Na Hamza Temba Wizara ya Maliasili na Utalii Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe kwa kushirikiana na balozi wa Ujer...
Na Hamza Temba Wizara ya Maliasili na Utalii
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe kwa kushirikiana na
balozi wa Ujerumani hapa nchini, Egon Konchanke amezindua Mradi wa
Uhifadhi na Maendeleo ya Ikolojia ya Pori la akiba la Selous SECAD
(Selous Ecosytem Conservation and Development Program) ambao
umefadhiliwa na Serikali ya Ujerumani kwa ushirikiano na Serikali ya
Tanzania, mradi huo utatekelezwa na Wizara ya Maliasili na Utalii
kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA, WWF (World
Wildlife Fund) na FZS (Frankfurt Zoological Society).
Akizungumza
katika hafla iliyofanyika jana, Matembwe Selous, Mkoani Morogoro,
Waziri Maghembe alisema Serikali ya Ujerumani kupitia benki ya ya KFW
imechangia Euro Mil. 18 (sawa na Shilingi Bil. 45.124) katika mradi huo
utakaodumu kwa miaka mitano huku mashirika ya WWF (World Wildlife Fund)
na FZS (Frankfurt Zoological Society) yakichangia Euro laki 4 kila moja
(sawa na Shilingi bil. 1.8). Pamoja na uzinduzi huo alizindua pia Mpango
Kazi wa Dharura wa miaka mitano wa kuendeleza pori hilo.
"Mradi
huu ni muhimu sana kwakua utasaidia kuongeza nguvu kwenye jitihada zetu
za kuendeleza na kuimarisha hifadhi ya pori hili la Selous ikiwemo
upatikanaji wa vitendea kazi pamoja na kutuongezea nguvu kwenye
mapambano dhidi ya ujangili", alisema Prof. Maghembe.
Alisema
jitihada ambazo Serikali imeshazifanya katika pori hilo ni pamoja na
kuimarisha doria za ndege zenye rubani na zisizo na rubani (drones),
kutoa mafunzo ya jeshi usu kwa askari, kuongeza maaskari pamoja na
vitendea kazi ambapo katika mwaka ujao wa fedha Serikali itatoa magari
mengine 15 kusaidia pori hilo.
"Pamoja
na jitihada hizo tuna mpango wa kuwekeza dola za kimarekani Milioni 156
(sawa na Shilingi bilioni 352.560) kwa ajili ya kuboresha pori hili
(Selous), Ruaha, Mikumi, Ruangwa na Kitulo kuhakikisha watalii
wanatembelea maeneo haya na kuondoa kile kikwazo cha wao kutotembelea
hifadhi za kusini, hiyo inaenda sambamba na kuimarishwa kwa shirika la
ndege la Serikali la Air Tanzania kuondoa changamoto iliyokuwepo ya
usafiri wa anga", alisema Prof. Maghembe.
Akizungumzia
changamoto ya ujangili katika pori hilo alisema Serikali imefanikiwa
kwa kiasi kikubwa kupambana na tatizo hilo ambapo majangili wengi
wameshakamatwa katika maeneo ya Tunduru, Namtumbo na maeneo ya katikati
ya Selous. Alisema changamoto hiyo bado ipo katika maeneo ya Mkoa wa
Ruvuma ambapo imeripotiwa na kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa huo
kuwa kuna upatikanaji wa silaha za kivita kutoka nchini Msumbiji ambazo
zinapatikana kwa watu kubadilishana na magunia ya mchele changamoto
ambayo inaendelea kufanyiwa kazi.
Wakati
huo huo, Prof. Maghembe akijibu swali aliloulizwa na wanahabari kuhusu
hatua iliyofikiwa juu ya kauli aliyoitoa bungeni hivi karibuni ya
kuunganisha taasisi zote za uhifadhi nchini alisema, tayari ameshaunda
kamati ya watu sita ikiongozwa na Mkuu wa Chuo cha Wanyamapori Mweka,
Prof. Kidegesho kwa ajili kuangalia namna bora ya kutekeleza azma hiyo.
"Tayari kamati hiyo imeshaanza kazi na itaonana na wadau mbalimbali
kupata maoni yao na katika kipindi cha mwezi na nusu watatuletea
ripoti", alisema.
Kwa
upande wake Balozi Konchanke alimuahakikishia Prof. Maghembe kuwa
Serikali ya Ujerumani itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania
katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili hifadhi hiyo
ikiwemo ubovu wa miundombinu na uvamizi pori hilo kwa faida ya jamii
kwa ujumla. Aidha, alitoa wito kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori
Tanzania TAWA kubuni mbinu mpya za kukabiliana na changamoto zilizopo.
Meja
Jenerali Gaudence Milanzi ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na
Utalii, yeye alisema "Serikali kwa kushirikiana na wadau wa uhifadhi
imefanya kazi kubwa kuhakikisha Selous haiondolewi katika orodha ya
maeneo ya urithi wa dunia yaliyopo hatarini kutoweka, hiyo ni pamoja na
kunzishwa kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyanapori Tanzania TAWA,
kuanzishwa kwa mkakati wa kitaifa wa kukabiliana na ujangili na miradi
mbali ukiwemo huu wa SECAD uliozinduliwa leo ambayo kwa kiasi kikubwa
imeasaidia katika kuendesha hifadhi zetu pamoja na kusaidia kwenye
mapambano dhidi ya ujangili".
Naye
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania,
TAWA, Martin Loibooki aliishukuru Serikali ya Ujerumani kwa mradi huo na
kusema kuwa utasaidia kwa kiasi kikubwa kukabiliana na changamoto
mbalimbali katika pori hilo ikiwemo ya uhaba wa vitendea kazi na
ujangili na hivyo kuifanya hifadhi hiyo iendelee kuwa miongoni mwa
maeneo ya urithi wa dunia.
Pori
la Akiba la Selous ni hifadhi kubwa kuliko zote Tanzania ikiwa ukubwa
wa Kilomita za mraba 50,000. Hifadhi hiyo ambayo ipo katika mikoa ya
Morogoro, Pwani, Lindi, Mtwara na Ruvuma ina vivutio vingi vya utalii na
inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo miundombinu ya barabara za
kuingia katika hifadhi hiyo, ujangili, rasilimali watu na vitendea
kazi.
COMMENTS