Serikali imesema awamu ya pili ya Upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kigoma itaanza rasmi Julai mwaka huu. Waziri wa Ujenzi, Uchuku...
Serikali
imesema awamu ya pili ya Upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kigoma itaanza rasmi
Julai mwaka huu.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema zabuni kwa
ajili ya ujenzi zitatangazwa badae mwaka huu ili kuuwezesha Uwanja huo kuwa na
hadhi ya kimataifa na kuchochea fursa za utalii katika ukanda wa Magharibi na
Mwambao wa Ziwa Tanganyika.
Zaidi ya
Shilingi Bilioni 40 kutoka Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB), zinatarajiwa
kutumika hivyo kuwataka wananchi ambao eneo lao liko katika Uwanja huo kuondoka
mara moja mara baada ya kulipwa fidia.
“Nia ya
Serikali ni kuongeza njia ya kuruka na kutua ndege kutoka urefu wa mita 1800
sasa hadi mita 3100 na hivyo kuruhusu ndege kubwa aina ya Boeing 737 kutua
katika uwanja huo”, amesema Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa
amewataka wananchi wa Kigoma kutoa ushirikiano mkubwa kwa Mamlaka ya Viwanja
vya Ndege na Mamlaka ya Usafiri wa Anga ili zoezi la ujenzi lifanikiwe kwa haraka
na kuepuka vikwazo vinavyoweza kuchelewesha mradi huo.
Naye Mbunge wa
Kigoma Mjini, Mhe. Zitto Kabwe amewataka wananchi wa Kigoma na wawekezaji
kujipanga kutumia fursa ya uwanja huo kuwekeza ili kukuza sekta ya utalii na
usafirishaji katika Mwambao wa Ziwa Tanganyika pindi uwanja huo utakapokamilika.
“Tuna bahati
kupata Serikali inayowekeza katika mkoa wa Kigoma, nawaomba wana Kigoma
wenzangu tuepuke migogoro na kutumia fursa hii kuwekeza kikamilifu ili kukuza
utalii katika ukanda wa Magharibi na kuongeza mapato katika mkoa wa Kigoma”,
amesisitiza Mhe. Zitto.
Amemhakikishia
Profesa Mbarawa kuwa Uwanja wa Ndege wa Kigoma utafungua usafiri wa Anga kwa
ukanda wa magharibi na nchi jirani na hivyo kuongeza idadi ya watalii na
watumiaji wa usafiri wa anga katika mwambao wa Ziwa Tanganyika, hifadhi za Taifa za Gombe na Mahale na mikoa
ya kanda ya magharibi.
Kwa upande wake
Meneja wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Mkoani Kigoma Bw. Godlove Longole ameiomba
Serikali kukamilisha Ujenzi wa uzio,
Jengo la Abiria, Mnara wa kuongozea ndege na huduma za zimamoto katika uwanja
huo ili kuuwezesha kufanya kazi zake kwa viwango vinavyotakiwa.
Meneja wa
Kiwanja cha Ndege cha Kigoma Bw. Mohamedi Issa amemhakikishia Waziri kwamba
atasimamia mchakato mzima wa mradi wa ujenzi kwa uadilifu, uaminifu ili thamani
ya mradi huo iwiane na ubora wa kazi itakayofanywa na hivyo kuuwezesha uwanja
huo kufikia kiwango cha Code 4C kinachowezesha ndege zenye ukubwa wa Boeing 737
kutua katika uwanja huo.
COMMENTS