SOKO LA FERI LATAKIWA KUTAFUTA GESI YA BEI NAFUU WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Bodi ya soko la Kimataifa la Samaki la Fer...
SOKO LA
FERI LATAKIWA KUTAFUTA GESI YA BEI NAFUU
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Bodi ya soko la Kimataifa la Samaki la Feri, kukutana
na makampuni mbalimbali yanayouza gesi ili kupata kampuni inayouza kwa bei
nafuu zaidi lengo likiwa ni kuwapunguzia gharama wakaangaji wa samaki sokoni hapo.
Pia
Waziri Mkuu Majaliwa alimtaka Meneja wa soko hilo, Bw. Solomon Mushi kuhakikisha
wanakuwa na kifaa maalumu cha kupimia ujazo wa mitungi ya gesi sokoni hapo ili
kubaini kama ni sahihi.
Ametoa
agizo hilo leo mchana (Jumanne, Machi 22, 2016) wakati alipofanya ziara ya
ghafla katika Soko la Kimataifa la Samaki la Feri iliyokuwa na lengo la
kuangalia mfumo wa majiko ya gesi sokoni hapo ambapo aliridhishwa na
unavyofanya kazi.
Waziri
Mkuu ambaye ametumia dakika 44 kulitembea soko hilo, alitoa maagizo hayo baada
ya kupokea malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara ambao wamesema wamekuwa
wakiuziwa gesi kwa bei kubwa ambayo imekuwa ikiongezeka mara kwa mara.
Akizungumza
kwa niaba ya wafanyabiashara hao, Bw. Ally Iddi amesema awali walikuwa
wanauziwa mtungi wa gesi wenye ujazo wa kilo 32 kwa sh. 70,000 na sasa
umeongezeka hadi sh. 98,000 kiasi ambacho ni kikubwa ukilinganisha na
uzalishaji wao. “Nimeulizia kwenye baadhi ya maduka na kukuta mtungi wenye
ujazo kama huo unauzwa sh. 75,000,” alisema.
Kijana
mwingine ambaye ni mkaangaji wa samaki, Bw. Mwanya Selemeni alisema hivi sasa
hali ya soko la feri ni nzuri tofauti na walivyokuwa wakitumia kuni kwa sababu
hakuna moshi. Alimuomba Waziri Mkuu ahakikishe wanafikishiwa gesi ya kutoka
Mtwara ili gharama ziweze kupungua.
Mfanyabiashara
mwingine wa soko hilo, Bi. Mariam Samweli ambaye alikuwa akiuza kuni na sasa
yeye na wenzake wanataka kufanya biashara nyingine lakini banda walilokuwa
wakilitumia halina umeme licha ya kuwa wameomba mara nyingi. “Tunaomba kupatiwa
umeme ili tuweke vipepeo tuweze kufanya biashara nyingine,” alisema.
Waziri
Mkuu pia alitembelea eneo la mnada wa kuuza samaki sokoni hapo ambako alielezwa
matatizo ya umeme na uzibaji wa mitaro ya maji machafu hali ambayo inatishia
usalama wa afya zao.
“Kuna
jipu la umeme hapa, tunachangishwa hela na kumpa mtu ambaye hatumjui lakini
hatujawahi kuona risiti, wao wanaweka umeme juu kwa juu na umeme wenyewe wala
haukai. Mita tunayo hapa lakini hata namba hatujapewa,” alisema Bw. Omari
Masoud kwa niaba ya wenzake.
Kuhusu
tatizo la uzibaji mitaro na kutiririsha majitaka, kiongozi wa mama lishe sokoni
hapo, Bi. Fatma Ally aliomba watatuliwe tatizo hilo ambalo limedumu kwa zaidi
miezi miwili.
Akijibu
kero zao, Waziri Mkuu alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Bw. Raymond Mushi
asimamie suala la kuweka umeme kwenye hilo banda pamoja ahakikishe mama lishe
wa soko hilo upande wa mnadani waanze kutumia majiko ya gesi badala ya mkaa.
Kuhusu
mitaro, alimwagiza meneja wa soko hilo, Bw. Solomon Mushi aimarishe uzibuaji wa
mitaro katika soko hilo. “ Mwambie mkandarasi azibue mitaro kila siku jioni na
watumiaji wa soko waache kutumia mifuko ya plastiki kwa sababu inapoingia kule
inaziba na wala haiozi,” alisema.
Aliwataka
wafanyabiashara waimarishe usafi kwa sababu ni sehemu ya chakula. “Lengo letu
ni kufanya soko hili liwe kwenye viwango vya kimataiafa ili mteja anapokuja
kununua samaki wabichi ama wa kukaanga awe na chaguo,” alisema.
Kwa
upande wake, Meneja wa soko hilo, Bw. Mushi alisema bodi ya soko hilo ambayo
imeundwa hivi karibuni itakutana kesho kwa mara ya kwanza na miongoni mwa mambo
yatakayojadiliwa ni maelekezo yaliyotolewa na Waziri Mkuu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
JUMANNE, MACHI 22, 2016.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua eneo la kukaangia samaki kwenye soko la
samaki Feri la jijini Dar es salaam Machi 22, 2016, Kushoto kwake ni Mkuu wa
Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi. Waziri
Mkuu alipata fursa ya kuzungumza na wakaanga samaki, wapaa samaki, mama ntilie
na wadau wengine wa soko hilo la kimataifa hapa nchini. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mama Lishe wakati
alipotembelea soko la samaki la Feri jijini Dar es salaam Machi 22, 2016
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mama Lishe wakati
alipotembelea soko la samaki la Feri jijini Dar es salaam Machi 22, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
COMMENTS