Na Greyson Mwase, Dar es Salaam Visiwa vidogo vilivyopo katika Ziwa Viktoria vinatarajiwa kupata umeme wa uhakika ifikapo Juni mw...
Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Visiwa vidogo vilivyopo katika Ziwa Viktoria vinatarajiwa kupata umeme wa uhakika ifikapo Juni mwakani.
Hayo
yalielezwa na Kamishna Msaidizi- Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya
Nishati na Madini Mhandisi Styden Rwebangila, alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa akielezea
mafanikio yaliyopatikana Sekta ya Nishati kupitia Nishati Jadidifu chini
ya Idara ya Nishati katika upatikanaji wa umeme wa uhakika.
Alisema
kuwa, wakandarasi wameshaanza kuweka miundombinu kwa ajili ya umeme wa
jua ambapo miradi hiyo inatarajiwa kukamilika kwa asilimia mia moja
ifikapo mwezi Juni mwakani.
Akielezea
mipango ya Serikali katika kuhakikisha kuwa nishati ya umeme inakuwa ni
ya uhakika Mhandisi Rwebangila alisema Wizara inahamasisha vyanzo
vingine vya uzalishaji wa umeme kama vile jua, upepo, jotoardhi na
kuongeza kuwa inakaribisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi
kutafiti na kutumia vyanzo hivyo.
Alisema
kwa upande wa jotoardhi utafiti ulifanyika na kuonesha maeneo ya Songwe
na Ziwa Ngozi mkoani Mbeya na Mlima Meru mkoani Arusha yana viashiria
vya jotoardhi.Aliongeza
kuwa mara baada ya utafiti kukamilika mwishoni mwa mwaka huu, visima
vinatarajiwa kuanza kuchimbwa kwa ajili ya uzalishaji wa nishati ya
jotoardhi.
Aliendelea
kutaja mipango mingine kuwa ni pamoja na uanzishwaji wa mwongozo kwa
ajili ya mfumo wa umeme kwenye majengo na wa udhibiti wa matumizi ya
umeme viwandani.
Alisema
pia, Wizara inatarajia kuanzisha mfumo mpya wa uhifadhi data na utoaji
taarifa za Nishati Jadidifu ujulikanao kama Tanzania Renewable Energy
Management Information System (TREMIS) utakaowezesha wawekezaji ndani na
nje ya nchi kubaini fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta ya Nishati
Jadidifu.
Alisema
katika mfumo huo kutawekwa taarifa mbalimbali kuhusu, tafiti mbalimbali
na fursa za uwekezaji katika nishati jadidifu , sera, sheria na
taratibu ili kuvutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.
“Kupitia
mfumo huu kutakuwa hakuna haja ya mwekezaji kutoka nje ya nchi kufunga
safari hadi Tanzania kwa ajili ya kupata taarifa, taarifa zote
zitakuwepo katika mfumo huu utakaounganishwa na tovuti ya Wizara,”
alisema Mhandisi Rwebangila.
Kamishna
Msaidizi- Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi
Styden Rwebangila, (kushoto) akielezea mafanikio ya sehemu ya nishati
jadidifu chini ya Idara ya Nishati katika upatikanaji wa umeme wa
uhakika katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es
Salaam mapema tarehe 06 Februari, 2017. Kulia ni Mtaalam wa Nishati
Jadidifu, Emillian Nyanda.
COMMENTS