Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Mawaziri wa Asasi ya Si...

Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na
Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Mhe
Augustine Mahiga yupo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa
ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 10 hadi 13 Oktoba, 2016.
Mhe.
Mahiga ambaye anaongoza ujumbe wa Mawaziri wa Asasi hiyo yupo nchini
humo kwa maagizo ya Mwenyekiti wa Asasi, Mhe. John Pombe Magufuli, Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kutathmini hali ya siasa
ilivyo nchini humo ili kushauri ipasavyo.
Aidha,
tathmini hiyo inafanyika kufuatia hali tete ya kisiasa, kiulinzi na
kiusalama nchini DRC iliyochangiwa na maandamano yaliyofanyika tarehe 19
Septemba, 2016 ambayo yaliandaliwa na vyama vya upinzani kwa lengo la
kushinikiza Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya DRC (CENI) kutangaza tarehe ya
kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu.
Awali
misheni hii ilikuwa ifanye ziara kati ya tarehe 4 na 5 Oktoba, 2016,
lakini kutokana na ziara ya Kitaifa ya Mhe Joseph Kabila, Rais wa
Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo hapa nchini ililazimu kuahirishwa. Aidha,
kufuatia mazungumzo kati ya Mhe Rais John Pombe Joseph Magufuli, na Mhe
Rais Jospeh Kabila wakati wa ziara hiyo walikubaliana Misheni hiyo
ifanye ziara kwa tarehe hizo.
Hadi
sasa Misheni hiyo imeweza kukutana na wadau mbalimbali ambapo
imewasisitiza umuhimu wa kushiriki kwenye mjadala ikiwa ni njia pekee ya
kuweza kuwakwamua hapo walipo pamoja na umuhimu wa uvumilivu wa kisiasa
na hatimaye kufanyika kwa uchaguzi kwa kipindi watakachokuwa
wamekubaliana pamoja.
Wadau
hao ni pamoja na Mabalozi wa Nchi SADC walioko nchini Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo; Mhe. Eden Kodjo, Msuluhishi Mkuu wa Umoja wa
Afrika; Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo;
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Wadau wengine ni Muungano wa
vyama vilivyosusia kushiriki katika mjadala shirikishi wa kitaifa (
Rassamblement); Muungano wa vyama vinavyounda Serikali (Presidential
Majority); Asasi zisizo za kiserikali zinazoshiriki katika mjadala
shirikishi wa kiitaifa; Asasi zisizoshiriki katika mjadala shirikishi wa
kitaifa na Taaisi za kidini.
Itakumbukwa
kuwa, Mkutano wa 36 wa Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya
Maendeleo ya Kusini mwa Afrika uliofanyika Mbabane, Swaziland mwezi
Agosti 2016 ulimteua Mhe. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kuwa Mwenyekiti wa Asasi ya SADC ya Siasa, Ulinzi
na Usalama. Nchi zingine zinazounda Asasi hii ni Angola (Makamu
Mwenyekiti) na Msumbiji (Mwenyekiti anayeondoka).
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 11 Oktoba, 2016.
Mwenyekiti
wa Baraza la Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya
ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Mhe. Balozi Dkt.
Augustine Mahiga (wa sita kushoto) akiongoza kikao cha pamoja cha
Mawaziri kilichofanyika katika Hoteli ya Pullman, Kinshasa, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC). Wengine katika picha upande wa kulia ni
Mabalozi wa Nchi wanachama wa SADC wanaowakilisha nchi zao DRC.
Mhe.
Dkt. Augustine Mahiga (wa tatu kulia) akiongoza ujumbe wa SADC katika
kikao alichokifanya na Mhe. Raymond Tshibanda (wa nne kushoto), Waziri
wa Mambo ya Nje wa DRC ambaye aliongozana na viongozi wa juu wanaoratibu
uchaguzi nchini DRC.
COMMENTS