Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TenMeT), Bi. Cathleen Sekwao akizungumza kufungua katika kikao cha wadau wa elimu jijini Dar es Sala...
Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TenMeT), Bi. Cathleen Sekwao akizungumza kufungua katika kikao cha wadau wa elimu jijini Dar es Salaam kujadili namna ya kutekeleza mradi wa kusaidia maboresho ya elimu kwa makazi yenye msongamano wa watu mkoani Dar es Salaam.
MTANDAO wa Elimu Tanzania (TENMET) kwa kushirikiana na African Population and Health Research Center (APHRC) umekutana na wadau wa elimu jijini Dar es Salaam kujadili namna ya kutekeleza mradi wa kusaidia maboresho ya elimu kwa makazi yenye msongamano wa watu mkoani Dar es Salaam.
Akizungumza katika kikao hicho cha majadiliano kilichoshirikisha viongozi kama wabunge, madiwani wa maeneo hayo pamoja na watendaji wa sekta ya elimu, Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TenMeT), Bi. Cathleen Sekwao alisema kikao hicho kinajadiliana namna ya kutekeleza mradi huo utakao lenga kuboresha elimu.
Akifafanua zaidi, Bi. Sekwao alisema kikao hicho kitaangalia matatizo gani kielimu yanayowakwaza watoto wanaoishi katika miji na majiji yenye msongamano wa makazi kiujumla na kuangalia namna wanaweza kukabiliana nayo. Alisema mradi huo utakuwa wa miaka miwili lakini baadaye unaweza kuwa endelevu kadri ya mahitaji yake kwa jamii husika.
Akichangia katika kikao hicho, Mthibiti Ubora wa Shule Wilaya za Temeke na Kigamboni, Mashaka Munjalloh alisema mradi huo utawasaidia watoto kutoka maeneo yenye msongamano kupata elimu bora itakaowasaidia katika maisha yao.
Alisema kutokana na msongamano wa makazi na idadi ya watu mijini yapo maeneo kama Manzese, Tandale, Buguruni, Temeke na Kigamboni yameathiriwa kwa watoto kusoma huku wakikabiliwa na changamoto za msongamano, kwa kile kutopata vifaa vya kufundishia na kujifunzia vikiwemo vitabu na madaftari kutokana na shule zao kuelemewa.
Kwa kuanzia kikao kiliangalia changamoto mbalimbali zinazowakabili watoto na elimu inayotolewa katika maeneo ya miji yenye msongamano kwa kuanzia na Jiji la Dar es Salaam, mradi huo pia unaweza kuendelezwa katika miji ya mikoa mingine hapo baadaye.
COMMENTS