WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema mabasi yaendayo kasi (DART) yataanza kufanyiwa majaribio ndani wiki moja kuanzia sasa ili madereva ...
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema mabasi yaendayo kasi (DART) yataanza kufanyiwa
majaribio ndani wiki moja kuanzia sasa ili madereva waanze kuzoea njia na taa
za kuongozea magari.
“Wataanza
na mabasi kati ya 30 – 50 ambayo yatapita kwenye njia zote za mradi huo. Zoezi
hilo litafanyika ili watumiaji wengine wakiwemo waendesha daladala, bodaboda na
watembea kwa miguu waweze kutambua kuwa njia ya mabasi yaendayo kasi si ya kwao,
hivyo waanze kuzoea,” alisema.
Ametoa
kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Machi 22, 2016) wakati alipofanya ziara ya
ghafla katika Soko la Kimataifa la Samaki la Feri iliyokuwa na lengo la
kuangalia mfumo wa majiko ya gesi sokoni hapo na kukagua ujenzi wa ukuta unaotenganisha
soko hilo na mabasi yaendayo kasi.
Waziri
Mkuu ambaye ametembelea soko hilo kuanzia saa 5:10 hadi saa 5:54, alitoa jibu
hilo wakati akijibu maombi ya mfanyabiashara mmoja, Bw. Sharifu Ramadhani
ambaye alisema wanatumia fedha nyingi kwa ajili ya usafiri kwa vile mabasi
mengi yanaishia Mnazi Mmoja. “Mabasi yanaishia Mnazi Mmoja na huku ni mbali kwa
hiyo tunalazimika kutembea kwa miguu kwa sababu kukodi taxi ni gharama kubwa,”
alisema.
Akifafanua
kuhusu hatua iliyofikiwa kwenye utekelezaji wa mradi huo, Waziri Mkuu alisema: “Hivi
sasa wanakamilisha ufungaji wa mitambo ya kukatia tiketi ambapo abiria atakuwa
na kadi kama za benki ambayo anaijaza fedha halafu anapita kwenye mashine, kiasi
cha nauli kinakatwa halafu anaingia kwenye basi, hakutakuwa na muda wa kukata
tiketi.”
Alisema
tatizo la usafiri kwa wafanyabiasha wa feri litakwisha hivi karibuni baada ya mabasi
hayo kuanza.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
JUMANNE, MACHI 22, 2016.
COMMENTS