WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema
Serikali imepiga marufuku uchapaji holela wa vitabu vya kufundishia na
kujifunzia kwa wachapaji binafsi na badala yake uchapaji huo utasimamiwa na
Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE) ili kuthibiti ubora.
Amesema mbali na kudhibiti wa ubora pia
uamuzi huo unalenga kuwa na kitabu kimoja kwa kila somo kwa kila mwanzfunzi kwa
nchi nzima ili kuweka uwiano mzuri katika ufundishaji na upimaji wa wanafunzi .
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Desemba 2, 2016) wakati akizungumza na walimu
wa halmashauri ya Jiji la Arusha na wilaya ya Arusha kwenye Ukumbi wa Mikutano
wa Kimataifa wa Arusha (AICC) akiwa katika siku ya kwanza ya ziara ya kikazi
mkoani Arusha.
Ziara hiyo inalenga kukagua utelelezaji
wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM,Utendaji wa Serikali, kusikiliza na kujionea kero
zinazowakabili wananchi wa Mkoa huo kwa
kushirikiana na viongozi wa Mkoa ili kuweza kuzitafutia suluhisho.
Amesema
kipindi cha nyuma vitabu vilikuwa vinachapwa na watu mbalimbali hivyo kusababisha
malalamiko makubwa kutokana na vitabu hivyo kuwa na makosa mengi. “Sasa vitabu
vikibainika kuwa na makosa tutaibana Taasisi ya Elimu Tanzania,”.
Aidha,
amesema Serkali itahakikisha kila mtoto anakuwa na kitabu chake ili kuwawezesha
kusoma vizuri na kuwa na uelewa wa kutosha ikiwa ni pamoja na kuwarahisishia
walimu katika ufundishaji.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu amezungumzia kuhusu madeni ya walimu, ambapo amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kutenga fedha katika
mapato yao kwa ajili ya kulipa madai ya watumishi mbalimbali katika maeneo yao
wakiwemo walimu.
Awali
Waziri Mkuu alizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Jiji na wilaya ya Arusha
na kumuagiza Kamanda wa Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
mkoa wa Arusha kumchunguza Ofisa Utumishi wa wilaya ya Arusha, Bi. Imelda Isosi
kufuatia tuhuma za rushwa, ufisadi, unyanyasaji kwa watumishi zilizotolewa
dhidi yake.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo baada watumishi hao kupewa
fursa ya kumuuliza maswali ambapo mhudumu wa Chumba cha kuhifadhia maiti wa
Hospitali ya Ortumet Wilayani Arusha, Bw. Bernard Mtei kudai kwamba halmashauri
ya wilaya ya Arusha inanuka ufisadi na rushwa hususan katika sekta ya afya.
Baada
ya kutoa madai hayo Bw. Mtei alimkabidhi Waziri Mkuu nyaraka mbalimbali zenye
uthibitisho wa madai hayo, ambapo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Mrisho Gambo amuhakikishia
Waziri Mkuu kwamba watafanya uchunguzi wa kina dhidi ya tuhuma hizo na
zikithibitika wahusika watachukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria
Wakati huo huo Waziri Mkuu ameitaka
Idara ya Uhamiaji kudhibiti wahamiaji haramu kwa kuanza kufanya misako katika
nyumba za kulala wageni ili kuwabaini wageni wanaoingia nchini bila ya kibali
kwani ni chanzo cha kuingiza silaha haramu nchini.
Amesema
inashangaza kuona silaha za aina nyingi katika maeneo mbalimbali ambazo Tanzania
hakuna ambazo zinadaiwa kuingia nchini kupitia maeneo ya mpakani. “Hivyo ni
lazima Idara ya Uhamiaji ihakikishe wanadhibiti uingiaji wa wahamiaji kwenye mipaka
mbalimbali nchini,”.
Waziri
Mkuu amesema Serikali haizuii wageni kutoka mataifa mengine kuingia nchini ila
ni lazima udhibiti wa wageni hao ufanyike ikiwa ni pamoja na kujiridhisha
sababu za kuja nchini na muda watakao kuwepo.
Hata
hivyo aliwasihi watumishi wa idara mbalimbali za Serikali kuhakikisha wanafanya
kazi kwa nidhamu, weledi, uadilifu na kuwatumikia wananchi wanaohitaji huduma
mbalimbali hata kama wamekosea kuuliza katika maeneo yao.
Amesema
“baadhi ya wananchi hawana uelewa juu ya wapi wapeleke malalamiko yao
lakini kwa kuwa wewe ni mtumishi wa umma unapaswa kumsikiliza na kumwelekeza
aende wapi badala ya kumtolea maneno yasiyofaa,”.
IMETOLEWA NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU
IJUMAA,
DESEMBA 2, 2016.
COMMENTS