Na Jovina Bujulu-MAELEZO, Dar es Salaam WANATASNIA ya habari nchini wametakiwa kuukubali muswada wa sheria wa huduma...
Na Jovina Bujulu-MAELEZO, Dar es Salaam
WANATASNIA
ya habari nchini wametakiwa kuukubali muswada wa sheria wa huduma ya
habari unaotarajia kuwasilishwa hivi karibuni Bungeni kwa kuwa
umekusudia kuifanya taaluma hiyo kuaminika kwa jamii.
Hayo
yamasemwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Hassan Abbas Jijini Dar es
salaam wakati wa ziara yake ya kutembelea vyombo vya habari vilivyopo
Jijini humo.
Alisema
kwa muda mrefu wadau wa Habari na wanatasnia wenyewe wamekuwa na kiu ya
kupata sheria mpya baada ya ile ya mwaka 1976, ambayo imepitwa na
wakati.
“Kutokana
na teknolojia kubadilika, ni wakati mwafaka wa kuanzishwa kwa taasisi
inayosimamia maadili ya wanahabari, hivyo vyombo vya Habari waliona ni
muhimu kuwa na sheria mpya itakayokidhi mabadiliko hayo” alisema Abbas.
Aidha,
alisema kuwa sheria hiyo itahusu vyombo vya habari vya mfumo wa
machapisho, ambavyo ni pamoja na magazeti na majarida na si mitandao ya
kijamii kama wadau wanatafsiri.
Aliongeza
kuwa miongoni mwa masuala yanayozungumziwa katika muswada huo ni pamoja
na kuundwa kwa bodi ya ithibati kwa wanahabari, Baraza huru la habari,
Ofisi ya mkurugenzi wa habari, na Mfuko wa mafunzo kwa wanahabari.
Abbas
aliongeza Serikali imewashirikisha wadau muhimu wakati wa mchakato wa
kuandaa muswada huo ikiwemo Baraza la Habari Tanzania (MCT), Chama cha
wamiliki wa vyombo vya habari (MOAT), Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF)
na baadhi ya wadau wa haki za binadamu.
Aidha alitoa wito kwa wadau wote kutoa maoni yao kwa lengo la kuboresha muswada huo sheria kupitia barua pepe ya ofisi ya Bunge can.bunge.go.tz ili kuyawasilisha mbele ya kamati ya kudumu ya bunge ya huduma za maendeleo ya jamii.
COMMENTS