Benny Mwaipaja, WFM, Arusha Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Doroth Mwanyika, amewataka wakaguzi wa ndani n...
Benny Mwaipaja, WFM, Arusha
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Doroth Mwanyika, amewataka wakaguzi wa ndani nchini kuhakikisha kuwa miradi mikubwa ya ujenzi wa miundombinu ikiwemo barabara na majengo yanajengwa kwa ubora unaolingana na thamani ya rasilimali fedha iliyotumika.
Bi. Mwanyika ametoa rai hiyo Jijini Arusha wakati akifungua mafunzo ya siku nne ya wakaguzi wa ndani kutoka Halmashauri za wilaya na Sekretarieti za mikoa iliyoko Kanda ya Kaskazini, Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara
Amesema kuwa wabunge na wananchi kwa ujumla wamekuwa wakilalamikia miradi mingi mikubwa ikijengwa chini ya kiwango na kuisababishia serikali hasara kubwa kutokana na usimamizi mbovu unaofanywa na mamlaka na idara za serikali wakiwemo wakaguzi wa ndani.
“Nina Imani kuwa mafunzo mnayoyapata ya namna ya kukagua ubora wa miradi mikubwa inayotumia fedha nyingi za serikali yatasaidia kuokoa fedha na kuifanya miradi inayojengwa idumu muda mrefu” aliongeza Bi. Mwanyika.
Kwa upande wake Mkaguzi wa ndani Mkuu wa Serikali Bw. Mohammed Mtonga, amesema kuwa kuanzishwa kwa mafunzo hayo yanayofadhiliwa kupitia mradi wa kuboresha Mifumo ya Fedha (PFMRP), yanatokana na mahitaji makubwa ya ujuzi wa namna ya wakaguzi wa ndani wanavyoweza kutambua ubora wa miradi mikubwa ya ujenzi inayotekelezwa hapa nchini kama inakidhi viwango.
“Wakaguzi hawa si wataalamu wa masuala ya ukandarasi lakini uwezo wanaojengewa ni pamoja na kupelekwa kwenye miradi mikubwa ya uejnzi ikiwemo barabaraba ambapo wataelekezwa namna ya kutambua miradi ambayo haikidhi viwango na kutoa ushauri kwa watoa maamuzi ili kuokoa fedha ya serikali isipotee” aliongeza Mtonga.
Wakaguzi wa ndani 302 kutoka Halmashauri na Sekretarieti za Mikoa nchini wamepatiwa mafunzo hayo ambapo pamoja na mafunzo ya nadharia, wakaguzi hao wa ndani wamefundishwa kivitendo namna ya kutambua miradi iliyojengwa chini ya viwango.
COMMENTS