F UKOMO WA KUSHUGHULIKIA MAOMBI YA MUDA MREFU YA KUUNGANISHA UMEME NI AGOSTI 30. WAZIRI KALEMANI | Okandablogs

Friday, August 18, 2017

UKOMO WA KUSHUGHULIKIA MAOMBI YA MUDA MREFU YA KUUNGANISHA UMEME NI AGOSTI 30. WAZIRI KALEMANI

Na Teresia Mhagama

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani ameeleza kuwa ukomo wa kuunganishia umeme wateja walioomba kuunganishiwa huduma hiyo kwa muda mrefu ni Agosti 30, 2017 na Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) atakayeshindwa kutimiza agizo hilo atashushwa cheo.

Dkt. Kalemani aliyasema hayo kwa nyakati tofauti akiwa katika ziara ya kuzindua mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini wa Awamu ya Tatu katika mikoa ya Rukwa, Ruvuma na Mtwara.

"Unakuta kuna wateja wameomba kuunganishiwa umeme miezi kadhaa iliyopita lakini mpaka sasa hawajaunganishwa wakati vifaa vipo, kwa hili lazima tuchukue hatua kwa Meneja kama ni wa wilaya, mkoa, Kanda au Mkurugenzi atayechelewa kuunganishia wateja Umeme," alisema Dkt. Kalemani.

Dkt. Kalemani alisema kuwa muda wa kumuunganishia mteja Umeme mara anapolipia huduma hiyo ni Siku Saba na si vinginevyo."Natambua kuna maeneo ambayo TANESCO mnafanya kazi vizuri lakini katika hili tutawajibishana," alisisitiza Dkt. Kalemani.

Wakati huohuo. Dkt. Kalemani aliwaagiza watendaji wa TANESCO kuhakikisha kuwa watu wote wanaofanya kazi ya kutandaza nyaya za umeme ndani ya nyumba wawe wanatambulika na Shirika hilo ili kuondoa tatizo la vishoka kufanya kazi hiyo pasipo ufanisi na baadaye kuleta madhafa kama ya moto.

Vilevile aliwataka watendaji hao kutokukaa maofisini na badala yake wawafuate wananchi sehemu walipo, suala ambalo litafanya Shirika hilo kuongeza idadi ya wateja na kuwaondolea wananchi kero ya kutembea kwa umbali mrefu kufuata huduma TANESCO.

Kuhusu usimamizi wa mradi wa usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu ambao umeshaanza kutekelezwa nchini, Dkt Kalemani aliwataka watendaji wa TANESCO kuhakikisha kuwa wanawasimamia wakandarasi wanaofanya kazi hiyo usiku na mchana ili mradi ukamilike ndani muda uliopangwa.

Aidha Dkt. Kalemani alitoa maagizo mbalimbali ambayo yanapaswa kutekelezwa na wakandarasi wote waliopewa kazi ya kusambaza umeme vijijini katika Mradi wa Awamu ya Tatu.

Naibu Waziri aliwaagiza Wakandarasi hao kutoajiri wakandarasi wasaidizi wanaotoka nje ya eneo lao la kazi ili wananchi wanaotoka katika maeneo hayo wapate ajira na kutoa huduma mbalimbali kwa wakandarasi hao na hivyo kujiongezea kipato.

Pia aliwataka wakandarasi hao kutokuruka kijiji, kitongoji, sehemu zinazotoa huduma muhimu kama mitambo ya maji, Shule, vituo vya afya na sehemu za biashara, na nyumba ambazo tayari zimeshafanyiwa malipo ya kuunganishwa na huduma ya umeme.

" nisingependa kusikia Kituo cha Afya, Shule au Mitambo ya Maji imerukwa na haijawekewa Umeme hivyo nichukue nafasi hii kuwashauri watendaji wa Halmashauri nchini kutenga fedha kwenye Bajeti zao kwa ajili ya kutandaza nyaya za Umeme kwenye sehemu hizo ili wakandarasi waweze kuingiza Umeme," alisema Dkt. Kalemani.

Vilevile, Dkt. Kalemani aliwataka wakandarasi hao kutoa malipo kwa wakandarasi wadogo ndani ya wakati ili kuepusha mradi huo kusuasua na kuwacheleweshea huduma wananchi.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani akizungumza na wananchi (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa mradi wa kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu katika mkoa wa Ruvuma.

0 comments:

Post a Comment