Mkurugenzi wa Idara ya Habari, MAELEZO Bw. Hassan Abbas akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu taasisi za S...
Mkurugenzi wa Idara ya Habari, MAELEZO Bw. Hassan Abbas akizungumza na
waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu taasisi za Serikali kutekeleza agizo la
kuhuisha taarifa na huduma katika Tovuti zao mapema kabla ya mwisho wa mwezi huu
katika mkutano uliofanyika Ofisi za Wakala ya Serikali Mtandao (EGA) hivi karibuni
Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Meneja wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa Wakala ya
Serikali Mtandao, Susan Mshakangoto.
Meneja wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa Wakala ya Serikali Mtandao Bibi.
Susan Mshakangoto akifafanua jambo kwa waandishi wa habari wakati wa mkutano na
waandishi hao hivi karibuni jijini Dar es Salaam, kuhusu taasisi za umma kuhuisha
taarifa katika Tovuti zao. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari, MAELEZO, Hassan Abbas.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari, MAELEZO Bw. Hassan Abbas akiwaonyesha
waandishi wa habari mwongozo wa utengenezaji wa Tovuti za Serikali wakati wa
mkutano wake na waandishi hao hivi karibuni Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Meneja wa
Habari, Elimu na Mawasiliano wa Wakala ya Serikali Mtandao, Susan Mshakangoto.
Na Ismail Ngayonga, Dar es Salaam.
SERA
ya Taifa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ya mwaka 2003,
pamoja na mambo mengine inasisitiza umuhimu wa Serikali kutumia fursa
za TEHAMA katika utendaji kazi wa kila siku na utoaji huduma kwa
wananchi.
Katika
kutekeleza sera hiyo, mwaka 2004 Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi
wa Umma (OR-MUU) ilianza kuchukua hatua mbalimbali kuongeza matumizi ya
TEHAMA katika kuimarisha mifumo ya utoaji habari na huduma kwa
wananchi.
Moja
ya maeneo ya TEHAMA ambayo Serikali imewekeza na kupata mafanikio
makubwa ni pamoja na eneo la tovuti ambapo hadi kufikia mwaka 2010
takribani Taasisi zote za Serikali zilikuwa na tovuti.
Katika
kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Tano, kumekuwepo na
mapinduzi makubwa katika mfumo wa upashanaji wa habari na utoaji wa
huduma kwa umma kupitia tovuti.
Mtendaji
Mkuu wa Serikali Mtandao, Dkt. Jabiri Bakari anasema taasisi za umma
zinapaswa kuwa na tovuti zitakazosaidia wananchi kupata kwa urahisi
taarifa zinazohusu shughuli na huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi
hizo.
“Tovuti
za Serikali zinatakiwa kuwa kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza na
mwananchi anapofungua tovuti hizo lugha itakayoonekana kwanza iwe ni
Kiswahili na muda wowote mwananchi huyo anaweza kubadili kwenda kwenye
lugha ya Kiingereza”.
Dkt.
Bakari amesema kuwa Wakala imetoa miongozo ya kusimamia na kuendesha
tovuti hizo na unapatikana kwenye tovuti ya Wakala www.ega.go.tz sehemu
ya Miongozo na Viwango.
Akizungumzia
mafanikio ya Wakala hiyo, Dkt. Jabiri anasema Wakala imetengeneza
mifumo mbalimbali na kuweka miundombinu ya kuwezesha taasisi za umma
kutumia Tehama katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Tovuti
Kuu ya Serikali ni zao la kwanza la Wakala na ilibuniwa na kusanifiwa
na wataalam wa ndani. Katika tovuti hiyo ambayo pia ni mfumo, ina
taarifa za baadhi ya taasisi za umma, sekta mbalimbali na huduma zake
pamoja na balozi zilizoko nchini na zile za kwetu zilizoko nje ya nchi”,
anasema Dkt. Bakari.
Anaongeza
kuwa mfumo mwingine uliotengenezwa na Wakala hiyo ni Tovuti Kuu ya
Ajira ambayo humwezesha mwananchi kuona ajira mbalimbali zinazotangazwa
na Serikali ambapo muombaji wa ajira anaweza kutuma wasifu wake kwa
njia ya mtandao na nafasi zinapotangazwa zenye kuhitaji mtu mwenye sifa
hizo.
Kwa
mujibu wa Dkt Jabiri anasema jitihada mbalimbali zinatekelezwa na
Wakala ili kuwezesha taasisi za umma kutoa huduma zao kwa njia ya
mtandao kwa kuongeza uwezo wa wataalam wa Tehama kwa kuwapa maarifa na
ustadi wa kubuni.
Dkt.
Jabiri anasema Wakala imetoa mafunzo kuhusu usimamizi na Ujenzi wa
Mtandao wa Mawasiliano Serikalini kwa taasisi za umma 149 wakiwemo
Maofisa TEHAMA 226, Mafunzo ya uendeshaji wa Vituo vya data kwa Taasisi
za umma 91 wakiwemo Maofisa TEHAMA 162.
Aidha
Mafunzo ya Usimamizi wa Mfumo wa Barua Pepe Serikalini yametolewa kwa
taasisi 157 pamoja na Mafunzo ya usimamizi wa taarifa tovuti za serikali
yametolewa kwa taasisi 71.
“Mafunzo
ya uwekaji taarifa katika tovuti kuu yametolewa kwa taasisi 86 na
Mafunzo hayo yanaendelea kutolewa kwa kila taasisi ambayo inatengenezewa
Tovuti na Wakala” anasema Dkt. Jabiri.
Kwa
upande wake Meneja Habari, Elimu na Mawasiliano wa Wakala wa Serikali
Mtandao, Suzan Mshakangoto anasema mbali na kuanzisha mtandao huo
Serikali imeziagiza taasisi zote za umma kuhuisha taarifa katika tovuti
zake na Tovuti Kuu ya Serikali (www.tanzania.go.tz).
Anaongeza
kuwa tangu kuanzishwa kwa tovuti hizo kumesaidia kuongeza kasi ya
utendaji, uwazi, ufanisi, uwajibikaji na tija katika utoaji wa taarifa
na huduma kwa wananchi, pamoja na changamoto kadhaa zilizojitokeza
katika usimamizi wa tovuti hizo.
Akifafanua
zaidi anasema miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na tovuti za
taasisi za umma kutokuwa na taarifa mpya na za mara kwa mara, na
kutofuatwa kwa mwongozo uliowekwa unaosisitiza usanifu wa tovuti hizo.
Naye
Mkurugenzi wa Habari, Hassan Abbas anasema ofisi yake kwa kushirikiana
na e-GA tayari imezisaidia Halmashauri 93 kuhuisha taarifa zilizopo
katika tovuti zao ili kuwawezesha wananchi kufahamu huduma mbalimbali
zinazotolewa na Serikali katika maeneo yao.
Abbas
anasema tovuti ni mojawapo ya nyenzo na njia rahisi na ya haraka ya
kutoa taarifa na kufikisha huduma kwa umma kwani miaka ya nyuma taarifa
na huduma za Serikali zilitolewa kwa njia ya kutembelea ofisi husika au
kwa kupitia vyombo vya habari.
Anasema
Serikali imetoa mafunzo kwa Maafisa Habari katika Wizara, Idara, Wakala
na Taasisi mbalimbali jinsi ya kuboresha taarifa katika tovuti zao, na
kuanzia sasa ofisi yake itaanza kufanya tathimini ili kufahamu Wizara
ambazo hazijaanza kuhuisha taarifa zake.
Kwa
mujibu wa Abbas anasema Serikali imekusudia kupanua wigo wa mawasiliano
katika Wizara, Idara, na Taasisi zake kwa kuwahimiza Maafisa Habari
kutumia zaidi mitandao ya kijamii kwa ajili ya kujibu na kutoa ufafanuzi
wa hoja mbalimbali zinazoelekezwa kwa Serikali.
Katika
kuboresha mfumo wa mawasiliano Serikalini, ofisi yake imeanzisha
akaunti ya twitter ya; msemaji wa Serikali@TZ_Msemaji Mkuu ambayo
mwananchi anaweza kuifuata akaunti hiyo kwa kutafuta Msemaji Mkuu wa
Serikali on Twitter.
Anasema
wananchi wengi kwa sasa wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kwa
ajili ya kuendesha mijadala mbalimbali ambayo baadhi yao imekuwa
ikipotosha ukweli kuhusu utelekezaji wa sera mbalimbali za Serikali.
Abbas
anasema jukumu la kuboresha mawasiliano kati ya Serikali na Wananchi ni
suala mtambuka, na hivyo ni wajibu wa Maafisa Habari wa Wizara, Idara,
Taasisi, Wakala za Serikali kutoogopa kutoa taarifa muhimu kwa waandishi
wa habari.
“Waandishi
wa habari wasitoe taarifa zisizofanyiwa utafiti wa kutosha kwa
wananchi, ni vyema sote tushirikiane katika kutoa taarifa sahihi kwa
wananchi kuhusu sera na mikakati ya serikali ili kuleta maisha bora kwa
watanzania wote” anasema Abbas.
Kwa
kutambua umuhimu wa tovuti kama nyenzo kuu ya mawasiliano, Serikali
kupitia Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Umma (PS3) unaofadhiliwa na
shirika la misaada la Marekani iliunda kikosi kazi kwa ajili ya
uhuishaji wa tovuti za Mamlaka ya Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Kikosi
kazi hicho kinahusisha Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,
Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), na
Wakala wa Serikali Mtandao (E-GA).
Msimamizi
wa Mifumo ya Taarifa wa PS3, Bunto Mbozi anasema tovuti nyingi za
TAMISEMI zimetengenezwa, zinasimamiwa na kuendeshwa bila kuwepo na
utaratibu unaofanana, hali hiyo inasababisha uwepo wa tovuti
zisizokidhi viwango na ubora kufuatana na mahitaji ya watumiaji.
Anaongeza
kupitia mradi, PSE3 imekusudia kuhuisha taarifa zote za tovuti za
Serikali, ambapo kwa sasa wataanza na Halmashauri 93 nchini na baadae
katika Wizara, Idara, Taasisi nyingine za Umma.
Bunto
anasema mradi huo ulizinduliwa mapema mwaka huu mkoani Iringa ambapo
hadi kufikia mwezi Agosti mwaka huu, jumla ya mikoa 13 ilifikiwa na
taasisi hiyo na kuendesha mahojiano na Watendaji Wakuu wa Mikoa, Wakuu
wa Idara na vitengo mbalimbali.
Anaitaja mikoa hiyo kuwa ni Iringa, Shinyanga, Dodoma, Mbeya, Mwanza, Kagera, Mara, Rukwa, Kigoma, Lindi, Mtwara na Morogoro.
Akifafanua
zaidi anasema katika utafiti uliofanyika ulibaini kuwa mikoa mingi
ilianza kutengezeza tovuti zao lakini hazikikuwa na taarifa muhimu
zinazohitajika na wananchi wa kawaida.
“Tovuti
ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inatembelewa na watu zaidi ya
500,000 kwa siku, hii inatokana na mahitaji ya huduma inazotoa TRA kwa
wananchi, hivyo mradi huu pia umekusudia kuzifanya tovuti za Mikoa na
Halmashauri kutembelewa na wananchi wengi zaidi” anasema Bunto.
Kwa
mujibu wa Bunto anasema, mradi huo uliichagua TAMISEMI kutokana na Ofisi
hiyo kutoa huduma muhimu zinazomgusa wananchi wa kawaida ikiwemo afya,
maji, elimu, mazingira, uvuvi, ufugaji na kadhalika, ambapo wananchi
wengi wanapenda kufuatilia taarifa na huduma hizo katika ofisi za umma.
Anaongeza
uhuishaji wa taarifa za tovuti utasaidia kutangaza fursa na rasilimali
za kiuchumi zilizopo katika mikoa, hatua itayoziwezesha halmashauri
nyingi kuibua vivutio vya uwekezaji sambamba na kuboresha utoaji huduma
kwa wananchi.
COMMENTS