Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard K. Membe (Mb) akisalimiana na Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kag...
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa Mhe. Bernard K. Membe (Mb) akisalimiana na Rais wa Rwanda Mhe. Paul
Kagame alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam. Mhe. Rais Kagame yupo nchini kwa ajili ya kushiriki
Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Ukanda wa Kati kuhusu Uwekezaji na Viwanda
unaofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Rais Kagame akipokea shada la maua kutoka kwa mtoto Elizabeth Jackson kama ishara ya kumkaribisha nchini Tanzania.
Rais Kagame akipokea kwa heshima alipowasili uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Dar es Salaam leo.
Rais Kagame na Waziri Membe wakiangalia burudani ya ngoma za asili uwanjani hapo.
Waziri
Membe akiwa ameongozana na Rais Kagame mara baada ya kuburudika na ngoma za asili. (Picha na Reginald Philip)
Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Rais Paul Kagame wa Rwanda wakiteta jambo walipotembelea bandari ya Dar es Salaam leo Machi 26, 2015. |
Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Rais Paul Kagame wa Rwanda wakiteta jambo walipotembelea bandari ya Dar es Salaam leo Machi 26, 2015. |
Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Rais Paul Kagame wa Rwanda wakiteta jambo walipotembelea bandari ya Dar es Salaam leo Machi 26, 2015. |
*****************
THE UNITED REPUBLIC
OF TANZANIA
DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512,
2116898
E-mail: ikulucommpress@googlemail.com
Website : www.ikulu.go.tz
Fax: 255-22-2113425 |
|
PRESIDENT’S OFFICE,
STATE
HOUSE,
1 BARACK OBAMA ROAD,
11400
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na mgeni wake, Rais Paul Kagame wa
Rwanda, leo, Alhamisi, Machi 26, 2015, wametembelea Bandari ya Dar es Salaam na
baadaye Rais Kagame ameanzisha safari ya treni maalum za kusafirisha mizigo ya
Rwanda kutoka Tanzania.
Rais Kagame amewasili nchini asubuhi
ya leo na kufungua Mkutano wa Wawekezaji katikaUjenzi wa Miundombinu Ukanda wa
Kati (High Level Investors Forum –
Central Corridor Development Acceleration Programme) uliofanyika kwenye
Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere mjini Dar es Salaam.
Mara baada ya hotuba ya ufunguzi
na kipindi cha maswali kutoka kwa washiriki na majibu kutoka kwa viongozi wa
nchi tano zinazounda Shirika la Uwezeshaji wa Usafiri wa Ukanda wa Kati (The Central Corridor Transit Transport
Facilitation Agency (CCTTFA), viongozi hao wawili wamekwenda Bandari ya Dar
es Salaam.
CCTTFA lilianzishwa Septemba 2,
mwaka 2006, na Makubaliano yaliyotiwa saini na nchi tano ambazo zinanufaika na
usafiri wa Ukanda wa Kati – Tanzania, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo
(DRC), Rwanda na Uganda.
Katika Bandari ya Dar es Salaam,
Rais Kagame na mwenyeji wake wameanza kwa kutembelea ofisi mpya za Mpango wa
Ukusanyaji Ushuru kwa Pamoja (Single
Customs Territory) miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC), mpango ulioanza kutumika Julai mwaka jana, 2014. Chini ya
Mpango huo, kila nchi inashughulikia mizigo yake yenyewe, ikiwa ni pamoja na
kukusanya kodi yake.
Rais Kagame na mwenyeji wake
wametembelea ofisi za Mamlaka ya Kodi ya Rwanda (RRA) na Mamlaka ya Kodi ya DRC
ambako walipewa maelezo kuhusu faida za mpango huo.
Miongoni mwa mambo mengine,
marais hao walielezwa kuwa chini ya Mpango huo, waagizaji wa mizigo ya Rwanda,
kupitia Bandari ya Dar es Salaam, sasa wanajaza fomu moja tu badala ya tatu na
sasa mizigo ya Rwanda inachukua siku mbili tu kutoka Bandari ya Dar es Salaam
hadi Kigali, badala ya siku kati ya tano na 10 kabla ya kuanzishwa Mpango huo.
Nchi ambazo tayari zimefungua
ofisi zao katika Bandari hiyo kutekeleza Mpango huo ni Tanzania yenyewe, Burundi,
DRC na Rwanda. Uganda inakamilisha maandalizi ya utekelezaji na Zambia
imeonyesha nia ya kujiunga na Mpango huo, kwa sababu inapitishia mizigo yake
katika Bandari ya Dar es Salaam, hata kama siyo mwanachama wa EAC.
Kutoka kwa ofisi za Single Customs Territory, viongozi hao
wamekwenda kwenye Bandari ya Dar es Salaam ambako wamepatiwa maelezo kuhusu
jinsi utendaji wa Bandari hiyo ulivyoboreka katika miaka miwili iliyopita.
Aidha, viongozi hao wameelezwa
jinsi gani pia utendaji wa kampuni binafsi ya upakiaji na upakuaji mizigo ya
TICTS inavyofanya kazi na ilivyoboresha utendaji wake katika sehemu nne za meli
kutia nanga (berths) ambako
inafanyia kazi yake katika Bandari hiyo yenye sehemu 11 za kupakia na kupakulia
mizigo.
Katika Bandari hiyo, marais hao
wameelezwa kuwa katika miaka mitano iliyopita, kiwango cha mizigo inayopitia
katika Bandari hiyo kimekuwa kinaongezeka kwa wastani wa asilimia 12.8 kila
mwaka.
Wameelezwa pia kuwa mwaka jana,
kiasi cha tani milioni 14.6 ya mizigo kilipitia katika Bandari hiyo zikiwemo
kontena 621,000 na kuwa kati ya mizigo hiyo kiasi cha asilimia 34, sawa na
mizigo tani milioni 5.020 ilikuwa mizigo kwa ajili ya nchi za jirani.
Aidha, viongozi hao wameelezwa
kuwa muda wa kontena kukaa Bandarini hapo sasa ni siku tisa tu badala ya siku
21 Februari mwaka 2008, muda wa meli kukaa nje ya Bandari ikisubiri kuingia
Bandarini ili ipakuliwe, sasa ni siku moja unusu badala ya siku tatu unusu za
mwaka 2013.
Marais Kagame na Kikwete pia
wameelezwa kuwa usalama wa mizigo ya waagizaji sasa umeongezeka mno, kiasi cha
kwamba halijakuwepo tukio hata moja la wizi wa mizigo ya wateja yakiwemo magari
na spea zake kwa miaka mitatu mfululizo sasa.
Bandari ya Dar es Salaam ambayo
huhudumia mizigo ya nchi saba – ya Tanzania yenyewe, Malawi, Zambia, DRC,
Burundi, Rwanda na Uganda pia huendesha Bandari kwenye maziwa makuu ya
Victoria, Tanganyika na Nyasa.
Jana, Jumatano, Machi 25, 2015,
Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi pamoja na wawakilishi wa nchi za DRC na
Uganda pia walianzisha safari za treni za namna hiyo kwenda katika nchi zao.
Rais Kagame ameondoka nchini
kurejea kwao leo baada ya kuanzisha safari hizo na mkutano wenyewe kuhusu
Ukanda wa Kati, ambao pia ulihudhuriwa na Rais Yoweri Museveni wa Uganda,
umemalizika jioni ya leo.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais,
Ikulu
– Dar es Salaam.
26 Machi, 2015
COMMENTS