PM MAJALIWA AZINDUA KITABU KATIKA KILELE CHA MAADHIMISHO YA MIAKA 55 YA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM KUJITATHMINI KIMKAKATI

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizindua Kitabu Kiitwacho 'From Lumumba Street to the Hill and Bey...




















Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizindua Kitabu Kiitwacho 'From Lumumba Street to the Hill and Beyond' katika kilele cha Maadhimisho ya Miaka 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam baada ya kuhutubia kwenye ukumbi wa Nkurumah jijini Dar es salaam  Oktoba 25, 2016. Katikati ni Makamu Mkuu wa Cuuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Tekinolojia na Mafunzo ya Ufundi, Dkt Leonard Akwilapo. (PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU)
 


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akiwa na makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Profesa Rwekaza Mukandala baada ya kwasili kwenye ukumbi wa Nkurumah chuoni hapo kuhutubia kwenye kilelele cha Maadhimisho ya Miaka 55 ya Chuo hicho Oktoba 25, 2016
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dae es salaam wa zamani  Profesa Matthew Luhanga  baada ya kuhutubia  kwenye kilele cha Maadhimisho ya Miaka 55 ya Chuo hicho kwenye ukumbi wa Nkurumah jijini Dar es salaam Oktoba 25, 2016
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam wa zamani, Balozi  Nicholas Kuhanga baada ya kuhutubia  kwenye Maadhimisho ya Miaka 55 ya Chuo hicho kwenye ukumbi wa Nkurumah jijini Dar es salaam Oktoba 25, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na Rais wa Jumuiya wa Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Jaji Joseph Warioba baada ya kuhutubia kwenye kilele cha Maadhimisho ya Miaka 55 ya chuo hicho kwenye ukumbi wa Nkurumah jijini Dar es salaam Oktoba 25, 2016


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongozana na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Profesa  Rwekaza Mukandala  (kulia  kwake) kuelekea kwenye ukumbi wa Nkurumah baada ya kuwasili kwenye Chuo Kikuu cha Dar es salaam kuhutubia kwenye kilele cha Maadhimisho ya Miaka 55 ya Chuo hicho Oktoba 25, 2016. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ally Happy, kushoto ni Rais wa  Jumuiya ya Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Jaji Joseph Warioba na wapili kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Tekinoloji, Dkt. Leonard Akwilapo
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia kwenye kilele cha Maadhiisho ya miaka 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam  kwenye ukumbi wa Nkurumah jijini Dar es salaam Oktoba 25, 2016


Baadhi ya waliohudhuria kwenye kilele cha Maadhimisho ya miaka 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam  wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipowahutubia kwenye ukmbi wa Nkuruma jijini Dar es Salaam Oktoba 25, 2016. 

HOTUBA YA WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHESHIMIWA KASSIM MAJALIWA (MB) ILIYOTOLEWA KATIKA SHEREHE ZA KILELE CHA MAADHIMISHO YA MIAKA 55 TANGU KUANZISHWA KWA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM ILIZOFANYIKA KATIKA UKUMBI WA NKRUMAH TAREHE 25 OKTOBA, 2016


Mheshimiwa Prof. Joyce Ndalichako (MB), Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia;
Mheshimiwa Peter Ngumbullu, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam;
Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba, Rais wa Jumuiya ya Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Makamu wa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo;
 Prof. Rwekaza Mukandala, Makamu Mkuu wa Chuo;
 Wajumbe wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam;
 Manaibu wa Makamu Mkuu wa Chuo: Prof. Florens Luoga, Prof. David Mfinanga na Prof. Kimambo;
 Viongozi Waandamizi wa Serikali waliopo;
 Waheshimiwa Wabunge waliopo hapa;
 Waheshimiwa Mabalozi wa Nchi za Kigeni;
 Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa;

Wanataaluma na Wafanyakazi wengine wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam;
 Wanafunzi na Wanajumuiya wote wa Chuo Kikuu cha       Dar es Salaam;
 Wageni Waalikwa;
 Mabibi na Mabwana.

SHUKURANI
  • Napenda kutumia fursa hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kuwa hapa siku ya leo kusherekea maadhimisho haya ya Miaka 55 ya kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
  • Pili, ninawashukuru waandaji wa tukio hili kwa heshima kubwa mliyonipa kuwa mgeni rasmi katika tukio hili muhimu na la kihistoria. Kwangu mimi ni jambo la fahari, furaha na heshima kubwa kupata fursa ya kushiriki pamoja nanyi katika shughuli hii adhimu.
  • Kuna sababu nyingi zinazonifanya kufurahia fursa hii ya kushiriki katika maadhimisho haya. Kwanza kabisa, kama mnavyofahamu, mimi ni mdau wa elimu. Mimi ni mwalimu ambaye ninayeitumikia sekta hii kwa muda wa kutosha. Pili, kama Kiongozi Mwandamizi wa Serikali iliyopo madarakani hivi sasa, nina dhamana ya kushirikiana na wananchi wenzangu katika kuendeleza na kuboresha utoaji elimu kwa jamii yetu, jukumu ambalo pia ni kiini cha wajibu na utendaji wa Chuo hiki.  Tatu, mimi ni mhitimu wa Chuo hiki. Chuo hiki kimenilea na kunipatia ujasiri na maarifa; ambayo yamekuwa nyenzo muhimu katika utendaji wangu wa kazi kwa miaka mingi.

  • Hivyo, ninatoa shukrani zangu za dhati kwa kupata fursa hii. Ninaushukuru uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kubuni na kuandaa maadhimisho haya ya kihistoria. Niseme tu kwa uwazi kwamba, kushiriki kwangu katika sherehe hii kunanipa fursa adimu ya kurudi kwa mama ili kuungana na wahitimu wenzangu, wa miaka ya nyuma na wa hivi karibuni, pamoja na wadau wote wa Chuo chetu hiki, katika kutambua upya jukumu kubwa lililotekelezwa na chuo hiki katika maendeleo ya nchi yetu.

HISTORIA YA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM
Kuanzishwa Kwa Chuo
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Ni vyema tukajikumbusha kwamba Chuo hiki kilianza kikiwa kidogo sana, na kwamba kuanzishwa kwake kulihitaji ushupavu na moyo wa kizalendo. Ni muhimu kuyakumbuka na kuyaelezea mambo haya kwa ufasaha, kwani si wengi wanaofahamu nafasi ya Chuo hiki katika historia ya nchi yetu. Kwa bahati nzuri, baadhi ya mambo haya yamehifadhiwa katika kumbukumbu za kihistoria. Wakati wa sherehe za uzinduzi wa Chuo hiki hapo mwaka 1961, aliyekuwa wakati ule Waziri Mkuu wa Tanganyika, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alisema, na hapa namnukuu:
“Chuo hiki kimeanzishwa kwa dharura. Mapendekezo yote ya kuanzisha Chuo Kikuu Kishirika nchini Tanganyika yalitaja tarehe ya baadaye sana ya kuanzishwa huko. Lakini Serikali yangu iliona kwamba suala hili lina umuhimu wa juu kabisa kielimu. Baadhi ya watu wamesema kuwa ule ilikuwa uamuzi wa kisiasa. Kweli, ulikuwa ni uamuzi wa kisiasa”.   Mwisho wa kunukuu.

Ni dhahiri kwamba kuanzishwa kwa Chuo hiki kulitokana na ndoto sahihi ya viongozi waasisi wa nchi yetu, ndoto ambayo ilikataa dhana ya kuwa na nchi huru isiyokuwa na mpango thabiti wa kuwapa wananchi wake elimu ya juu. Badala yake, waasisi wa taifa hili walichukua hatua sahihi ya kuanzisha taasisi ya elimu ya juu itakayokuwa chemchemi ya maarifa na mahali pa kuwatayarishia wataalamu wa ngazi za juu watakaochochea maendeleo. Kwa kupigania na kufanikiwa kuanzisha Chuo hiki, waasisi wa Taifa letu walidhihirisha uwezo wao wa kuona mbali na uzalendo wa hali ya juu. Viongozi hao walikuwa werevu, na walielewa vizuri kwamba msingi wa maisha na maendeleo ya jamii yoyote iwayo ile ni elimu, na kwamba uwekezaji katika elimu ni jambo lisilokwepeka kwa Serikali inayotaka kuwakwamua watu wake kutoka katika adha ya umaskini, ujinga na maradhi. 
Waasisi wa Chuo
Ndugu Wanajumuiya ya Chuo na Wageni Waalikwa,
Ni vyema basi, tunaposherehekea miaka 55 ya Chuo hiki, tufanye huku tukiwakumbuka na kuwashukuru viongozi waasisi wa nchi yetu na wote walioshiriki katika kukianzisha na kukiendeleza Chuo hiki hadi hapa kilipofikia. Kwa mantiki hiyo, sherehe hizi, ambazo zilianza rasmi jana, vilevile ni sherehe za kuwapongeza na kuwatambua watu wote waliofanya uamuzi makini wa kuanzisha Chuo Kikuu hata kabla nchi yetu haijapata uhuru kamili. Tunawapongeza na kuwashukuru wote walioshiriki katika kutekeleza jukumu lile hasa kwa sababu hawakutishika na changamoto za kuanzisha taasisi kama hii katika nchi ambayo ilikuwa ikikabiliwa na changamoto za umaskini, maradhi na ujinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti,
Siyo rahisi kuwakumbuka wote waliohusika katika kutekeleza jukumu lile la kihistoria, lakini hatuwezi kusahau mchango wa Waziri Mkuu wa siku zile, Mwalimu Nyerere, pamoja na Baraza lake la Mawaziri. Vile vile, si rahisi kusahau michango maalum iliyotolewa na Profesa Cranford Pratt, aliyekuwa Rasi (Principal) wa kwanza wa Chuo, na pia Profesa Arthur Brian Weston, ambaye alikuwa Mkuu wa kwanza wa Kitivo cha Kwanza kuanzishwa Chuoni, yaani Kitivo cha Sheria, pamoja na wanafunzi wake 12 waanzilishi, ambao baadhi yao naambiwa waliweza kuhudhuria sherehe za miaka 50 ya Chuo zilizofanyika mwaka 2011 katika ukumbi huu. Tuwakumbuke pia wanataaluma wote waanzilishi pamoja na viongozi waendeshaji wa Chuo ambao walifanya kazi kubwa ya kuweka msingi imara kwa ajili ya maendeleo ya taasisi hii.
 Chuo Kikuu Cha Umma
Ndugu Wanajumuiya na Wageni Waalikwa,
Kwa kuwa Chuo hiki kilianzishwa katika miaka ya awali ya uhuru wa nchi yetu, hakijawahi kuendekeza sana kasumba za kikoloni kama ilivyokuwa katika baadhi ya vyuo vikuu vya Kiafrika vilivyoanzishwa katika miaka ya 1950 na 1960. Tangu awali Chuo hiki kimechukua taswira ya kuwa Chuo cha Umma, kwa Kiingereza People’s University. Inatia moyo kufahamu kwamba dhana hiyo ya People’s University imeendelea kutekelezwa hadi hivi sasa. Nimefarijika kufahamu kwamba uongozi wa Chuo umekuwa ukifanya jitihada za makusudi kuhakisha kuwa taaluma zinazotolewa hapa zinaendelea kuwa chimbuko la maarifa yanayohitajika katika kuboresha maisha ya wananchi na kuleta maendeleo ya nchi kwa ujumla. Matumaini yangu ni kwamba jitihada hizi zitaendelea na Chuo kitaendelea kudhihirisha kwa vitendo kuwa kiko karibu na wananchi wa kawaida.
UMUHIMU WA MAADHIMISHO YA MIAKA 55 YA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM
Mabibi na Mabwana,
Leo ni siku ambayo tunahitimisha Maadhimisho ya Miaka 55 tangu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Sherehe kama hizi hutoa fursa kwa wahusika kutathmini mafanikio waliyopata na changamoto walizopambana nazo katika kipindi kilichopita. Ni fursa pia ya kufikiria maendeleo ya taasisi husika kwa siku zijazo. Ukweli huo huonekana katika kila aina ya jubilei, lakini pale tunaposherehekea miaka 55 ya taasisi kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam umuhimu wa kufanya mambo haya unakuwa mkubwa zaidi. Kwa hiyo, sote tutambue kwamba ni wajibu wa kila mmoja wetu kuchangia kikamilifu zoezi la kutathmini mafanikio ya Chuo hiki kikongwe, changamoto ambazo Chuo kimekumbana nazo na kusaidia kuchangia jitihada za kukiendeleza zaidi Chuo hadi kufikia mafanikio makubwa.

CHANGAMOTO NA MIKAKATI
Mabibi na Mabwana,
Maslahi ya watumishi, wanataaluma na waendeshaji:
Ninafahamu kuwa yapo madai mbalimbali ikiwemo malimbikizo ya mishaara kwa watumishi hususan baada ya kuanza kwa muundo wa pamoja wa wanataaluma wa vyuo vikuu vya umma. Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuhakikisha inaondoa malimbikizo ya madai kwa watumishi wote wa umma. Mojawapo ya mikakati ya kukamilisha azma hii ni pamoja na; kufanya uhakiki wa taarifa za kiutumishi kwa watumishi wa umma ili kubaini watumishi hewa; zoezi ambalo limesaidia kuwabaini watumishi wa umma hewa wapatao 16,500 kufikia tarehe 20/10/2016.  Baada ya zoezi hilo tutarudia uhakiki wa madeni yote yaliyowasilishwa Serikalini na kasha tutalipa madeni ya watumishi wote.  Natumaini kuwa wote mnakumbuka, Mheshimiwa Rais alitoa tamko la kupunguza kodi kwenye mshahara kuanzia Julai 2016.  Aidha, Serikali inaendelea na maboresho na kuimarisha maslahi kwa watumishi wote wa umma kupitia bodi ya mishahara na motisha mara tutakapokamilisha tutapanga upya mishahara na motisha kwa watumishi.
Wahadhiri Waandamizi na Maprofesa katika Vyuo vya Umma
Mabibi na Mabwana,
Ninatambua kuwa katika vyuo vya umma kuna upungufu mkubwa wa wahadhiri waandamizi na maprofesa na hivyo kuathiri hali ya utoaji wa taaluma kwa fani za “Post –Graduates”. Ninajua kuwa pamoja na sababu nyingine, hali hii inachangiwa pia na masharti ya ajira za mikataba kwa wahadhiri waandamizi kuwa miaka 65 na maprofesa kuwa miaka 70. Serikali itaendelea kuweka kipaumbele cha upatikanaji wa fedha za kutosha kwa ajili ya mafunzo. Wakati huohuo vyuo vya elimu viweke taratibu na mipango endelevu ya kurithishana (kuachiana nafasi) “Succession Plan”. Jambo hii ni muhimu sana kwani bila hivyo, wakati wote kutakuwa na “Gap” kubwa katika utoaji wa taaluma. Aidha, Serikali itatoa ushirikiano wa kutosha katika utekelezaji wa mipango hii ya kuwa na watalaamu wa kutosha katika vyuo. Kwa upande mwingine Serikali itaendelea kutekeleza majukumu ya kuwaajiri wanataaluma na wafanyakazi wapya pale wanapohitajika.
Hali ya upatikanaji wa fedha za uendeshaji
Mabibi na Mabwana,
Kwa wakati tofauti nimekuwa napata malalamiko juu ya vyuo kutopata fedha za kutosha za uendeshaji (OC) na hivyo kuathiri utoaji wa taaluma. Serikali hii imeamua kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ili iweza kumudu mjukumu ya uendeshaji wa Serikali bila ya kutegemea kwa kiwango kikubwa wafadhili wa nje. Matarajio yetu ni kuwa kutokana na kuongezeka kwa makusanyo na kukua kwa uchumi, Serikali itaimarisha hali ya upatikanaji wa fedha za uendeshaji na maendeleo katika taasisi zote za umma. Aidha, vyuo viimarishe ubunifu, umakini na uhalisia ili kukuza makusanyo ya ndani na kuhakikisha matumizi yanafanyika kwa kuzingatia tija (value for money).
Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
Mabibi na Mabwana,
Serikali kupitia Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa ufafanuzi wa namna ya ya kutekeleza utoaji mikopo na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inaendelea kufanya uhakiki wa taarifa za waombaji wa mikopo. Ninapenda kutoa wito kwa wanufaika na waombaji wote wa mikopo wahakikishe kuwa wanatoa taarifa zilizo sahihi na za uhakika.  Hata hivyo, Serikali ilishaongeza bajeti ya mikopo ya Elimu ya Juu kutoka Shilingi Bilioni 340 mwaka 2015/2016 hadi Bilioni 483 kwa mwaka 2016/2017.   
Matokeo ya Kukua kwa Sekta ya Elimu
Mabibi na Mabwana,
Kutokana na kukua kwa sekta ya elimu hususan ushiriki wa sekta binafsi katika sekta ya elimu kumekuwepo na changamoto kubwa ya vyuo kadhaa nchini kuanzisha programu za masomo ambazo haziendani na mahitaji halisi ya taifa letu pamoja na soko la ajira. Ninaamini kuwa jumuiya ya wanataaluma na viongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mnaelewa wajibu na majukumu yenu katika kutekeleza azma ya kukipeleka Chuo mbele kutoka hapa kilipo. Nimeelezwa mambo mengi yanayofanyika ili kuboresha mfumo wa Chuo na kuongeza ufanisi katika utoaji maarifa, ikiwa ni pamoja na kuanzisha programu mpya za masomo kulingana na mahitaji ya taifa letu kwa hivi sasa. Napenda kusisitiza Tume ya Vyuo Vikuu Nchini kuhakikisha kuwa program za masomo zinazoanzishwa na vyuo vikuu zinazingatia mahitaji ya Taifa na soko la ajira.
Mabibi na Mabwana,
Serikali kwa upande wake itaendelea kutekeleza majukumu yake ya kawaida, ambayo ni pamoja na kuendelea kuwaajiri wanataaluma na wafanyakazi wapya pale wanapohitajika; kuwapa stahili zao wale wanaostaafu; kutoa mikopo kwa wanafunzi kulingana na sera iliyokubalika; na kulipa gharama za uendeshaji wa Chuo kadiri ya taratibu za kibajeti. Licha ya hayo, Serikali pia itachukua hatua madhubuti kushughulikia changamoto zinazokwamisha utendaji na ustawi wa Chuo.
Hali ya Miundombinu ya Chuo
Mabibi na Mabwana,
Natambua kutokana na ukubwa na umri wa Chuo ziko changamoto kadhaa zinazohusu mazingira ya kujifunzia na kufundishia hususan utoshelevu wa miundombinu kama vyumba vya mihadhara, maabara, mabweni, ofisi na vifaa mbalimbali. Napenda kuwahakikishia wanajumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuwa Serikali itaendelea kulifanyia kazi tatizo la uhaba wa mabweni ya wanafunzi, na itachukua hatua kushughulikia pia tatizo la upungufu wa maabara, vifaa vya kufundishia na ofisi za wafanyakazi. Tutayatekeleza haya kwa kuzingatia umuhimu wa miradi husika katika uendeshaji na maendeleo ya Chuo pamoja na uwezo wa Serikali kifedha. Mheshimiwa Rais amekwishaonesha mfano wa hatua ambazo Serikali ya Awamu ya Tano itakuwa inachukua katika kushughulikia kero sugu zinazokabili Chuo hiki. Sote tumefurahishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi unaoendelea hapa chuoni wa ujenzi wa mabweni ya wanafunzi, ambao utawapa wanafunzi takribani 3,840 nafasi za malazi chuoni badala ya kupanga mitaani. Aidha, Serikali imeshaanza kutenga fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya taasisi za elimu ya juu na nyinginezo. Tumefanya hivyo katika bajeti ya mwaka huu wa fedha, na tutaendelea kufanya hivyo katika bajeti zijazo. Lengo ni kuziwezesha taasisi hizo, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kikiwepo, kufanyia ukarabati unaostahiki miundombinu yao iliyochakaa. Kwa kutumia fedha hizo, taasisi za umma zitaweza pia, kutekeleza miradi midogo midogo ya maendeleo.
HITIMISHO
Mabibi na Mabwana,
Matumaini yangu ni kwamba Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kitaendelea kutumia changamoto zinazojitokeza mara kwa mara kama chemchemi ya ubunifu wa mambo mapya na mikakati yenye tija. Vilevile ninatumaini kuwa Chuo kitaendelea kuboresha uwezo wake wa ndani wa kupata rasilimali muhimu na kuboresha utendaji wake na kuongeza uwezo wa kujiletea maendeleo. Aidha, Serikali inategemea kuwa Chuo hiki kitaendeleza sifa yake ya kuwa kinara katika utoaji wa taaluma kwa viwango vya kimataifa na hivyo kuwa mfano wa ubora katika sekta ya elimu ya juu hapa nchini na katika ukanda huu wa Afrika. Sina shaka kuwa haya yote yanawezekana kwa kuwa yako katika uwezo wenu wa kitaasisi. Ninawahakikishia kuwa Serikali itakuwa nanyi daima katika jitihada za kufikia ndoto yenu kuelekea mwaka 2061.
 Mabibi na Mabwana,
Ningependa kumalizia hotuba yangu kwa kuwashukuru tena wote waliohusika katika kuandaa maadhimisho haya na kutekeleza majukumu mbalimbali. Nawashukuru pia nyote mliohudhuria hafla hii ambayo ndiyo kilele cha maadhimisho ya miaka 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Na sasa, kwa mamlaka mliyonipa kama Mgeni Rasmi katika hafla hii, ninayo furaha, kutamka kuwa Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es Slaam zimefungwa rasmi.
Nawatakia heri na fanaka katika shughuli zenu zitakazoendelea baada ya maadhimisho haya.
ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA
https://ssl.gstatic.com/ui/v1/icons/mail/images/cleardot.gif
 

COMMENTS

Name

analogia,2,Biashara,618,dijital,235,Jamii,3473,Magazeti,385,Michezo,334,Mikoani,1262,Moto,334,Sanaa,247,Siasa,369,Slide,10,tv,4,Uchumi,276,
ltr
item
Okandablogs: PM MAJALIWA AZINDUA KITABU KATIKA KILELE CHA MAADHIMISHO YA MIAKA 55 YA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM KUJITATHMINI KIMKAKATI
PM MAJALIWA AZINDUA KITABU KATIKA KILELE CHA MAADHIMISHO YA MIAKA 55 YA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM KUJITATHMINI KIMKAKATI
https://i.ytimg.com/vi/weiguwFPtX8/hqdefault.jpg
https://i.ytimg.com/vi/weiguwFPtX8/default.jpg
Okandablogs
http://robertokanda.blogspot.com/2016/10/pm-majaliwa-azindua-kitabu-katika.html
http://robertokanda.blogspot.com/
http://robertokanda.blogspot.com/
http://robertokanda.blogspot.com/2016/10/pm-majaliwa-azindua-kitabu-katika.html
true
7708052459372695991
UTF-8
Loaded All Posts Not found any posts VIEW ALL Readmore Reply Cancel reply Delete By Home PAGES POSTS View All RECOMMENDED FOR YOU LABEL ARCHIVE SEARCH ALL POSTS Not found any post match with your request Back Home Sunday Monday Tuesday Wednesday Thursday Friday Saturday Sun Mon Tue Wed Thu Fri Sat January February March April May June July August September October November December Jan Feb Mar Apr May Jun Jul Aug Sep Oct Nov Dec just now 1 minute ago $$1$$ minutes ago 1 hour ago $$1$$ hours ago Yesterday $$1$$ days ago $$1$$ weeks ago more than 5 weeks ago Followers Follow THIS CONTENT IS PREMIUM Please share to unlock Copy All Code Select All Code All codes were copied to your clipboard Can not copy the codes / texts, please press [CTRL]+[C] (or CMD+C with Mac) to copy