Marehemu Jaji Mstaafu Ernest Mwipopo Rais Kikwete aomboleza kifo cha Jaji Mstaafu Ernest Mwipopo Rais wa Jamhuri ya Muunga...
![]() |
Marehemu Jaji Mstaafu Ernest Mwipopo |
Rais Kikwete
aomboleza kifo cha Jaji Mstaafu Ernest Mwipopo
Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amempelekea salamu za
rambirambi Jaji Mkuu wa Tanzania, Mheshimiwa Mohamed Chande Othman kuomboleza
kifo cha Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mjumbe wa Kamisheni ya
Mabadiliko ya Sheria nchini (Tanzania Law Reform Commission), Jaji Ernest
Mwipopo ambaye amefariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea Mkoani Morogoro
leo, Jumatano, Aprili 3, 2013.
“Nimepokea kwa
mshtuko mkubwa na huzuni nyingi taarifa za kifo cha ghafla cha Jaji Mstaafu
Ernest Mwipopo ambaye nimejulishwa kuwa amepoteza maisha yake katika ajali ya
gari Mkoani Morogoro akiwa njiani kutoka Iringa kwenda Dar es Salaam,” Rais
Kikwete amemwambia Jaji Mkuu Othman.
“Nakutumia wewe
Jaji Mkuu wa Tanzania salamu zangu za rambirambi kuomboleza msiba huu mkubwa,
na kupitia kwako nawatumia Majaji wote wa Tanzania wastaafu na walioko bado
kazini rambirambi zangu kwa kuondokewa na Jaji mwenzao na Jumuia nzima ya
wanasheria nchini kwa kuondokewa na mwanasheria mwenzao,” amesema Rais Kikwete
na kuongeza:
“Jaji Ernest
Mwipopo alikuwa mtumishi mwaminifu na mwadilifu wa umma. Tutamkumbuka pia kama
mtumishi ambaye alitumia vipaji vyake vyote alivyojaliwa na Mwenyezi Mungu
kuitumikia nchi yetu kwa moyo wake wote. Alionyesha utumishi uliotukuka tokea
enzi zake kama Mwanasheria wa Serikali, Msaidizi wa Waziri wa Sheria,
Mkurugenzi wa Mashitaka nchini, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Jaji wa
Mahakama ya Kazi hadi katika nafasi aliyokuwa nayo wakati wa kifo chake ya
Kamishna wa Kudumu wa Kamisheni ya Mabadiliko ya Sheria nchini.”
Aidha, Rais
Kikwete amemwomba Jaji Mkuu Mohamed Othman Chande kumfikishia salamu za pole za
chati ya moyo wake kwa familia ya Marehemu Jaji Mstaafu Ernest Mwipopo.
“Wajulishe
wanafamilia na wanandugu kuwa niko nao katika msiba huu mkubwa na natambua
machungu yao katika kipindi hiki kigumu. Naungana nao katika kuomboleza kifo
cha mpendwa wao na katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke
pema peponi roho ya Marehemu Jaji Mstaafu Ernest Mwipopo. Amina.”
COMMENTS