Na Mwandishi Wetu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, amefungua Kikao kinachowakutanisha Wadau wa Masuala ya Wakimbizi k...
Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, amefungua Kikao kinachowakutanisha Wadau wa Masuala ya Wakimbizi kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Watendaji Wakuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) Agosti 9, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa Ufunguzi huo, Mwigulu aliwataka washiriki wa kikao hicho kujadili kwa kina na kufikia makubaliano juu ya suala la uhifadhi wakimbizi na suluhisho la kudumu la wakimbizi huku akiahidi Serikali iko tayari kupokea wakimbizi kama ilivyokuwa desturi huku akisisitiza Serikali haitumvumilia mkimbizi atakaevunja sheria na kuwaasa kufanya utaratibu wa kurudi katika nchi zao wakimbizi ambao nchi zao hali ya usalama imerejea.
“Tukiwa leo tuko katika kikao hiki cha viongozi wa juu wa Serikali na Uongozi wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi, nina imani tutafikia muafaka juu ya suala la uhifadhi wakimbizi na suluhisho la kudumu la wakimbizi, Serikali ya Tanzania imekua na desturi ya muda mrefu ya kupokea wakimbizi na kuwahudumia,ila nawaaasa wadau wote washirikiane kwa pamoja katika kubeba gharama zinazohusu jambo la kuwahifadhi wakimbizi,” alisema Mwigulu
Akizungumza wakati wa Kikao hicho, Makamu Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR), Volker Turk, alisema wamekuja nchini ili kujadili suala nzima la uhifadhi wakimbizi na kupokea maoni kutoka kwa nchi wenyeji huku akisisitiza lengo la kikao hicho ni kuona jinsi gani changamoto mbalimbali zinazoletwa na wakimbizi zinaweza kutatuliwa.
“Napenda kwanza kuishukuru Serikali ya Tanzania na wananchi wanaoishi katika jamii zilipo kambi za wakimbizi kwa ukarimu wao wa muda mrefu wa kuwapokea wakimbizi kutoka nchi mbalimbali wanaokimbia machafuko katika nchi zao,tunafahamu changamoto wanazopata jamii hizo, ndio maana tumeomba kukutana na Serikali kuona suluhisho la kudumu la changamoto hizo.
Kikao hicho kimewashirikisha wadau mbalimbali ikiwemo Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Mambo ya Nje, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Rais,Wakuu wa Mikoa zilipo kambi za wakimbizi na Viongozi wa juu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani kutoka Makao Makuu nchini Geneva.
COMMENTS