Siasa

Sunday, December 4, 2016
 Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Fedha (TRA), Anna Mndeme kulia akipokea tuzo ya utunzaji bora wa mahesabu kwa taasisi za umma  kutoka kwa Mwakilishi wa Mhasibu Mkuu wa Serikali  Bw .Shogolo Msangi katikati  wakati wa sherehe za kukabidhi tuzo hizo kwa  wawasilishaji bora wa mapato kwa mwaka 2015 yaliyofanyika nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam wa kwana kushoto ni Mwenyekiti wa NBAA Prof. Isaya Jairo.
 
 
 
 Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) Dkt. Ayoub Rioba akipokea tuzo ya utunzaji bora wa mahesabu kwa taasisi za umma baada kuwa mshindi wa pili kutoka kwa kwa Mwakilishi wa Mhasibu Mkuu wa Serikali, Shogolo Msangi wakati wa sherehe za kukabidhi tuzo hizo kwa  wawasilishaji bora wa mapato kwa mwaka 2015 yaliyofanyika nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
 
 
 Afisa Mkuu wa Mapato kutoka kampuni ya kutengeneza cement (Tanga Cement Plc) Pieter De Jager akiwa na tuzo ya washindi wa jumla kwenye mashindano ya wawasilishaji bora wa mapato kwa mwaka 2015 yaliyofanyika nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

 Mwakilishi wa Mhasibu Mkuu wa Serikali, Shogolo Msangi (katikati waliokaa)  akiwa katika picha ya pamoja na washindi wa uwasilishaji bora wa mapato  wakati wa sherehe za kukabidhi tuzo hizo kwa mwaka 2015 iliyofanyika nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam. (Picha Na Ally Daud-Maelezo)
Na Ally Daud-MAELEZO
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imeshinda tuzo ya utunzaji bora wa mahesabu kwa taasisi za umma  zilizoandaliwa na   Bodi ya Ukaguzi na Wahasibu (NBAA) kwa mwaka 2015. 
Akipokea tuzo hiyo Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Fedha (TRA) Bi. Anna Mndeme amesema kuwa wamepata tuzo hiyo kutokana na  kuwasilisha vizuri mahesabu ya mwaka wa fedha yaliyowasilishwa kufuatana na viwango vya uwasilishwaji  vinavyozingatiwa na Bodi ya Ukaguzi na Wahasibu (NBAA).
“Tumefanya vizuri na tumepata tuzo kwa kushika nafasi ya kwanza kutokana na  kuwasilisha vizuri mahesabu ya mwaka wa fedha yaliyowasilishwa kufuatana na viwango vya uwasilishwaji  vinavyozingatiwa na Bodi ya Ukaguzi na Wahasibu (NBAA)” alisema Bi. Mndeme.
Aidha Bi. Mndeme amesema kuwa tuzo hiyo ni chachu kwa TRA itayofanya waendelee kujituma zaidi katika ukusanyaji na utunzaji wa mapato ili kusaidia nchi kupata huduma bora za jamii kwa maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi TRA Bw. Richard Kayombo amesema kuwa huo ni uthibitisho kwamba TRA inafanya kazi  kwa ueledi na uwazi kupelekea kupata tuzo ya heshima.
Katika mashindano hayo Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) wameibuka washindi wa pili huku kampuni inayotengeneza Sementi  (Tanga Cement Plc) wakiibuka kuwa washindi wa jumla kwenye tuzo hizo .

Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi, Mhe. Cleopa Msuya (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wengine waliohudhuria kwenye mahafali ya 10 ya chuo hicho akiwemo Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho, Prof, Evelyne Ambede (wa pili kushoto), wa tatu kulia ni Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhandisi Stella Manyanya. Mahafali hayo yamefanyika jana Jijini Dar es Salaam katika viwanja vya chuo hicho.
     Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Chuo Kikuu Ardhi kimekamilisha ujenzi na uwekaji wa vifaa katika Bandari ya Tanga ikiwa ni moja ya miradi ya kiutafiti inayofanywa chuoni hapo kwa ajili ya kupima hali halisi ya bahari.
Makamu wa Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Idrissa Mshoro ameyasema hayo alipokuwa akisoma hotuba wakati wa mahafali ya 10 ya chuo hicho yaliyofanyika jana chuoni hapo jijini Dar es Salaam.
Prof. Mshoro amesema kuwa pamoja na jukumu la kutoa wahitimu katika fani mbalimbali kwa maendeleo ya nchi pia chuo hicho kina majukumu ya kufanya utafiti na kutoa ushauri wa kitaalam hivyo kupitia Mradi wa Utafiti wa Mabadiliko ya Tabia Nchi uliofadhiliwa na Serikali ya Norway kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania umeweza kufanikisha ujenzi huo.
“Madhumuni ya Mradi huu ni kusaidia kuboresha mawasiliano kati ya Bandari na watumiaji wake kwani taarifa sahihi zitakazotolewa kuhusu hali halisi ya bahari zitasaidia kufanya maamuzi sahihi ya kutumia Bandari hiyo pia, taarifa hizo zitakuwa msaada mkubwa kwa wadau wengine kama wavuvi, watalii pamoja na watafiti mbalimbali,” alisema Prof. Mshoro.
Ameongeza kuwa katika kutoa ushauri na huduma za kitaalam, chuo kimetekeleza miradi mbalimbali ya Serikali, taasisi za Umma na Binafsi katika fani zote zinazofundishwa chuoni hapo hivyo kusaidia katika kuongeza kipato cha chuo kwa ajili ya miradi, kutoa motisha kwa wafanyakazi pamoja na kutoa fursa kwa wana taaluma kupata uzoefu kwa vitendo katika fani mbalimbali walizosomea. 
Aidha, Prof. Mshoro ameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuendelea kukipatia chuo fedha na misaada mingine kwa ajili ya kuendeshea shughuli za chuo ambapo kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali imetengea jumla ya shilingi bilioni 5 kwa ajili ya bajeti ya maendeleo ya chuo hicho.
Akiongelea kuhusu wahitimu, Prof.  Mshoro amefafanua kuwa jumla ya wanafunzi 968 watatunukiwa shahada na stashahada mbalimbali ambapo wanafunzi 868 watatunukiwa shahada za awali, 80 shahada za uzamili, 14 watatunukiwa stashahada pamoja na shahada za uzamivu kwa wanafunzi 6.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhandisi Stella Manyanya amesema kuwa bado kuna changamoto kubwa kwa wasichana kujiunga na masomo ya sayansi kwani idadi imeonyesha kuwa wahitimu wa kike ni 320 ambayo ni sawa na asilimia 33 ya wanafunzi wote hivyo ametoa rai kwa wasichana kutumia fursa za kusomea masomo hayo bila kuogopa.
Mhandisi Manyanya amewashauri vijana kujikita kusoma masomo yatakayowapelekea kujiajiri wenyewe kuliko yale yanayohitaji kuajiriwa kwani njia hiyo itasaidia kujikwamua kiuchumi kwa haraka na kuchangia katika maendeleo ya taifa.

 Jeneza lililokuwa na mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kundi la Yanga Asili, marehemu Yusuf Mzimba nyumbani kwa mtoto wake Magomeni jijini Dar es Salaam, kabla ya kusafirishwa kwa mazishi katika kijiji cha Msoga, Chalinze mkoani Pwani. (Picha na Francis Dande).
 Mchezaji wa zamani wa timu ya Yanga na  Taifa Stars,  Abeid Mziba (kushoto), akimfariji Ramadhan Yusuf 'Kampira' ambaye ni mtoto wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kundi la Yanga Asili, marehemu Yusuf  Mzimba jijini Dar es Salaam jana, kabla ya mwili wake kusafirishwa kwa mazishi Msoga, Chalinze Mkoa wa Pwani. 

Mzee Ibrahim Akilimali (kushoto), akifurahia jambo na wazee wenzake katika msiba wa mzee Yusuf Mzimba. Katikati ni Said Motisha.
 Kisomo kikisomwa.
 Mzee Ibrahim Akilimali akisoma wasifu wa marehemu Yusuf Mzimba.
 Wakiombea Dua mwili wa marehemu.
 Safari ya kuelekea Msoga ikianza.

NA FRANCIS DANDE
 MAMIA ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam, jana walijitokeza kwa wingi kuaga mwili aliyekuwa Mwenyekiti wa Kundi la Yanga Asili, marehemu Yusuf Mzimba, uliosafirishwa kutoka nyumbani kwa mtoto wake, Ramadhan Yusuf ‘Kampira’, Magomeni jijini Dar es Salaam leo.
Marehemu alifariki juzi na amezikwa jana katika makaburi ya familia yaliyopo kijijini kwake, Msoga, Chalinze, mkoani Pwani.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mtoto wa marehemu mzee Mzimba, Kampira alisema kuwa baba yake  alikuwa anasumbuliwa na maradhi kwa muda mrefu na kwamba ameacha watoto sita.
Kampira aliongeza kuwa, Rais mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Kikwete ataongoza waombolezaji katika maziko hayo, yatakayofanyika katika makaburi ya familia yaliyopo kijijini Msoga.
Akisoma wasifu wa marehemu, Mzee Ibrahim Akilimani alisema kwamba marehemu alikuwa mwanachama wa siku nyingi wa Yanga na amewahi kushika nyadhifa mbalimbali katika klabu ya Yanga ikiwemo nafasi ya umeneja.
Alibainisha ya kuwa, Mzee Mzimba aliwahi pia kuwa Katibu Mwenezi wa Yanga na mtu ambaye alikuwa na misimamo katika kuipenda Yanga na hakubadilika katika kuitetea klabu yake ya Yanga. 
Pia alitoa mchango mkubwa ndani ya Yanga na hasa ulipotokea mgawanyiko mkubwa uliodumu kwa miaka 7 na kuibuka makundi ya Yanga Asili na Yanga Kampuni. 
Mzee Akilimali aliongeza kwamba, licha ya kuibuka kwa migogolo ndani ya klabu hiyo, lakini Mzee Mzimba alibaki na msimamo wake mpaka leo na kuwa Yanga kitu kimoja.
“Mtu kama Yusuf Mzimba alivyokuwa maarufu kwa Yanga leo hebu nitazamieni hao viongozi wa Yanga wako wapi, tumeondokewa na wapenzi wa Yanga kama Ismail Idrissa, Bilal Hemed Chakupewa hakuonekana hata kiongozi hata mmoja, naamini hata Ibrahim Akilimali akifa, hatoonekana kiongozi yeyote wa Yanga,” alisema.
Mzee akilimali alisema kuwa Yanga ilianzishwa na wazee mwaka 1935 ikiwa na lengo la kujuana, kuzikana, kusaidiana kufurahi pamoja, lakini leo imekuwa hawajuani. 
Aidha amewasihi wana Yanga kutopoteza adhima ya kuanzishwa kwa klabu hiyo.
Naye mchezaji wa zamani wa Taifa Stars na Yanga, Abeid Mziba alisema kuwa: “Katika miaka ya 80 wakati najiunga na Yanga, Mzee Mzimba ni miongoni mwa wazee walionipokea, kwa kweli tumepoteza nguzo muhimu sana ndani ya Yanga na katika familia ya mpira kwa ujumla.”
Naye Mzee wa Yanga, Hashim Mhika alisema kuwa alimfahamu siku nyingi mzee Mzimba kutokana na misimamo yake pia alisema kuwa katika serikali ya Kikoloni, Mzee Mzimba aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya (DC), lakini, ameshangazwa kuona hata viongozi wa serikali hawakuonekana katika msiba huo.WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Charles Tizeba kufanya uchunguzi kwa nini mbolea ya minjingu inayozalishwa nchini haitumiki na badala yake inaagizwa mbolea kutoka nje ya nchi.
Ametoa agizo hilo jana (Jumamosi, Desemba 3, 2016) wakati alipotembelea kiwanda cha Fibre Board 2000 Limited ambacho kinatengeneza bidhaa mbalimbali ikiwemo mbolea ya Minjingu, wakati akiwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi mkoani Arusha.Alisema mbolea hiyo licha ya kuwa na viwango vya ubora vinavyohitajika, haitumiki nchini kwa sababu ya kuingiliwa na masuala ya kisiasa dhidi ya matumizi yake.
“Nchi jirani ya Kenya inaiona mbolea hii bora kuliko sisi wa ndani? Mheshimiwa Waziri wa Kilimo are we serious? Tunazalisha mbolea hapa tunasema haina kiwango lakini Kenya wanaitaka na wameagiza tani 300,000,” alisema.
Waziri Mkuu aliongeza kuwa “Jambo hili lazima liangaliwe ndani ya Wizara kwa nini mnaagiza mbolea kutoka nje wakati ndani tunazalisha hii ni mianya ya rushwa, rushwa ulaji ulaji tu. Waziri lichukulie maanani jambo hili hatutaki siasa katika sekta ya kilimo,”.Alisema kumekuwa na mijadala mingi kuhusu mbolea ya minjingu kumbe baadhi ya watendaji wanatengeneza mianya ya kwenda kununua mbolea nje ambako hutumia fedha nyingi ambazo zingeweza kutumika katika miradi mingine ya maendeleo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kiwanda cha Fibre Board 2000 Limited, Tosk Hansi  amesema kampuni hiyo inayozalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo mbolea ya minjingu, imetoa ajira kwa watu zaidi ya 1,800 wengi wao wakiwa ni vijana ila inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ya urasimu wakati wanapoomba vibali vya uvunaji mazao ya misitu.
Awali, kampuni hiyo ya Fibre Board 2000 limited imemkabidhi Waziri Mkuu mchango wa madawati 1,000 kwa ajili ya shule mbalimbali za mkoani Arusha ili kuwawezesha wanafunzi kusoma katika mazingira mazuri.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMAPILI, DESEMBA 4, 2016.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati ufunguzi wa mkutano wa Wadau wa kuendeleza maeneo Tengefu ya Viwanda vya Usindikaji Vyakula uliofanyika kwenye ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati ufunguzi wa mkutano wa Wadau wa kuendeleza maeneo Tengefu ya Viwanda vya Usindikaji Vyakula uliofanyika kwenye ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam ambapo aliwapongeza TAFOPA kwa kazi nzuri wanayoifanya lakini pia aliwataka Wasindikaji kuongeza ushirikiano ili kufikia maendeleo na mafanikio ya juu.
Wadau waliohudhuria na kushiriki wakimsikiliza kwa makini Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati ufunguzi wa mkutano wa Wadau wa kuendeleza maeneo Tengefu ya Viwanda vya Usindikaji Vyakula uliofanyika kwenye ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam. 
 
 
 
Mwenyekiti wa TAFOPA Bi. Suzy Laizer akihutubia wakati ufunguzi wa mkutano wa Wadau wa kuendeleza maeneo Tengefu ya Viwanda vya Usindikaji Vyakula uliofanyika kwenye ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam, mgeni rasmi kwenye mkutano huu alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.
 
 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiangalia bidhaa mbalimbali za vyakula vilivyosindikwa zinazotengenezwa na wajasiriamali muda mfupi kabla ya kufungua wa mkutano wa Wadau wa kuendeleza maeneo Tengefu ya Viwanda vya Usindikaji Vyakula uliofanyika kwenye ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.

.................................................................

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema Serikali ipo mbioni kupunguza muda wa utoaji wa leseni za biashara nchini ili kutoa fursa kwa wananchi wengi zaidi kupata leseni hizo kwa ajili ya shughuli za kibiashara.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere wakati anafungua mkutano wa wadau wa kuendeleza maeneo tengefu ya viwanda vya usindikaji wa vyakula nchini.
Makamu wa Rais amesema mpango utaenda pamoja na kupunguza baadhi ya kodi na tozo ambazo ni kero kwa wananchi hasa wenye viwanda kama hatua ya kukuza biashara na uwekezaji katika sekta ya viwanda nchini.

Amesisitiza kuwa Serikali inaendelea na mazungumzo na wenye mabenki hususani benki ya TIB ili kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa wawekezaji wenye nia ya kuanzisha viwanda.
Kuhusu usindikaji wa bidhaa nchini, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Mjumbe katika jopo la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa la kumuwezesha mwanamke kiuchumi akiwakilisha nchi za ukanda wa Kusini na Mashariki mwa Afrika amepongeza jitihada zinazofanywa na wasindikaji wadogo nchini katika utengenezaji wa bidhaa mbalimbali ambazo zitakidhi katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

“Serikali inafarijika sana kuona kuwa wasindikaji wadogo nchini wamethubutu na wana uwezo wa ushindani katika biashara ya ndani na hata nje, hivyo tunayohaki ya kujigamba kwa kuthubutu, Tumeweza na Tuendelea Kusonga mbele

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema umefika wakati kwa Wizara na taasisi za Serikali na wadau wa maendeleo kuona umuhimu wa kuhakikisha viwanda vinajengwa vijijini ili mkulima mdogo anapolima awe na uhakika wa kupata soko katika viwanda hivyo.
Amesema kuwa hali hiyo itaondoa changamoto ya kusafirisha bidhaa nyingi ambazo zinaharibika njiani au zinapofika sokoni na hivyo kukosesha jamii kipato kilichotarajiwa.
Makamu wa Rais pia amehimiza watafiti nchini wajielekeza katika kufanya tafiti ambazo zitasaidia sekta binafsi na serikali kwa ujumla kuhusu namna bora ya kukuza sekta ya viwanda nchini.
Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda,Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage amekiri kuwa bado kuna changamoto kubwa ya maeneo ya yatakayojengwa viwanda na kwamba Serikali imeliona tatizo hilo na inalifanyia kazi ambapo tayari imeshaziagiza Halmashauri zote nchini kujenga maeneo kwa ajili ya viwanda.