Na Greyson Mwase, Arusha Imeelezwa kuwa vyanzo vya nishati jadidifu kama vile upepo, jua, jotoardhi vitachangia upatikanaji wa...
Na Greyson Mwase, Arusha
Imeelezwa
kuwa vyanzo vya nishati jadidifu kama vile upepo, jua, jotoardhi
vitachangia upatikanaji wa nishati ya uhakika ya umeme kwa kila kijiji
ifikapo mwaka 2030 kama mpango wa nishati kwa wote unavyofafanua.
Hayo
yameelezwa na Kamishna Msaidizi- Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya
Nishati na Madini, Mhandisi Styden Rwebangila katika mafunzo kwa wadau
wa nishati jadidifu kuhusu matumizi ya mfumo mpya wa uhifadhi data na
utoaji taarifa kwa ajili ya nishati jadidifu ujulikanao kama Tanzania
Renewable Energy Management Information System (TREMIS) yaliyofanyika
jijini Arusha leo.
Mhandisi
Rwebangila alisema kuwa ili nchi ya Tanzania kuingia kwenye orodha ya
nchi za kipato cha kati ifikapo mwaka 2025, nishati ya uhakika ya umeme
inahitajika hususan katika kuchochea uwekezaji katika viwanda na kukuza
uchumi wa nchi.
Alisema
mbali na gesi iliyogunduliwa katika mkoa wa Mtwara na maeneo mengine,
nishati ya umeme kutokana na vyanzo vingine kama vile upepo, jua, joto
ardhi vinahitajika ili kuongeza kiwango cha umeme katika Gridi ya Taifa.
“
Kuna maeneo ambayo hayajafikiwa na miradi mikubwa ya Wakala wa Nishati
Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kama visiwani,
ambapo Wizara ya Nishati na Madini imeweka utaratibu wa kutumia vyanzo
vya nishati mbadala kama jua, upepo na jotoardhi kulingana na maeneo
husika ili kila mwananchi afikiwe na huduma ya umme,” alifafanua
Mhandisi Rwebangila.
Aliendelea
kusema kuwa ili kuvutia fursa za uwekezaji, Wizara imeanzisha mfumo
mpya wa uhifadhi data na utoaji taarifa kwa ajili ya nishati jadidifu
ujulikanao kama Tanzania Renewable Energy Management Information
System (TREMIS) utakaowezesha wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi
kupata taarifa kuhusu fursa za uwekezaji katika nishati jadidifu, sera
na taratibu.
Alisema
kuwa taarifa za kampuni zote zinazojihusisha na nishati jadidifu, fursa
za uwekezaji, sera, sheria na taratibu zitawekwa katika mfumo huo
utakaounganishwa na tovuti ya Wizara ili wadau kupata uelewa kabla ya
kuwekeza.
Aliendelea
kusema kuwa hatua iliyofikiwa kwa sasa katika maandalizi ya mfumo huo,
ni utoaji wa mafunzo na ukusanyaji wa maoni kutoka kwa wadau mbalimbali
wa nishati mbadala nchini ambapo mpaka sasa wamekwishafanya zoezi hilo
katika Kanda ya Ziwa.
Kamishna
Msaidizi- Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi,
Styden Rwebangila (kulia) akibadilishana mawazo na Mtaalam kutoka
Kitengo cha Teknolojia ya Habari
na Mawasiliano (TEHAMA)- Wizara ya Nishati na Madini, Danford Phiri
(kushoto) katika mafunzo yaliyokutanisha wadau wa nishati jadidifu
jijini Arusha Februari 16, 2017.
Wadau wa nishati jadidifu wakiendelea na majadiliano katika mafunzo hayo
COMMENTS