Meneja wa Shughuli za Kitakwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Wilfred Mwingira akizungumza na wadadisi wakati wa mafunzo y...
Meneja wa Shughuli za Kitakwimu
kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Wilfred Mwingira akizungumza na wadadisi
wakati wa mafunzo ya Utafiti wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Tanzania
yanayoendelea kufanyika katika ukumbi wa Chuo cha Mipango mkoani Dodoma.
Wadadisi wakijifunza kwa vitengo
namna ya kutumia vifaa vya kielektroniki - tablets vitakavyotumika wakati wa
Utafiti wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Tanzania unaotarajia kufanyika mwezi
Agosti mwaka huu. Mafunzo ya Wadadisi wa utafiti huo yanaendelea kufanyika
katika ukumbi wa Chuo cha Mipango mkoani Dodoma.
NA: VERONICA KAZIMOTO, DODOMA
UTAFITI wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini
Tanzania wa awamu ya pili unatarajia kufanyika mwezi Agosti mwaka huu.
Akizungumza wakati wa mafunzo ya wadadisi
yanayoendelea kufanyika mkoani Dodoma Meneja wa Shughuli za
Kitakwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Wilfred Mwingira
amesema lengo kuu la utafiti huo ni kufuatilia viashiria
vilivyowekwa kwenye utafiti wa awamu ya kwanza ili kutathmini na kujua kama kuna
athari yoyote iliyotokea.
"Utafiti huu ni wa kitaifa na utafanyika
Tanzania Bara na Zanzibar kwa lengo la kutathmini na kujua kama kuna athari
yoyote iliyojitokeza kwenye viashiria vilivyowekwa kwenye utafiti wa awamu ya
kwanza", amesema Mwingira.
Nae Mratibu wa utafiti huo Rainer Kiama
amesema kuwa utafiti huu unafanyika ili kutathmini kama mpango unaleta manufaa
yaliyokusudiwa katika ngazi ya kaya kwa kutumia viashiria kama vile elimu,
afya, kazi na matumizi ya muda, shughuli za kaya zisizo za kilimo, mapato,
mikopo, akiba na uhamishaji fedha.
Viashiria vingine ni shughuli za
kilimo, makazi ya kaya na upatikanaji wa maji, matumizi na usalama
wa chakula katika kaya, maamuzi katika kaya, ukatili kwa wanawake na
matarajio ya vijana, mahusiano ya kaya na jamii pamoja na mtazamo wa kaya
kuhusu Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.
Utafiti wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini
Tanzania wa awamu ya pili utahusisha kaya takribani elfu saba
(7,000) ambazo zilihojiwa katika utafiti wa awamu wa kwanza uliofanyika
mwezi Juni, 2015.
COMMENTS