Na Frank Shija, MAELEZO. Serikali ya Awamu ya Tano ndani ya mwaka mmoja imeanza mipango ya kuboresha usafi...
Na
Frank Shija, MAELEZO.
Serikali ya Awamu ya
Tano ndani ya mwaka mmoja imeanza mipango ya kuboresha usafiri wa reli ya Kati
kwa kuijenga kwa kiwango cha kimataifa yaani Standard Gauge. Usafiri huu
utaongeza fursa za kiuchumi kwani mazao ya chakula na biashara toka mikoa ya
Kigoma, Kagera, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Tabora na Singida kuelekea Dar es Salaam
yatasafirishwa kwa haraka.
Reli hii itarahisisha
pia usafiri wa abiria wa mikoa ya Kanda ya Ziwa, Kati na Magharibi. Usafiri wa
treni kwa kiwango kikubwa huwa ni wa uhakika na wa gharama nafuu. Hivyo ujenzi
wa reli kwa Standard Gauge uteleta ukombozi mkubwa wa kiuchumi kwa watu wa
maeneo hayo na Taifa kwa ujumla.
Kwa kipindi kirefu
huduma ya usafiri wa treni kupitia Reli ya Kati (Central Line Railway) imekuwa
msaada mkubwa kwa wananchi wa mkoa wa Kigoma na maeneo ya Kanda ya ziwa na nchi
za jirani zikiwemo Burundi, Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Historia inaonesha
kuwa Reli ya Kati kama inavyojulikana sasa ilijengwa kati ya mwaka 1905 hadi
1914 wakati huo ikiitwa Reli ya Tanganyika kwa kuwa ilikuwa ikielekea Mkoani
Kigoma ambako Ziwa Tanganyika linapatikana.
Kutokana na umuhimu wake
katika kukuza uchumi kupitia usafirishaji bidhaa na huduma mbalimbali ndani na
nje ya Tanzania, Katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali imeamua kuja na
mpango kabambe wa kuifanyia maboresho miundombinu ya reli hiyo ili iweze kwenda na wakati na kasi
ya ukuaji wa uchumi.Mpango huo unahusisha
ujenzi wa mtandao wa Reli mpya ya Kati katika Viwango vya Kimataifa (Standard
Gauge 80’) ili kuendana na kasi ya ongezeko la mizigo.
Msemaji wa Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Bw. William Budoya anaeleza kuwa gharama
iliyokaidiriwa kutumika kukamilisha mradi huo ni Dola za Kimarekani Bilioni 7.6
ambazo ni sawa na shilingi za Kitanzania Trilioni 16.Fedha hizo zitatumika
kugharamia ujenzi wa Kilomita 2,561 za reli kwa kiwango cha Kimataifa . Ili
kufanikisha mradi huo Serikali imepata ufadhili kutoka Benki ya Exim ya China ambayo
imekubali kutoa mkopo wenye masharti nafuu.
Aidha, katika
kuhakikisha kuwa ujenzi huo unafanikiwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. John Pombe Magufuli anakutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Benki ya
Exim ya China Bw. Liu Liang Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo yao
Rais wa benki hiyo anamuhakikishia Rais Dkt. John Magufuli kuwa Benki hiyo iko tayari
kutoa kiasi hicho cha fedha ili kufanikisha ujenzi wa kilometa 2,190 za reli.
Pia anamuhakikishia Rais kuwa Benki hiyo itashirikiana na Tanzania katika
kubadilishana uzoefu na utaalamu katika ujenzi na uendeshaji wa reli hiyo.Akiuzungumzia ujenzi
wa Reli hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli
anabainisha kuwa kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuinua uchumi wa Tanzania
na nchi jirani zisizopakana na bahari zikiwemo Uganda, Rwanda, Burundi, na Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Congo.
Anasema reli hiyo mpya
itakua tofauti na inayotumika sasa kutokana na uwezo wake wa kuhimili usafirishaji wa mizigo mingi
kwa kuwa inajengwa kwa kiwango cha Kimataifa "Standard Gauge railway
" na itaanzia Dar es Salaam Mpaka Kigoma, kupitia Tabora, Mwanza,Isaka
hadi Rusumo; Kaliua -Mpanda -Karema na Uvinza -Musongati nchini Burundi.
Katika ufafanuzi
alioutoa hivi karibuni kuhusu ujenzi wa reli hiyo wakati wa Mkutano Mkuu Maalum
wa Chama cha Mapinduzi mjini Dodoma hivi karibuni, Rais John Pombe Magufuli
alisema tayari mchakato wa ujenzi wa reli hiyo umeanza kwa kutangaza zabuni ili
kumpata mkandarasi atakaye jenga Reli hiyo.
Anasema sambamba na kazi hiyo Serikali itakarabati
matawi ya reli ya kati sehemu ya Kaliua-Mpanda ili kuboresha ufanisi wake, kwa
kutenga Sh. bilioni 5.5 za ajili ya usanifu.Aidha, Mpango wa
Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano uliowasilishwa bungeni Dodoma na Waziri wa
Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango unaeleza kuwa Serikali imejipanga kufanya
usanifu na ujenzi wa madaraja 16 kati ya 28 yaliyochakaa kati ya Dar es Salaam
na Tabora.
Aliyekuwa
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Servaciaus Likwelile akizungumza
mara baada ya utiaji saini wa makubaliano wa ujenzi wa reli hiyo kwa niaba ya
Serikali ya Tanzania na Naibu Meneja Mikopo Nafuu wa Benki ya Exim ya China Bw.
Zhu Ying anasema kuwa Dola za Kimarekani bilioni 7.6 ambazo ni sawa na Shilingi
Trilioni 16 zitatumika kutekeleza mradi huo.
Dkt.
Likwelile anasema hatua hiyo inawezesha kuanza kwa kazi ya upembuzi yakinifu,
usanifu na uundwaji wa timu za pamoja kuanza kuainisha mahitaji halisi ya
ujenzi wa mradi huo.Anasema mradi huu
umekuja wakati muafaka kutokana na kwamba reli iliyopo sasa ambayo ni ya
Kiwango cha "meter gauge” haina uwezo mkubwa katika ubebaji wake wa
mizigo, hata baada ya kufanyiwa ukarabati.Kwa mwaka ni tani
Milioni 5 za mizigo ndizo zinaweza kupitishwa na reli ya sasa, ambazo haziwezi
kukabili mahitaji ya mizigo ya Kanda hii ambayo itafikia tani Milioni 30
ifikapo mwaka 2025.
Kutokana na uhitaji
huo wa kukabiliana na uongezaji wa mizigo kwa kujenga uwezo wa kuihudumia kwa
kuwa na reli ambayo pamoja na kuwa na uwezo wa kubeba mizigo hiyo itakuwa na
uwezo wa kubeba abiria wengi zaidi na kwa starehe lakini pia kwa kasi ya spidi
ya wastani wa kilometa 100 kwa saa hivyo kuwezesha abiria kufika haraka zaidi
sehemu wanazokwenda.
Pia wakati wa ujenzi
wa reli hiyo watanzania takribani 300,000 watapata ajira kutokana na kushiriki
katika ujenzi wa reli hiyo.
COMMENTS