Hussein Makame, NEC 2/11/2016. Dar es Salaam. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kuwa itazialika Asasi za Kiraia zina...
Hussein
Makame, NEC
2/11/2016. Dar
es Salaam.
Tume ya Taifa
ya Uchaguzi (NEC) imesema kuwa itazialika Asasi za Kiraia zinazotaka kutoa
Elimu ya Mpiga Kura kutuma maombi ya kupata kibali cha kutoa Elimu hiyo ili
kuhakikisha kila Mtanzania anapata Elimu ya Mpiga Kura.
Hayo yamesemwa
na Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Emmanuel
Kawishe wakati akitoa Elimu ya Mpiga Kura kwenye kipindi cha Kumekucha cha
Televisheni ya ITV jijini Dar es Salaam leo.
Alisema kwa
kuanzia asasi hizo zitapewa muda wa miezi sita kupima mafanikio ya kutoa Elimu
hiyo na kwamba NEC itatoa kibali kwa asasi ambayo imetimiza vigezo vya kutoa
Elimu ya Mpiga Kura nchini.
Bw. Kawishe
alitaja vigezo hivyo kuwa ni asasi iwe imesajiliwa Tanzania, imefanya kazi ya
kutoa Elimu si chini ya miezi sita, iwasilishe majina ya viongozi wake, iwe
inaweza kujigharamia na iwasilishe anuani yake.
Aliongeza
vigezo vingine kuwa ni kama ni asasi ya nje inayofanya kazi pamoja na Tanzania,
kati ya viongozi wake wakuu watatu wawili wawe ni Watanzania na isiwe na historia
ya kuchochea machafuko ama ndani ya Tanzania au nje ya Tanzania.
“Katika kupata
uhakika wa taarifa hizi, sisi Tume ya Taifa ya Uchaguzi hatuna taarifa za
kutosha kuhusiana na hizo asasi, kwa hiyo tunashirikiana na Jeshi la Polisi na
Msajili wa Asasi tutawaomba taarifa za asasi hizo ili kujiridhisha” alisema Bw.
Kawishe.
Alifafanua
kuwa NEC inahitaji kuzifahamu asasi zinazotoa Elimu ya Mpiga Kura ili kujihakikishia
zinatekeleze lengo ambalo tume hiyo inataka litekelezwe ambalo ni kutoa Elimu ya
Mpiga Kura kwa wananchi katika maeneo
wanayotaka kuitoa.
“Kwa hiyo hizi
asasi tutazialika, tutatoa tangazo kuanza na kumalizika kwa kipindi na kuna
watendaji ambao wameandaliwa rasmi kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi watakaokuwa
wanaratibu asasi hizo, watakapoleta maombi yao watayapitia na kuona je
yanakidhi vigezo” alifafanua Bw. Kawishe.
Alisema katika
maombi yao asasi za kiraia zitaombwa kuainisha maeneo ambayo wanataka kwenda
kutoa Elimu hiyo lakini NEC itazisii kwenda kutoa Elimu hiyo maeneo ya
pembezoni ili kuifikisha Elimu ya Mpiga Kura katika maeneo hayo.
Bw. Kawishe
alisema NEC imeamua kutoa Elimu hiyo endelevu kwa kuwa tathmini imeonesha kuwa
Elimu hiyo haitolewi kama inavyotakiwa kiasi cha kuwafanya wananchi wengi kutofahamu
majukumu ya Tume na kutumia kadi ya kupigia kura kama utambulisho kwenye
taasisi za mikopo badala ya kupigia kura.
Mkurugenzi
huyo wa Huduma za Sheria wa NEC aliwataka Watanzania kuifuatilia Tume kwenye
mikutano ambayo itashiriki kutoa Elimu hiyo, kupitia kwenye vyombo vya Habari
au kuingia kwenye Tovuti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ili kupata Elimu ya Mpiga
Kura.
COMMENTS