Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
22/3/2014. Dar es salaam.
Wanafunzi wanawake wa Chuo cha
Elimu ya Biashara Dar es salaam (CBE) wamezindua mchakato wa kuanzisha mfuko wa
Jumuiya ya wanafunzi wa kike wenye lengo la kumkomboa na kumwezesha
mwanafunzi wa kike kujitambua, kielimu, kisiasa na kiutamaduni.
Akizungumza na jumuiya ya
wanafunzi wa kike wa chuo hicho wakati wa uzinduzi wa mfuko huo leo
jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi wa Wizara ya Viwanda na
Biashara Dkt. Mary Mwangisa ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo amesema
kuwa kuanzishwa kwa jumuiya hiyo ni ishara ya umoja na mshikamano wa
wanafunzi wa kike chuoni hapo.
Amesema kuanzishwa kwa mfuko huo
kunatokana na kuongezeka kwa changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake
pia kukosekana kwa mifuko ya aina hiyo katika taasisi nyingi za elimu ya
juu hapa nchini.
Ameeleza kuwa malengo ya
mfuko huo ni kumwezesha mwanafunzi wa kike wa CBE kujitambua kielimu, kisiasa
na kiutamaduni na kuongeza kuwa yamekuja wakati muafaka kufuatia
mabadiliko yaliyopo sasa ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni.
Amefafanua kuwa mfuko huo
ulioanzishwa katika chuo hicho ni fursa pekee ya kuwawezesha wanafunzi wa kike
kunufaika kwa kupata elimu bora bila vikwazo.
“Napenda kutumia fursa hii
kuushukuru uongozi wa chuo hiki kwa kuonyesha njia ya kuwajali wanawake na pia
katika kuweka taratibu nzuri za kulinda maadili, katika maisha yangu sijawahi
kusikia chuo kikuu chochote kimezindua jukwaa la wanawake lenye malengo mazuri
kama yenu” Amesema Dkt. Mwangisa.
Ameeleza kuwa kwa muda mrefu
wanawake kote nchini wamekuwa na juhudi mbalimbali za kujikomboa kiuchumi
pamoja na kulitumikia taifa kwa kushika nyadhifa mbalimbali serikalini kwa
ufanisi mkubwa na kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii pindi wanapokabidhiwa
madaraka.
“Ninapowaangalia ninyi nafarijika
maana naona viongozi wakuu wa serikali, naona marais na pia wakurugenzi wa
biashara”
Akizungumza kuhusu kuanzishwa kwa
mfuko huo na mafanikio yake Dkt. Mwangisa amesema kuwa atatoa ushirikiano
kwa wanafunzi hao ili kuhakikisha kuwa mfuko huo unajengewa uwezo wa
kusimama na kuwanufaisha wanawake wanaokumbwa na changamoto zinazokwamisha
maendeleo yao ikiwemo ukosefu wa fedha.
Amesema kuwa kukamilika kwa
taratibu za jumuiya hiyo ikiwemo maandalizi ya katiba ya jukwaa hilo
kutaliwezesha jukwaa hilo kupanga, kuandaa na kutekeleza mikakati mbalimbali ya
kujiendesha ili kuwawezesha wanafunzi hao kutatua changamoto zinazowakabili kwa
kulinda heshima yao katika jamii.
Kwa upande wake mjumbe wa Bodi ya
Taaluma ya Chuo hicho Dkt. Ellen Otaru Okoedion amesema kuwa wanafunzi wa kike
wa chuo hicho wanahitaji msaada kupitia mfuko huo utakaowawezesha kupambana na
wimbi la wanafunzi wa kike kushindwa kumaliza masomo yao kwa kushindwa kumudu
gharama za masomo.
Amewataka wanafunzi wa kike wa
chuo hicho kutumia ipasavyo taaluma wanayoipata kusaidia mfuko huo kupata
fedha ili uwe endelevu kwa maendeleo ya wanawake na chuo hicho.
“Ninyi mnasoma elimu ya biashara
na ndio watalaam wenyewe sitarajii mfuko wenu ukose uwezo, naamini mtatumia
taaluma yenu mnayoipata hapa chuoni kutafuta fedha kwa kuwa mnao uwezo huo”
Amesisitiza Dkt. Ellen.
Naye Waziri wa Wanawake wa Chuo
cha Elimu ya Biashara (CBE) Bi. Mwajuma Sangali ameeleza kuwa wanawake kote
nchini wana jukumu la kuandaa kizazi cha watu wenye upendo, uzalendo, kupenda
kazi na maendeleo.
Amesema kuanzishwa kwa chombo
hicho kunalenga kuboresha maisha ya wanawake hasa katika masuala ya
elimu,jamii,uchumi na siasa
|
COMMENTS