F DKT. SHEIN AANZA ZIARA YAKE VISIWANI ZANZIBAR. | RobertOkanda

Saturday, August 12, 2017

DKT. SHEIN AANZA ZIARA YAKE VISIWANI ZANZIBAR.

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar  Dkt. Ali Mohamed Shein  amewataka viongozi na watendaji wa chama hicho kufanya kazi za kuimarisha taasisi hiyo ya kisiasa ili ishinde na kuongoza dola katika uchaguzi mkuu ujao.

Rai hiyo ameitoa  wakati akizindua Tawi la CCM la Kitope ‘B’  jimbo la Mahonda kwenye ziara yake ya kukagua na kuzindua miradi mbali mbali ya maendeleo aliyoianza leo Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Dkt. Shein alisema viongozi na wanachama wa chama hicho wanatakiwa kutumia vyema ofisi za Tawi hilo ambalo ni la kisasa kwa lengo la kutekeleza kwa ufanisi kazi za kisisaa zitakazozaa matunda ya ushindi katika uchaguzi wa mwaka 2020.

“Kwanza nakupongezeni viongozi na wanachama wote wa jimbo la Mahonda mlioshiriki kujenga tawi hili la kisasa linaloendana na hadhi ya chama chetu kimaendeleo kwani lina ofisi zote ambazo ngazi zote kiutendaji ndani ya tawi mtafanya kazi zenu kwa utulivu.

Pia nasaha zangu kwenu ni kwamba uchaguzi mkuu unakaribia haupo mbali hivyo tumieni ofisi hii vizuri kuchapa kazi kwa bidii sambamba na kuongeza wanachama wapya ambao ndio mtaji wetu mkubwa wa kisiasa ili kuhakikisha 2020 tunashinda.”, alisisitiza Dkt. Shein.

Aidha alisema kuwa lengo la serikali ya mapinduzi ya Zanzibar inayotokana na CCM ni kuimarisha huduma zote za kijamii na kiuchumi ili wananchi wa mijini na vijijini waweze kunufaika na fursa hizo.

Dkt.Shein ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alitembelea ujenzi wa kituo kipya cha mashine za kutibia maji kinachojengwa katika eneo la Donge mbiji ambapo mradi huo uliofadhiliwa na serikali ya China utagharimu zaidi ya Dola za kimarekani milioni 5.5.

Katika ziara hiyo  Dkt. Shein alitembelea  shamba la  karafuu  na  kuzungumza  na mliki wa mradi wa kilimo cha karafuu huko Donge  Pwani, Haroun Abou Mbarouk alieleza kuwa shamba hilo lenye mikarafuu zaidi ya 170 limekuwa likizalisha zao hilo kwa wingi ambapo kwa mavuno ya mwaka wanapata zaidi ya gunia 25.

Sambamba na hayo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alitembelea mradi wa ujenzi wa tangi la Maji huko Donge Kisongo unaojengwa na mafundi  kutoka jamhuri ya watu wa China utakaowanufaisha  wananchi  wa Wilaya ya Kaskazini “B”  na maeneo jirani.

Ziara hiyo itaendelea kesho katika Wilaya ya Kaskazini  ‘’A” Unguja ambapo Dkt.Shein ataweka  mawe ya msingi katika miradi mbali mbali ya kijamii na kuhitimisha kwa hotuba ya majumuisho ndani ya Mkoa huo.


Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein akisalimiana na wananchi pamoja na wanachama wa CCM  Jimbo la Mahonda katika uzinduzi wa Tawi la CCM Kitope ‘’B’’ katika ziara yake Zanzibar iliyoanza leo Mkoa wa Kaskazini Unguja.


Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein akizindua rasmi   Tawi la CCM Kitope ‘’B’’ katika ziara yake Zanzibar iliyoanza leo Mkoa wa Kaskazini Unguja.


Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein akiangalia  ngoma ya kibati  mara baada ya kuwasili katika kiwanda cha Sukari Mahonda kwa ajili ya kukagua maendeleo ya kiwanda hicho.


Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein akiwa na viongozi wengine wa serikali na wawekezaji wa kiwanda  cha sukari mahonda wakikagua maeneo mbali mbali ya kiwanda.


(Juu na chini) Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein akikagua mashine zilizopo katika kituo cha kutibia maji huko Donge Mbiji Wilaya ya Kaskazini “B’’ Unguja.0 comments:

Post a Comment