Spika wa bunge mstaafu, Samuel Sitta, au kama alivyojiita "Mzee wa Speed na Viwango" amefariki du...
Spika wa bunge mstaafu, Samuel Sitta,
au kama alivyojiita "Mzee wa Speed na Viwango" amefariki dunia usiku wa
kuamkia leo akiwa nchini Ujerumani alikopelekwa kupatiwa matibabu.
Taarifa iliyotolewa na mwanaye Benjamin Sitta, ambaye ni Meya wa
Manispaa ya Kinondoni, mapema leo aimethibitisha kifo cha Mzee Sitta.
Tayari Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe
Magufuli, amemtumia salamu za rambirambi spika wa bunge Job Ndugai,
kufuatia kifo cha mzee Sitta. Kwa muda mrefu Samuel Sitta ambaye aliwahi
kutumikia nyadhifa mbalimbali tangu serikali ya awamu ya kwanza,
alikuwa haonekani hadharani kutokana na kuugua. Ni miezi michache
iliyopita Mzee Sitta alikuwa akionekana kwenye vyombo vya habari
akitembeelwa na viongozi mbalimbali kumjulia hali. Mungu aiweke roho ya
marehemu mahali pema peponi AMIN.
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU
Simu: 255-22-2114512, 2116898
E-mail: press@ikulu.go.tz
Faksi: 255-22-2113425 |
OFISI YA RAIS,
IKULU,
1 BARABARA YA BARACK OBAMA,
11400 DAR ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia
salamu za rambirambi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Job Ndugai kufuatia kifo cha Spika Mstaafu na Mbunge Mstaafu wa
Jimbo la Urambo lililopo Mkoani Tabora Mhe. Samwel Sitta.
Mhe.
Samuel Sitta amefariki dunia usiku wa kuamkia leo katika hospitali ya
Technical University of Munich nchini Ujerumani alikokuwa akipatiwa
matibabu tangu mwezi uliopita.
Katika
salamu hizo, Rais Magufuli amesema amepokea kwa mshtuko na masikitiko
makubwa taarifa za kifo cha Mhe. Samwel Sitta na kwamba Taifa
limempoteza mtu muhimu aliyetoa mchango mkubwa katika uongozi na
maendeleo.
“Nitamkumbuka
Mzee Sitta kwa uchapakazi wake, uzalendo wake na tabia yake ya
kusimamia ukweli katika kipindi chote alichokuwa kiongozi katika ngazi
mbalimbali za siasa na Serikali.
“Kupitia
kwako Mhe. Spika naomba kutoa pole nyingi kwa Mke wa Marehemu Mhe.
Magreth Sitta ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Urambo na familia nzima ya
marehemu, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wananchi
wa Urambo Mkoani Tabora na watu wote walioguswa na msiba huu” amesema Rais Magufuli katika salamu hizo.
Dkt.
Magufuli amesema anaungana na wafiwa wote katika kipindi hiki kigumu
cha maombolezo na amewaombea moyo wa uvumilivu na ustahimilivu.
“Namuomba Mwenyezi Mungu aiweke roho ya Marehemu mahali pema peponi, Ameni”
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
07 Novemba, 2016
Samuel Sitta akiwa na mkewe, Mama Margaret Sitta wakati wa uhai wake.
Spika Sitta, akipokea ripoti maarufu ya
Richmond, kutoka kwa mwenyekiti wa kamati teule, Dkt. Harrison
Mwakyembe. Ripoti hii ilimuondoa madarakani aliyekuwa Waziri Mkuu wakati
wa kuingia kwa serikali ya awamu ya nne, Mh. Edward Lowassa.
Mzee Sitta alikuwa rafiki wa kila mtu. Hapa akiwa na Mbunge Tundu Lissu kutoka CHADEMA.
Spika Samuel Sitta, akila kiapo cha kushika uspika wa bunge, mwanzoni mwa serikali ya awamu ya nne.
COMMENTS