavuka bahari na kunigia nchini Marekani na
sehemu nyengine ulimwenguni, na mnamo karne ya 19 mapinduzi ya viwanda
yakachapuza katika uchapishaji wa kadi za maakazi na kuipa umaarufu
mkubwa zaidi siku hiyo. Katika mwaka 1913 shirika la Hallmark likaanza
kuchapisha kadi za Siku ya Wapendao na kubadilisha mkondo wa kihistoria
wa kuadhimisha siku hiyo.
Katika enzi za leo
Siku ya Wapendao si Sikuu Rasmi nchini Marekani. Watu huenda makazini
kama kawaida, hata hivyo kama zilivyo Siku Kuu nyingi nchini humu, nayo
pia imekumbwa na kimbunga cha biashara tangu pale Hallmark
walipoanzisha kuzalisha kadi zao kwa wingi. Hii ni siku ya pili kwa
ukubwa wa mauzo katika mwaka baada ya siku ya Christmas.
Inakadiriwa kuwa mauzo ya kadi hizo katika siku hiyo hufikia zaidi ya
Dola Billioni 15. Baadhi ya watani wanasema kuwa "iwapo sherehe za siku
ya Wapendanao zitapigwa marufuku nchini Marekani, basi shirika la
Hallmark litafilisika"
Biashara nyengine inayochangamka katika siku hiii ni ya maua. Tani za
maua huuzwa katika siku hii, na baadhi ya wauza-maua huajiri wafanyazi
wa kiasi wiki moja kabla ya siku hii ili kukabiliana na ongezeko la
wateja. Waridi ni nembo ya pili maarufu katika siku hii baada ya ile ya
moyo.
Mbali na biashara hizo mbili, kuna zawadi aina kwa aina ambazo watu
huwanunulia wale wawapendao, zikiwemo pipi, chakileti, na vitu vyengine
vya kula na kunywa ambavyo ama hutengenezwa katika umbo la "moyo" kama
ishara ya mapenzi, au kufungwa katika vifurushi vilivyopambwa katika
mfumo kama huo.
Siyo Hallmark tu wanaofaidika katika siku hii, bali biashara nyingi
mauzo yao huongezeka khususan mikahawa ambayo watu wanaotaka kudhirisha
mapenzi kwa wapenzi wao hujazana katika sehemu hizo na kudhihirisha
mapenzi ya hali ya juu kwa kuagizisha milo ya fakhari.
Kwa ujumla Waswahili wanasema "Mtu hujikuna ajipatapo". Kwa hivyo,
kuna wale ambao huwanunulia wapenzi zawadi khafifu kama vile kadi yenye
thamani ya chini, na kendelea mpaka kufikia vito vya thamani, magari,
majumba na sema upendavyo.
Nchini Marekani, Canada na kwengineko, baadhi ya maskuli huandaa
tafrija maalum za Siku ya Wapendanao ambapo wanafunzi hubadilishana
zawadi na marafiki zao ambazo aghlabu huwa ni pipi, chakileti na kadi za
maamkizi.
Wanaosherehekea na Wasiosherehekea siku hii.
Ingawaje siku hii huzalisha mabilioni ya Dola nchini Marekani, hata
hivyo wako watu ambao hawasherehekei siku hii kutokana na sababu
mbalimbali.
Wale wanaosherehekea wanaona kuwa ni siku iliyojaa upendo. "Siku ya
Wapendanao ni siku iliyojaa upendo, anga yote huwa imejaa mapenzi",
anasema Angie Bradlye, Msimamizi wa Uzalishaji katika kiwanda kimoja
nchini Marekani, na kuongeza, "ingawa mume wangu amefariki, lakini
katika siku hii hujihisi kama niko pamoja naye na moyo wangu hujaa
furaha"
Naye Mae, anaona kuwa ni fursa kwa wanaume kudhihirisha mapenzi kwa
wapendanao. "Ni siku muhimu kwa wanaume kudhihirisha mapenzi kwa
wanawake wawapendao" alisema.
Kwa upande wa wale wasiosherehekea siku hii nao pia wana sababu zao.
Scotty ni Mmarekani mwenye asili ya Afrika na anasema "Mimi
siadhimishi siku hii kwa sababu ni siku kuu iliyotengenezwa na Wazungu
tu kwa ajili ya kujipatia pesa kutokana na mauzo ya biashara zao"
Hata hivyo, Blue, ni mwanamke wa Kizungu, lakini hasherehekei siku
hii akisema "Huu ni upuuzi mtupu, si chengine chochote ispokuwa wanawake
wasiokuwa na shukurani kujipatia zawadi wasizostahiki kutoka kwa
mabwana zao"
Wengine huwa hawasherehekei kwa sababu hawana wapenzi wa kusherehekea
nao, kama ambavyo Kendra Simpson kutoka Jimbo la Karolina Ya Kusini
aliiambia Swahillivilla : "Mimi sisherehekei kwa sababu sina mpenzi kwa
sasa, kama nina mpenzi na anapenda kuadhimisha siku hii, basi nitaingia
naye pumbaoni". Hata hivyo alisisitiza kuwa kila siku inapaswa kuwa siku
ya mapenzi kwa wapendao, na siyo siku hii moja tu.
Rai hiyo inaungwa mkono na Bi LaToya Bragg wa jimbo la Ohio, ambaye
anasema "ni jambo la kushangaza kuona watu wanahemkwa na kupoteza mapesa
katika siku hii moja, wakati ambapo mapenzi yanatakiwa kudumu kwa muda
wote ambao watu wapendanao huwa pamoja katika uhai wao"
Athari mbaya za Kijamii.
Bi Latoya aliyeandika kitabu kwa jina "The Heart Of Me" pia haoni
sababu ya kuadhimisha siku hii katika mfumo wake wa sasa kwa vile
unaleta athari mbaya za kijamii. "Kuna watu wengine hali zao za kiuchumi
siyo nzuri, kwa hivyo hawawezi kunnuua zawadi kwa wapenzi wao, na hivyo
wapenzi wanaokosa zawadi kutoka kwa wapenzi wao, hujihisi duni mbele ya
wenzao"
"Aidha huleta athari za kiuchumi kwa watu wenye kipato cha chini kwa
kujikalifisha kuwanunulia wapenzi wao zawadi wazipendazo ambazo wakati
mwnengine ziko nje ya uwezo wao, almradi tu na wao waonekani ni watu
katika jamii"
Mbali na umaarufu wa siku hii, hata hivyo uchunguzi mdogo uliofanywa
na Swahilivilla umeonesha kuwa, idadi kubwa ya watu hawajui asili,
chimbuko na maana ya Siku ya Wapendanao. Kristy, ni afisa wa mapokezi na
usafirishaji katika Shirika moja la vifaa vya magari anasema:
"Ninavyojua siku hii ni ya wanaume kuwanunulia zawadi wapenzi wao, na
kwa wanaume siku yao ni ile inayoitwa 'sweetest hearts day'.."
Naye Amanda Waleker anasema: "Sijui chochote kuhusu asili ya siku
hii, watu wanasherehekea na kuadhimisha, lakini mimi si katika mambo
yangu"
COMMENTS