N a Mwandishi Wetu Mkuu wa Mkoa (RC) wa Dodoma, Jordan Rugimbana amezikumbusha taasisi za elimu ya juu nchini kuhakikisha zinaongeza ...
Na Mwandishi Wetu
Mkuu wa Mkoa (RC) wa Dodoma, Jordan
Rugimbana amezikumbusha taasisi za elimu ya juu nchini kuhakikisha zinaongeza
uwezo wa madawati ya mikopo yaliyopo katika taasisi zao ili yaweze kutoa
ushirikiano unaotakiwa katika kutatua changamoto za utoaji wa mikopo kwa
wanafunzi wa elimu ya juu.
Mkuu wa Mkoa huyo ametoa agizo
hilo leo (Alhamisi, Machi 17, 2017) wakati akifungua mkutano wa kazi wa siku
mbili kati ya watendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB)
na maafisa mikopo zaidi ya 100 kutoka taasisi za elimu ya juu nchini
wanaokutana katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
“Majukumu ya Bodi ni mazito na
hivyo Bodi inahitaji ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wadau mbalimbali mkiwemo
nyie maafisa mikopo mliopo vyuoni na mnaokutana na wanafunzi kila siku,”
amesema Rugimbana katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu Tawala
Msaidizi (Elimu) wa Mkoa wa Dodoma, Bw. Gosbert Damazo.
Akizungumza katika mkutano huo
kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq
Badru amesema Bodi yake inatambua mchango mkubwa unaotolewa na maafisa mikopo
hao katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wanufaika wa mikopo ya
elimu ya juu waliopo katika taasisi mbalimbali.
“Maafisa hawa ndio
wanaotuunganisha na wanafunzi katika utendaji kazi wetu wa kila siku, hivyo ni
watu muhimu sana kwetu na tunathamini sana mchango wao na wa taasisi zao kwa
ujumla,” amesema Bw. Badru.
Kwa mujibu wa Bw. Badru, Bodi
yake itatumia mkutano huo wa siku mbili kuwakumbusha maafisa hao wajibu wao
katika kutunza kumbukumbu muhimu za wanufaika wa mikopo na majukumu yao muhimu
ili kuongeza ufanisi na hivyo kupunguza malalamiko ya wadau wakiwemo wanafunzi
wanaoufaika wa mikopo ya elimu ya juu.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji huyo
alikumbusha kuwa mwaka 2011, Serikali ilivielekeza vyuo vyote vya elimu ya juu
nchini kuanzisha madawati ya mikopo ya elimu ya juu ili kuongeza ufanisi katika
usimamizi wa mikopo ya elimu ya juu inayotolewa na Serikali.
“Tangu wakati huo (2011),
kumekuwa na mafanikio makubwa katika utendaji wetu kutokana na kuongezeka kwa
ufanisi. Hivi sasa, malalamiko kutoka kwa wanafunzi yamepungua sana kwa kuwa
wana sehemu ya kuwasilisha hoja zao palepale chuoni …wito wangu kwao ni kuwa
wayatumie madawati haya vizuri,” amesema Bw. Badru.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu
cha Dodoma (Taaluma) Prof. Lawrence Msoffe, ambaye alihudhuria hafla ya
ufunguzi, amesema mkutano huo ni muhimu kwa kuwa utaisaidia Bodi kupata mrejesho
kutoka kwa maafisa hao ambao ndio wanaosimamia masuala ya utoaji mikopo katika
vyuo kila siku.
HESLB ilianzishwa kwa mujibu wa
sheria mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi mwezi Julai 2005 ili, pamoja na mambo
mengine, kutoa mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi watanzania wasio na uwezo
na pia kukusanya mikopo iliyoiva iliyotolewa na Serikali tangu mwaka 1994/1995.
COMMENTS