Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki akizungumza na watendaji, waganga wakuu wa wilaya na mkoa wa mkoa wa Dar es...
**************
Na Aron Msigwa – MAELEZO.
20/4/2015.Dar es Salaam.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki amezindua Mpango Kazi wa kuharakisha kupunguza
vifo vya akina mama na watoto walio chini ya miaka 5 kwa mkoa wa Dar es salaam
na kukemea tabia ya baadhi ya watumishi wasio waadilifu wanaotumia lugha za
kuudhi, kejeli na vitendo vya unyanyasaji kwa akina mama wajawazito wanaofika kupata huduma
za uzazi katika hospitali, vituo vya afya na Zahanati.
Akizungumza
katika kikao kilichowahusisha watendaji wa mkoa, waganga wakuu wa wilaya
na mkoa wa Dar es Salaam leo jijini humo, Mhe. Sadiki amesema watumishi wa afya wa mkoa huo wanao wajibu wa
kutekeleza majukumu yao na kutimiza malengo yaliyowekwa
na Serikali ya kuwapatia huduma bora za afya akina mama wajawazito na watoto walio na umri
chini ya miaka 5 yaliyowekwa na mkoa.
Amesema kuwa katika kutekeleza mpango kazi huo Serikali
haitasita kuwachukulia hatua za kinidhamu na kisheria watumishi wa afya watakaobainika
kushiriki katika vitendo ubadhirifu na wale watakaosababisha kwa namna moja au nyingine vifo vya mama
wajawazito na watoto chini ya miaka 5 watakaofika hospitalini kupata huduma za
afya na kupoteza maisha yao kutokana na uzembe wa watumishi katika vituo
husika.
Amebainisha kuwa mkoa
Dar es Salaam pamoja na mambo mengine umeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha
kuwa inawafikia akina mama na watoto na kuwapatia huduma bora akina mama
wajawazito wanaofika katika vituo vya afya vya Serikali kupata huduma za uzazi ili
kukabiliana na vifo vya akina mama na watoto vinavyotokea.
Ameeleza kuwa Tanzania
imekuwa ikitekeleza malengo ya millennia (MDG) ambayo yalipangwa kukamilika
ifikapo Disemba 2015 na kuongeza kuwa katika utekelezaji wa malengo hayo bado
inakabiliwa na changamoto za kupunguza vifo vya wajawazito ambavyo amesema kwa
takwimu za mwaka 2013 zinaonyesha vifo 410 kwa kila vizazi hai 100,000.
“ Tanzania katika jambo
hili tumepiga hatua japo bado tunakabiliwa na changamoto ya kuendelea kupunguza
vifo hivyo kufikia 133 kwa kila vizazi hai 100 if ikapo mwezi Disemba 2015”
Amesema akiwa kiongozi
wa mkoa huo atahakikisha lengo hilo linatimiza kabla ya muda uliopangwa na
kuwataka watendaji wa afya kwa ngazi zote kutimiza wajibu wao ipasavyo na
kuzitumia rasilimali zilizopangwa kutekeleza malengo yaliyopangwa ili
kuhakikisha kuwa vifo vinavyotokana na uzazi na vile vya watoto wachanga
vinapungua .
“Nachoweza kusema,
uwezo wa kukabiliana na changamoto hii tunao tukiunganisha nguvu zetu kwa
mazingira tuliyonayo ya taasisi za
Serikali na Binafsi bado tunayo nafasi nzuri ya kutimiza malengo yaliyowekwa, kwa
sasa tunaendelea na mkakati wetu wa kuongeza wodi za kujifungulia akina mama
wajazito wilaya ya Temeke, Ilala na
Kinondoni ili kuongeza wigo wa huduma za afya” Amesema.
Ametoa wito kwa
wataalamu wa afya kuendelea kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa akina mama
wajawazito ili waweze kuelewa umuhimu wa kuhudhuria Kliniki kabla na baada ya
kujifungua za afya kupitia mpango wa TIKA utakaoanzishwa katika jiji la Dar es Salaam utakaowawezesha kupata huduma za afya kwa mwaka mzima kwa gharama nafuu.
Katika hatua nyingine
Mhe. Sadiki amewataka wakurugenzi wa manispaa za Mkoa huo, kuendelea
kutenga fedha kwa ajili ya motisha kwa watumishi wa afya wanaotumia muda mwingi
kazini wakiwahudumia wagonjwa hususani akina mama wachanga na watoto chini ya
miaka 5 wa mkoa huo.
Kwa upande wake Mganga
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Grace Maghembe awali akiwasilisha Mpango Kaziwa
Kuharakisha kupunguza vifo vya akina mama, Watoto wachanga na watoto walio
chini ya umri wa miaka 5 kwa mkoa wa Dar es Salaam amesema kuwa licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali
toka kuzinduliwa kwake miaka 2 iliyopita na Rais Jakaya Kikwete umepata mafanikio.
Amesema kuwa pamoja na
kuongezeka wa idadi ya wazazi wanaojifungua kutoka 97,807 hadi 134,838 mwaka
2012 hadi 2014 vifo vya uzazi vimepungua kutoka 123 hadi 99 katika vizazi hai
100,000.
Amesema mafanikio zaidi
ya huduma ya afya ya mama na mtoto katika mkoa wa Dar es Salaam bado yanakabiliwa
na changamoto mbalimbali zikiwemo kiwango kidogo cha matumizi ya huduma ya uzazi
wa mpango wa asilimia 47, kiwango kidogo cha asilimia 51 ya wajawazito
wanaohudhuria Kliniki angalau mara 4 chini ya lengo kitaifa ambalo ni asilimia
90.
Aidha ameeleza kuwa
mkoa unaendelea kuchukua hatu mbalimbali za kuhakikisha kuwa huduma ya afya ya
mama na mtoto inaimarika katika jiji la Dar es Salaam kwa kuiweka huduma hii
kuwa kipaumbele cha mkoa na kuongeza usimamizi shirikishi wa huduma za afya,
mafunzo kazini kwa watumishi, kuongeza vitendea kazi, dawa na vifaa tiba pamoja
na kuhamasisha ushiriki wa wadau na wafadhili mbalimbali.
COMMENTS