F SERIKALI YADHAMIRIA KUMALIZA MGOGORO WA NYAMONGO-MAJALIWA | RobertOkanda

Friday, January 19, 2018

SERIKALI YADHAMIRIA KUMALIZA MGOGORO WA NYAMONGO-MAJALIWAWAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kumaliza mgogoro ulipo kati ya wananchi wa Kata ya Nyamongo na muwekezaji wa mgodi wa North Mara.


Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi pamoja na mwekezaji wa mgodi huo wanaishi na kuendesha shughuli zao za kimaendeleo kwa kufuata sheria za nchi.Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Januari 18, 2018) wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kata ya Nyamongo, wilayani Tarime.


Waziri Mkuu amesema Serikali haiwezi kuvumilia kuona wananchi na wawekezaji wakigombana, inataka kumaliza mgogoro huo ili pande zote zifanye kazi zake kwa amani.Katika kuhakikisha mgogoro huo unakuwa historia Waziri Mkuu ameitisha kikao kitakachowakutanisha wawakilishi wa wananchi , viongozi wa mgodi na mbunge wa jimbo la Tarime Bw. John Heche.


Amesema katika hicho kitakachofanyika Januari 28, 2018 Ofisini kwa Waziri Mkuu mjini Dodoma, ambapo aliwakikishia wananchi hao kwamba Serikali italinda maslahi yao.Awali, Waziri Mkuu alitembelea kata ya Nyamwaga na kukagua kituo cha afya cha Nyamwaga, ambapo amesema kinatosha kupandishwa hadhi na kuwa hospitali ya wilaya.


Hivyo amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dkt. Francis Mwanisi aanze mchakato wa kupeleka vifaa katika kituo hicho ili wananchi wa Halmashauri ya Tarime waanze kutibiwa.


Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. John Magufuli ameongeza bajeti ya ununuzi wa dawa na kufikia sh. bilioni 269 ili kuhakikisha hakuna mgonjwa anayekwenda hospitali na kukosa dawa.


Amesema mbali na kuongeza bajeti katika ununuzi wa dawa, pia ameziagiza halmashauri zote kuhakikisha suala la utoaji wa vitambulisho kwa wazee ili watibiwe bure linatekelezwa

0 comments:

Post a Comment