Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua mitambo ya maji ya DUWASA inayotoa maji yanayosambazwa katika Manispaa ya Dodo...
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua mitambo ya maji ya DUWASA
inayotoa maji yanayosambazwa katika Manispaa ya Dodoma wakati
alipotembelea chanzo cha maji cha Mzakwe Dodoma Oktoba 2, 2016.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua mitambo ya maji ya DUWASA inayotoa maji
yanayosambazwa katika Manispaa ya Dodoma wakati alipotembelea chanzo cha
maji cha Mzakwe Dodoma Oktoba 2, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
*Ni wa taasisi za umma,
wanadaiwa sh. bilioni 1.4
WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa ameagiza apatiwe orodha ya wadaiwa sugu wa taasisi zote za Serikali
mkoani Dodoma ambao wamelimbikiza deni la sh. bilioni 1.4 zikiwa ni bili zao za
maji.
Waziri Mkuu ametoa
agizo hilo leo (Jumapili, Oktoba 2, 2016) wakati akizungumza na watumishi na
viongozi wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dodoma (DUWASA) mara baada ya
kukagua utendaji kazi wa chanzo cha maji cha Mzakwe nje kidogo ya mji wa
Dodoma.
“Niletee haraka orodha
ya wadaiwa wote wa Ofisi za Serikali na taasisi za umma ambao hawajalipa bili
zao. Madeni yote ni lazima yalipwe,” amesema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu ambaye yuko
katika ziara ya siku mbili ya kukagua maandalizi ya Serikali kuhamia Dodoma,
anatembelea sehemu mbalimbali za kutolea huduma za jamii pamoja na kukagua
miundombinu ya mkoa huo.
Aliutaka uongozi wa DUWASA
na watumishi wote wahakakishe wanaboresha huduma za upatikanaji wa maji hasa
kwenye maeneo yanayopimwa viwanja ili wananchi au wawekezaji wanaponunua
viwanja wakute huduma hiyo ipo na waanze ujenzi mara moja.
“Tumealika wawekezaji, nataka
wajenge viwanda na mahoteli hapa Dodoma, sasa wakikuta maji na umeme kwenye
maeneo yao, itakuwa ni kichocheo cha kuharakisha kazi za ujenzi,” amesema.
Pia amemwagiza Mkuu wa
Wilaya ya Dodoma, Bi. Christina Mndeme ahakikishe eneo lililo jirani na chanzo
hicho cha maji halikaliwi na mtu yeyote na linalindwa dhidi ya uchomaji mioto.
“Uchomaji moto uoto wa
asili umeharibu vyanzo vingi vya maji. Ni tatizo kubwa hapa nchini na halina
budi kusimamiwa hadi liishe,” amesisistiza.
Amefikia uamuzi huo baada
ya kupokea taarifa kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi David
Pallangyo kwamba kuna wananchi wameanza kujenga na kufanya shughuli za kijamii jirani
na chanzo hicho licha ya kuwa walikwishaondolewa zamani.
Kuhusu wadaiwa sugu,
Mhandisi Pallangyo alisema mashirika ya umma na taasisi za Serikali ndiyo
wanaongoza kwa kulimbikiza madeni. “Wananchi wa kawaida wapo wanaodaiwa lakini
deni lao siyo kubwa na hao tunawamudu,” alisema wakati akizungumza na mwandishi
wa habari hizi.
Alisema changamoto nyingine
inayowakabili ni uchomaji moto ambapo hivi karibuni uliwashwa moto na kuunguza
baadhi ya nguzo za umeme ambazo zinapeleka umeme kwenye chanzo hicho.
Alisema askari wa JKT
Makutupora walisaidia kuzima moto huo ili usifike kwenye mitambo mingine ya
chanzo hicho cha maji.
Waziri Mkuu pia
alikagua maabara ya upimaji maji kwenye chanzo hicho kabla hayajasambazwa kwa
wateja na mara yanapokuwa yamefika kwa wateja na kuelezwa kuwa maji hayo
yanakidhi viwango vya kitaifa na vya kimataifa vilivyowekwa na Shirika la Afya
Duniani (WHO).
Waziri Mkuu anaendelea
na ziara yake kwa kutembelea kiwanda cha magodoro Dodoma na kituo cha kuzalisha
umeme cha Zuzu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMAPILI, OKTOBA 2, 2016
COMMENTS