Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Kanali mstaafu Abdulrahman Kinana amemtumia salamu za rambi rambi Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa...
Katibu
Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Kanali mstaafu Abdulrahman Kinana amemtumia
salamu za rambi rambi Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es salaam Ndg.
Ramadhan Madabida kufuatia kifo cha Muasisi wa TANU Bibi Hadija Bint
Kamba, kilichotokea jana tarehe 30 Novemba, 2016 jijini Dar es salaam.
Bibi
Hadija Bint Kamba ni miongoni mwa wanaharakati waliopigania uhuru na
ukombozi wa Taifa letu. Ameshiriki kuanzisha Baraza la Wanawake
Tanganyika mwaka 1955 na baadae Umoja wa Wanawake wa Tanganyika (UWT)
tarehe 02 Novemba 1962 akishirikiana na Bibi Titi Mohamed.
Bibi
Hadija hakuwahi kushika nafasi za uongozi ndani ya Chama na Serikali
baada ya uhuru mpaka mwaka 1985 ambapo Mwalimu Nyerere alimtangaza mbele
ya Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na Baraza la Wazee wa Dar
es salaam Diamond Jubilee, kuwa ni mtu aliyetoa mchango mkubwa katika
ujenzi wa Chama na Nchi, tangu wakati huo Bibi Hadija Bint Kamba
alihudhuria Mikutano mikuu ya Chama kama mjumbe mwalikwa mpaka umri
ulipomzuia kuweza kushiriki.
Bibi
Hadija Binti Kamba, atakumbukwa na wanachama wa CCM kwa uadilifu,
uvumilivu, ujasiri na mchango wake mkubwa katika ujenzi na uimarishaji
wa Chama chetu, na kwamba mchango wake katika kupigania uhuru na kuleta
ukombozi na maendeleo kwa Wanawake wa taifa hili utaendelea kuenziwa na
kuthaminiwa na Watanzania.
Hakika sisi ni wa MwenyeziMungu na kwake yeye ndio marejeo yetu.
Imetolewa na:-
Christopher Ole Sendeka (MNEC)
MSEMAJI WA CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)
01.12.2016
COMMENTS