Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mh. Pandu Ameir Kificho akiambatana na Makatibu na walinzi wa Baraza hilo wakitoa...
Spika
wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mh. Pandu Ameir Kificho akiambatana
na Makatibu na walinzi wa Baraza hilo wakitoa nje mara baada ya
kufungwa kwa Mkutano wa 18 wa Baraza la Wawakilishi Mbweni leo.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifunga Mkutano wa 18
wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar uliokuwa ukiendelea katika ukumbi wa
Majengo ya Baraza hilo uliyopo Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar leo.
Aliyepo meza ya juu ni Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho. Picha na – OMPR – ZNZ.
*************************************************
Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar inakamilisha utafiti wa kuibua vivutio vipya
vya Utalii vilivyopo katika maeneo ya vijiji nchini ambapo matokeo ya
utafiti huo yatasambazwa kwa wanachi ili kuongeza uelewa wa fursa za
sekta ya utalii zilizomo katika maeneo yao.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati
akiufunga Mkutano wa 18 wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar uliokuwa
ukiendelea katika ukumbi wa Majengo ya Baraza hilo yaliyopo Mbweni Nje
kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Balozi
Seif alisema utekelezaji wa mpango huo unatarajiwa kutoa ajira za moja
kwa moja zaidi kwa Wananchi hasa wale wa Vijijini katika kuendeleza ile
azma ya Serikali ya kuimarisha Utalii kwa wote.
Alisema
mwishoni mwa mwaka uliopita Sekta ya Utalii imefanikiwa kutoa fursa za
ajira zisizokuwa za moja kwa moja zipatazo 60,000 na zile za moja kwa
moja 22,884 ambapo takwimu zinaonyesha wazi kwamba mchango wa sekta ya
utalii katika pato la Taifa umefikia asilimia 27%.
Balozi
Seif alieleza kutokana na mchango mkubwa wa sekta ya utalii katika
maendeleo ya Taifa Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya
kitaasisi na kiutendaji ili kukidhi viwango vinavyokubalika kimataifa
katika utoaji wa huduma za kitalii.
Alifahamisha
kwamba Serikali itazidi kuhamasisha wananchi kuzalisha bidhaa bora na
zenye viwango ambazo zitakuwa na uwezo wa kuingia kwenye soko la utalii
na hivyo kuifanya sekta hii kuzidi kuwanufaisha zaidi wananchi ambao
ndio walengwa wakuu.
Alieleza
kuwa hivi sasa wananchi waliowengi hasa wakulima wamepata fursa ya
kuuza bidhaa wanazozalisha mashambani kuuza kwenye hoteli mbali mbali
hali ambayo imeongeza upatikanaji wa soko la uhakika wa bidhaa zao.
Alisema
kuwa ili sekta ya utalii izidi kukuwa na kuleta tija hakuna budi kwa
Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi na wananchi kuimarisha
vivutio pamoja na mindombinu itakayowavutia watalii ikiwemo usafi na
utunzaji wa mazingira, uwekezaji katika ujenzi wa hoteli zenye viwango
bora.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliziagiza Taasisi zinazohusika katika
kusimamia sekta hiyo kuandaa na kutekeleza mipango itakayoamsha ari ya
wananchi kupenda kutembelea maeneo yenye vivutio vya utalii kwa lengo la
kukuza utalii wa ndani.
Hata
hivyo Balozi Seif alitahadharisha wazi kwamba kuimarika kwa utalii
washirika wote wa sekta hiyo hawanabudi kuhakikisha kwamba mapato
yatokanayo na eneo hilo yanakusanywa kikamilifu na kuingia katika mfuko
Mkuu wa Serikali.
Aliendelea
kusisitiza umuhimu wa kuendelea kudumishwa kwa amani iliyopo hapa
nchini ambayo ndiyo kichocheo kikubwa kinachotoa fursa kwa wageni na
watalii kupenda kuvitembelea visiwa vya Zanzibar.
Akizungumzia
sekta ya kilimo ambayo bado ni tegemeo kubwa la wananchi waliowengi
katika kujipatia ajira, kipato,chakula na kuimarisha lishe na afya zao
Balozi Seif alisema Serikali inaendelea kutoa msukumo mkubwa kusaidia
sekta hiyo ili wananchi waweze kuongeza tija na uzalishaji na hivyo
kuimarisha vipato vyao.
Alisema
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Kilimo imejiandaa
kikamilifu kuhakikisha kwamba huduma za kilimo cha matrekta na zana
nyengine za kilimo zinapatikana kwa uhakika na kwa bei nafuu zitakazotoa
nafasi kwa wakulima kuzimudu.
Alisema
mpango huo utakwenda sambamba na ongezeko la kiwango cha upatikanaji wa
mbegu bora ya mpunga, dawa ya kuulia magugu na mbolea kupitia programu
ya ruzuku katika kilimo cha Mpunga.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa wito kwa wakulima wote wa zao la
mpunga nchini kuungana na juhudi zinazochukuliwa na Serikali kwa kutumia
fursa zilizopo kuhakikisha wanalima kwa wakati na kufuata kanuni za
kilimo bora.
Halkadhalika
Balozi Seif akawahimiza wakulima wote wa mazao mengine kuchukuwa juhudi
stahiki kwa kufuata ushauri wa mabwana shamba na Mabibi shamba ili nao
waweze kuongeza uzalishaji wa mazao yao.
Akigusia
suala la udhalilishaji wa kijinsia ambalo linaendelea kuwa changamoto
licha ya juhudi zinazochukuliwa za kudhibiti vitendo viovu lakini Balozi
Seif alisema bado wapo watu miongoni mwa jamii wanaoendeleza vitendo
hivyo.
Alisema
ni wajibu wa kila mwana jamii kuzidisha mapambano dhidi ya waovu
wanaohusika na matendo hayo kwa kuwafichua na kuwapeleka kwenye vyombo
vya sheria bila ya kuwaonea muhali.
Alisema
waovu hao kwa kiasi kikubwa wanavunja utu na heshima za kibinaadamu na
kuwasababishia madhara makubwa ya kimwili na kiakili.
“
Watu wote wenye taarifa za waovu hao ni vyema kutosita kufika
mahakamani kwa kutoa ushahidi pale wanapohitajika na kuacha kabisa
masuala hayo kumalizikia majumbani “. Alisema Balozi Seif.
Kuhusu
utolewaji wa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar aliwakumbusha Wananchi pamoja na Viongozi hasa wale wa
Kisiasa waelewe kwamba huduma hiyo hutolewa kwa mujibu wa sheria nambari
7 ya Mwaka 2005.
Alisema
muhusika lazima atimize matakwa ya sheria hiyo kabla ya kupatiwa
kitambulisho ambayo ni pamoja na Mzanzibari wa kuzaliwa, mwananchi kukaa
katika eneo lake si chini ya miezi 36 sambamba na kutimiza umri wa
miaka 18.
Hata
hivyo Balozi Seif alifafanua kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 13 { 1 } { 2
} cha sheria hiyo imetoa haki kwa mtu kukata rufaa kwa Mkurugenzi wa
Vitambulisho dhidi ya Afisi ya usajili pindipo hakuridhia na mamuzi
yanayotolewa au kwa waziri kama pia hakuridhika na uamuzi wa
Mkurugenzi.
Alisema
suala la utoaji wa vitambulisho vya Mzanzibari limekuwa na mjadala
mkubwa kutokana na baadhi ya wanasiasa na waheshimiwa kulalamikia juu ya
baadhi ya wananchi wao kutopatiwa vitambulisho hivyo kwa sababu mbali
mbali.
Alielezea
imani yake kwamba waheshimiwa wawakilishi, wanasiasa na wananchi hawana
sababu ya kulalamikia suala hilo ambalo lina utaratibu mzuri
uliowekwa kwa mujibu wa sheria.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitanabahisha kwamba suala zima la
upatikanaji wa vitambulisho hivyo lisihusishwe na mambo ya kisiasa kwani
utaratibu wa kisheria upo. Hivyo ni vyema na wajibu wa kila mwananchi
kutumia sheria hiyo katika kutafuta haki yake.
Miswada
Minne ya Sheria iliwasilishwa katika Mkutano huo wa 18 wa Baraza la
Wawakilishi na kujadiliwa na wajumbe wa Baraza hilo ambayo ni Mswada
wa sheria ya kuanzisha sheria ya kupunguza na kukabiliana na maafa
Zanzibar na Mambo mengine yanayohusiana na hayo.
Mwengine
ni Mswada wa sheria ya kuanzisha Taasisi ya ulinzi ya Jeshi la Kujenga
Uchumi Zanzibar, Mswada wa sheria ya kufuta sheria ya usimamizi wa
mazingira kwa ajili ya maendeleo endelevu nambari 2 ya mwaka 1996 na
kuweka badala yake msharti bora ya kuhifadhi, kulinda na kusimamia
mazingira pamoja na mswada wa sheria ya maadili ya Viongozi wa umma na
kuanzisha Tume ya maadili ya Viongozi na mambo mengine yanayohusiana na
hayo.
Baraza la Wawakilishi Zanzibar limeahirishwa hadi Jumatano ya Tarehe 11 Machi mwaka 2015 mnamo saa 3.000 za asubuhi.
COMMENTS