TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kuwa katika uchaguzi mdogo wa madiwani utakaofanyika Novemba 26, 2017 katika kata 43 uta...
TUME
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kuwa katika uchaguzi mdogo wa madiwani utakaofanyika
Novemba 26, 2017 katika kata 43 utagharimu kiasi cha Sh bilioni 2.5.
Mkurugenzi
wa Uchaguzi wa NEC Kailima Ramadhani, alisema msingi wa bajeti ya uchaguzi unategemea
idadi ya vituo vya kupigia kura na idadi ya wapiga kura walioandikishwa katika
kata husika. Amesema idadi ya Wapiga Kura ndio inatoa bajeti ya mahitaji ya
vifaa vya kuendeshea uchaguzi kama karatasi za kura pamoja na idadi ya vituo ambavyo vinakuwa na watumishi wasiopungua
wanne. Kailima alitoa mfano kwamba Kata yenye vituo 41 ina bajeti kubwa kuliko Kata
yenye vituo vikubwa.
Alisema
katika kituo cha kupigia kura kina watendaji wanne ambao ni Msimamizi na
Msimamizi Msaidizi, karani mwongozaji na mlinzi wa kituo “lakini pia kuna watu
wa ziada kama Wasimamizi Wasaidizi wako ngazi ya kata na jimbo ambao wanahusika
kusimamia zoezi la Uchaguzi katika maeneo husika.
Alifafanua
kuwa gharama nyingine za uchaguzi ziko kwenye usafirishaji wa vifaa kutoka Tume
kwenda kwenye Halmashauri husika na kutoka Halmashauri kwenda kwenye kata
ambako uchaguzi unafanyika. Gharama hizo
pia zanahusu utoaji wa Elimu ya Mpiga Kura kupitia machapisho mbalimbali ya
Elimu ya Mpiga Kura, Maelekezo mbalimbali kwa Watendaji wa Uchaguzi n.k.
Elimu
hiyo pia hutolewa kupitia Vyombo vya Habari pamoja na machapisho mbalimbali yatakayotumika
kwa ajili ya kutoa elimu ya mpiga kura.
“Kwenye
uchaguzi huu mdogo bajeti yetu ni Sh bilioni 2.5. Sio kwamba kila kata itatumia
gharama sawa za fedha hizi, bali kuna kata itatumia milioni 20 kutokana na
idadi ya vituo vya kupigia kura kuwa vichache na kata yenye vituo vingi kwenye
uchaguzi huu itatumia Sh milioni 150,” alisema Kailima.
Tume
pia imeviasa Vyama vya Siasa vinavyohusika kwenye uchaguzi mdogo wa madiwani
kutekeleza maadili ya uchaguzi ya 2015 waliyokubaliana kuyafuata na ameonya
kuwa chama au mgombea atakayekika maadili hayo atachukuliwa hatua kama
ilivyoanishwa kwenye maadili hayo ya uchaguzi.
Mkurugenzi
huyo amesema Vyama vya Siasa vinatakiwa kuhakikisha vinawaelemisha wafuasi,Wapenzi
na Wananchama wao juu ya kutekeleza maadili hayo katika kipindi chote cha
kampeni. Alisisitiza kuwa iwapo wafuasi wa vyama vya siasa watakikua maadili
hayo, chama husika pamoja na mgombea wake watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Alitaja
baadhi ya vitendo vya kuvunja maadili ya uchaguzi ni kuchana mabango ya
wagombea, kutoa lugha chafu wakati wa mikutano ya kampeni pamoja na kupitisha
muda wa kufanya mikutano ya kampeni.
Alisisitiza
kamati za maadili za kata na jimbo kuchukua hatua kali kwa chama au mgombea
ambaye atakikuka maadili hayo. Alisema kamati hizo zinatakiwa kuchukua hatua
ndani ya saa 48 mara chama au mgombea anapovunja maadili.
Alizitaja
baadhi ya adhabu zitazowakabili wagombea au chama ambacho kitavunja maadili ya
uchaguzi kuwa ni kuomba radhi wananchi hadharani, kutotumia vyombo vya habari
kwa muda fulani wakati wa kampeni, onyo la maandishi, kusimamishwa kufanya
kampeni, mgombea kutangaza mbele ya vyombo vya habari kuwa yeye ni bingwa wa kukikuka
maadili ya uchaguzi au kutozwa faini Sh 100,000,
“Ni
hatari kwa chama cha siasa kukiuka maadili, hivyo navisihi vyama vya siasa
kuheshimu na kuzingatia maadili hayo,” alisema Kailima. “Pia niwaombe vyama vya siasa vizingatie
maadili kwenye mikutano yao, viende kuwaambia wananchi watawafanyia nini katika
kata zao na sio vinginevyo,”alisema Kailima.
Kailima
pia alisema chama cha siasa ambacho kinataka kufanya mabadiliko ya ratiba ya
mikutano ya kampeni, lazima kimfahamishe msimamizi wa uchaguzi wa kata na ombi
hilo lazima lijadiliwe na vyama vyote vinavyoshiriki kwenye uchaguzi.
Kuhusu
vitambulisho mbadala vitakavyotumika wakati kupigia kura kwa wale ambao
wamepoteza kadi ya mpiga kura ambavyo ni vitambulisho vya taifa, leseni ya
udereva na hati ya kusafirisha; Kailima amesema vitambulisho hivyo vitatumika
tu kwa watu ambao wameandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika
kituo husika mwaka 2015, lakini pia bado
wana sifa za kupiga kura.
“Masharti
ya kutumia vitambulisho hivyo mbadala ni ya kisheria chini ya Sheria ya
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kifungu 62 (a). Masharti yake ni lazima mtu awe
bado na sifa ya kuwa mpiga kura, mfano mtu akishahukumiwa na kufungwa kwa kosa
la kukwepa kodi, au amechukua uraia wa nchi nyingine au amewekwa kizuizini kwa
mujibu wa sheria na katiba, mtu wa namna hiyo haruhusiwi kupiga kura hata kama ana
kadi ya mpiga kura au vitambulisho hivyo vingine vitatu,”amefafanua Kailima.
Akizungumza
Mikutano ya Kampeni Kailima alitoa wito kwa vyama vya siasa kutambua kwamba
Tume ya Taifa ya uchaguzi imeruhusu mikutano ya kampeni na sio mikutano ya
vyama vya siasa. Amesema mtu anayeruhusiwa kwenye mikutano ya kampeni ni
mgombea mwenyewe, chama chake au mtu yeyote ambaye anaona anaweza kumfanyia
kampeni ndani ya katiba iliyopitishwa.
COMMENTS