Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Ramadhani Kailima akitoa Ufafanuzi kuhusu malalamiko ya ukiukwaji wa maa...
Mkurugenzi
wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Ramadhani Kailima akitoa
Ufafanuzi kuhusu malalamiko ya ukiukwaji wa maadili ya Uchaguzi
yaliyotolewa na Chama cha ACT WAZALENDO.
Na. Aron Msigwa –NEC.
Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekishauri Chama cha ACT – Wazalendo na
Vyama vingine vyenye wagombea wa Ubunge katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo
la Dimani na Udiwani katika Kata Ishirini (20) za Tanzania Bara
,kuwasilisha malalamiko ya ukiukwaji wa Maadili ya Uchaguzi kwenye
Kamati za Maadili zilizo katika maeneo yao.
Akizungumza
na vyombo vya habari leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Uchaguzi
wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Bw. Kailima Ramadhan amesema NEC
imepata taarifa kupitia Vyombo mbalimbali juu ya malalamiko ya Chama Cha
ACT-Wazalendo kuvilalamikia Vyombo vya Dola pamoja na Watendaji wa Umma
kufanya vitendo vyenye muelekeo wa kukipendelea Chama Cha Mapinduzi
(CCM).
Bw.
Kailima amesema taarifa ya Chama hicho iliyotolewa kwenye Vyombo vya
Habari Januari, 12 2017, imeeleza kuwa Watendaji wa Halmashauri ya Geita
waliwakusanya Wazee katika Kata ya Nkoma waje na Vitambulisho vyao vya
kupigia Kura kwa lengo la kuwapatia huduma ya afya bure jambo
linalolalamikiwa na ACT- Wazalendo kwa madai kwamba Watendaji hao wana
lengo la kuwahadaa Wazee hao ili wakipigie Kura Chama Cha Mapinduzi
(CCM).
Aidha,
amesema katika malalamiko yake Chama cha ACT Wazalendo kimeibua tuhuma
za wananchi kupokwa kadi za kupigia Kura ili wasiweze kushiriki katika
uchaguzi mdogo utakaofanyika Januari 22, 2017.
Mkurugenzi
Kailima amesisitiza kuwa ni kosa chini ya kifungu cha 88 cha Sheria ya
Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na kifungu cha 100 cha Sheria ya Uchaguzi
ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292 mtu kumiliki kadi ya kupigia kura
isiyokuwa yake.
“Natoa
wito kwa wananchi wote kwamba, ni kosa chini ya kifungu cha 88 cha
Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na kifungu cha 100 cha Sheria
ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292 mtu yeyote kumiliki kadi
ya kupigia kura isiyokuwa yake” Amesema.
Amefafanua
kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuzingatia sehemu ya 5.4 ya Maadili
ya Uchaguzi inavikumbusha Vyama vya Siasa kuwa iwapo vitakuwa na
malalamiko ya ukiukwaji wa Maadili ya Uchaguzi katika Uchaguzi Mdogo wa
Udiwani viwasilishe malalamiko hayo kwenye Kamati ya Maadili ngazi ya
Kata ndani ya saa 72 tangu kutokea kwa tukio linalolalamikiwa.
“
Sehemu ya 5.4 ya Maadili ya Uchaguzi yayosainiwa na Tume ya Taifa ya
Uchaguzi, Serikali na Vyama Vya Siasa inaeleza wazi muda wa kuwasilisha
malalamiko kwa kuvitaka vyama au wahusika wenye malalamiko yoyote
kuyawasilisha kwa maandishi kwenye Kamati ya Maadili ya Uchaguzi ya
ngazi husika ndani ya saa 72 tangu kutokea kwa tukio” Amesisitiza
Kailima.
Amesisitiza
kuwa iwapo Chama cha Siasa au Mgombea hataridhika na maamuzi ya Kamati
ya Maadili ngazi ya Kata, kwa kuzingatia sehemu ya 5.7 (a) ya Maadili ya
Uchaguzi anatakiwa awasilishe rufaa yake kwa Msimamzi wa Uchaguzi ngazi
ya Jimbo ndani ya saa 24 tangu maamuzi ya Kamati ya Maadili ngazi ya
kata kutolewa.
Aidha,
Bw. Kailima amebainisha kuwa kama Chama cha Siasa hakikuridhika na
maamuzi ya Kamati ya Maadili ngazi ya Jimbo, bado kwa kuzingatia sehemu
ya 5.7 (b) na (c) kinayo fursa ya kuwasilisha Rufaa yake katika Kamati
ya Maadili ngazi ya Taifa au ngazi ya Rufaa ambayo ni Tume ya Taifa ya
Uchaguzi.
“
Tunavishauri Vyama vya Siasa na Wagombea kuzingatia matakwa ya Maadili
ya Uchaguzi katika kuwasilisha malalamiko yao ya ukiukwaji wa maadili ya
Uchaguzi, kwa mujibu wa sehemu ya 5.7(e) ya Maadili ya Uchaguzi, pale
ambapo Chama cha Siasa au Mgombea hakuridhika na maamuzi ya Kamati ya
Rufaa atakuwa na fursa ya kuwasilisha malamiko yake Mahakamani baada ya
Uchaguzi kwa mujibu wa Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na
Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292”.
Amesisitiza
kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea kuwasihi viongozi wa Vyama
vya Siasa na Wadau wengine wa Uchaguzi kuendelea na Kampeni za
kistaarabu na kuzingatia Sheria, Kanuni na Maadili ya Uchaguzi na kwamba
inaendelea kufuatilia kwa karibu kila hatua ya Uchaguzi na hasa Kampeni
huku akisisitiza kuwa haitasita kuchukua hatua kwa mtu yeyote
atakayekiuka Sheria za Uchaguzi.
COMMENTS