Na Hamza Temba - Wizara ya Maliasili na Utalii (WMU) Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imetembelea makao makuu ya Wizara ya ...
Na Hamza Temba - Wizara ya Maliasili na Utalii (WMU)
Kamati
ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imetembelea makao makuu ya Wizara ya
Maliasili na Utalii, Mpingo House jijini Dar es Salaam leo na kuzuru ghala la nyara
za Serikali kuona utunzaji wa meno ya tembo na changamoto zake.
Kabla ya
kutembelea ghala hilo kamati hiyo ilipokea taarifa maalum ya wizara juu ya
mchakato mzima wa taratibu za ukusanyaji wa meno ya tembo, usafirishaji, uhakiki,
usajili kwenye mfumo maalum wa kielektroniki, uhifadhi wake na ulinzi thabiti
wa ghara hilo.Akizungumza wakati wa kuwasilisha taarifa hiyo, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Kupambana na Ujangili wa Idara ya Wanyamapori, Bw. Robert Mande alisema meno yanayohifadhiwa katika ghala hilo ni yale yanayotokana na vifo asilia, kuuawa kutokana na uharibifu wa mali na maisha ya binadamu na yale yanayotokana na ujangili.
Waziri
wa Maliasili na utalii, Prof. Jumanne Maghembe akijibu moja ya swali la wajumbe
wa kamati hiyo ambao walitaka kujua uwezekano wa kuuza meno hayo ya tembo
yaliyohifadhiwa ili kulipatia taifa mapato, amesema msimamo wa Serikali
ya Tanzania kwa sasa sio wa kuuza wala wa kuchoma meno hayo.
"Msimamo
wetu ni kama ule wa nchi za Kenya, Uganda, Zambia, Malawi na Msumbiji wa
kutokuuza meno haya kwa sasa kwasababu mbalimbali za kimsingi kabisa, moja
ikiwa ni sababu za kiutafiti ambapo vinasaba vya meno ya zamani vinaweza
kutumika kubaini mambo mbalimbali ikiwemo utafutaji wa dawa ya magonjwa ya tembo”,
alisema Maghembe.Alisema kitendo cha kuuza meno hayo pia ni kuchochea zaidi biashara hiyo kwakuwa kitaongeza upatikanaji wa bidhaa hiyo kwenye masoko hivyo kuendelea kuipa uhai biashara hiyo haramu duniani.
Hapo awali, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Generali, Gaudence Milanzi akizungumza kwenye kikao cha kamati hiyo mkoani morogoro kilichohusisha uongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) alisema ujangili hapa nchini kwa sasa umepungua kwa kiasi kikubwa na kwamba nyara zinazokamatwa kwa sasa ikiwemo meno ya tembo ni za zamani zilizokuwa zikisubiria kusafirishwa nje ya nchi.
Alisema hatua hiyo ya kupungua kwa uhalifu huo imefanikiwa kutokana na kazi kubwa inayofanywa vikosi maalum vya Askari wa wanyamapori vya kudhibiti ujangili kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama nchini.
Alisema hatua ya Serikali ya China kupiga marufuku biashara ya meno ya tembo nchini humo ni jambo la kupongezwa na kwamba uamuzi huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza msukumo wa vitendo vya ujangili nchini na barani Afrika kwa ujumla.
Naye mwenyekiti wa kamati hiyo ya bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhandisi Atashasta Nditiye amewapongeza viongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii namna walivyojipanga katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara hiyo na kuwaahidi ushirikiano kutoka kwa kamati yake.
Aliahidi kutoa ushirikiano kwa uongozi wa wizara hiyo katika kuhakikisha kuwa wanaikabili changamoto kubwa ya uvamizi wa mifugo kwenye maeneo ya hifadhi. "Sisi tunaungana na nyie, hatukubali mifugo kwenye hifadhi zetu, kwakuwa zinaharibu ubora wa hifadhi hizo, tunawaahidi ushirikiano wa kukabiliana ma changamoto hiyo"
Kamati hiyo ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ilitembela pia makao makuu ya Wakala ya Mbegu za Miti Tanzania (TTSA), Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) na Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) zote za mkoani Morogoro.
COMMENTS