Wananchi wilayani Handeni wapigwa marufuku kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kutoka katika vyanzo vya maji na kutakiwa...
Wananchi
wilayani Handeni wapigwa marufuku kufanya shughuli za kibinadamu ndani
ya mita 60 kutoka katika vyanzo vya maji na kutakiwa kutunza mazingira
ili kuwezesha uendelevu wa maisha.
Marufuku
hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe aliyekuwa
mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya siku ya mazingira duniani
yaliyofanyika ngazi ya wilaya katika Kata ya Mkata katika bwawa la
Tulafimbo.
Gondwe
alisema kuwa wananchi lazima wazingatie sheria ya Mazingira inayozuia
kufanya shughuli za kibinadamu pamoja na kujenga kwenye maeneo yote ya
vyanzo vya maji ndani ya mita 60. “Kwa kuzingatia sheria hiyo, kupiga
marufuku kwa wananchi kufanya shughuli zozote za kibinadamu zenye
kuhatarisha usalama wa maji na uchafuzi wa mazingira kwenye maeneo
yanayozunguka vyanzo vya maji wilayani Handeni” alisema Gondwe.
Aidha,
aliwataka maafisa Tarafa, maafisa watendaji wa Kata na wenyeviti wa
Vijiji kuhakikisha wanatengeneza mipaka kwenye maeneo ya vyanzo vya maji
vyote vilivyopo Wilayani Handeni msimu huu ambao mvua imenyesha ya
kutosha na vyanzo vingi vimejaa maji. “Hii itasaidia kuzuia uvamizi wa
maeneo hayo na kurahisisha kuchukua hatua kwa watu watakaokwenda kinyume
na amri hiyo” alisema Gondwe.
Gondwe,
aliwataka wananchi wote walionunua mashamba kwa lengo la kilimo
kusafisha mashamba yao kwa kuacha asilimia 30 ya uoto wa asili badala ya
kusafisha maeneo yote ambayo wamenunua. “Tusipotunza mazingira, itakuwa
ni ubinafsi kwa kizazi chetu na kizazi kijacho. Tukitendee haki kizazi
hiki na kijacho kwa kuondoa ubinafsi wa kuharibu mazingira” alisema
Gondwe.
Wakati
huohuo, aliwataka viongozi ngazi ya Wilaya, Tarafa, Kata na Vijiji
kutunza kutunza mazingira kwa kusimamia uwiano wa ardhi uliyopo na idadi
ya mifugo ili kutunza mazingira kwa kuwa na mifugo inayoendana na
rasilimali ardhi iliyopo. Aliwataka kuweka mikakati ya kupiga chapa
mifugo ili kurahisisha utambuzi wa mifugo hiyo wilayani Handeni.
Katika
hatua nyingine Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni,
William Makufwe aliwataka wananchi kutunza rasilimali maji kidogo
inayopatikana kwa kipindi cha mvua kwa kupanda miti kwenye maeneo
yanayozunguka vyanzo vya maji. Alisema kuwa Serikali inaendelea
kushughulikia changamoto ya upatikanaji maji ya kudumu Wilayani
Handeni.
Aliwataka
wakuu wa shule za msingi na sekondari kuhakikisha kila mwanafunzi
anayeanza darasa la kwanza hadi la saba na kidato cha kwanza hadi cha
nne anakuwa na mti wake anaoutunza ili anapomaliza shule akikabidhiwa
cheti na yeye akabidhi mti alioutunza kwa kipindi chote alichokuwa
shuleni.
Maadhimisho
ya wiki ya mazingira kiwilaya yalitanguliwa na upandaji miti 28,954
yakiongozwa na kaulimbiu isemayo “hifadhi ya mazingira muhimili kwa
Tanzania ya viwanda”.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh Godwin Gondwe akipanda mti kwenye maadhimisho.
Mkurugenzi
Mtendaji Bw William Makufwe iyeshika chepeo na mwenyekiti wa
Halmashauri ya Handeni Mh Ramadhani Diliwa wakipanda mti.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh Godwin Gondwe akizungumza na wananchi.
Mkurugenzi Mtendaji Bw William Makufwe akizungumza na wananchi wakati wa maadhimisho.
Mwenyekiti wa Halmashauri Mh Ramadhani Diliwa akizungumza na wananchi.
Wanafunzi wa shule ya sekondari Mkata wkisherehesha kwa Ujumbe wa utunzaji mazingira.
Halila
Tongolanga amefariki jana usiku katika hospitali ya Muhimbili. Alikuwa
mwanamuziki wa siku nyingi na alifahamika kwanza kwa wengi baada ya kuanza kusikika kibao chake cha lugha ya Kimakonde cha Kila munu ave na kwao, chenye
tafsiri ya ‘Kila mtu ana kwao’ ambacho alikirekodi akiwa bendi ya jeshi ya CTU
Monduli, iliyojulikana kama Les
Mwenge. Kwa kifupi ni kuwa baada ya hapo aliitwa kujiunga na bendi iliyokuwa
mali ya Dr Alex Khalid, iliyokuwa ikiitwa Makondeko Six. Wakati huo Dr Khalid
alikuwa na sehemu kubwa ya burudani iliyokuwa pia na ukumbi na ilikuwa inaitwa
Makondeko ikawa na bendi ya watu sita hivyo bendi hiyo ikaitwa Makondeko Six.
Bendi hii awali ilikuwa ikipiga muziki kwa kufuata nyayo za bendi ya Tatu Nane,
lakini Dr Khalid baada ya kuona bendi haina umaarufu kutokana na aina ya muziki iliyokuwa ikipiga, ndipo alipomuita
Halila Tongolanga nae akaja na baadhi ya wanamuziki wakajiunga na kuanzisha kundi
lililoendelea kutumia jina la Makondeko Six japo wanamuziki walikuwa wengi zaidi
ya sita. Na ndipo katika kundi hili lilikuwa na wanamuziki wengine kama
Innocent Nganyagwa, Anna mwaole wakaweza kurekodi tena wimbo wa Kila Munu Ave
na kwao na kundi kupata umaarufu mkubwa mpaka baada ya kusambaratika kwa Makondeko baada ya kifo cha Dkt. Alex Khalid lakini Tongolanga aliendelea
kutumia jina la Makondeko.
Tongolanga amefanya kazi nyingi za muziki ikiwemo
kuwa mmoja wa kundi lililoundwa na wanamuziki wengine mahiri kama Moshi William, Muhidin Mwalim, Huluka Uvuruge, Kandaya na wengine lililojulikana
kama Bana mwambe, ambapo waliweza kutoka nyimbo nyingi nzuri sana wakati
biashara ya kuuza album ilipokuwa ina faida. Tongolanga ameagwa na wapenzi wa
muziki ndugu na marafiki, lakini kulikuwa na uhaba mkubwa wa wanamuziki wenzie katika
kundi lililokuja kumuaga mwanamuziki huyu. Waliojitokeza hasa ni wanamuziki wale tu
ambao waliwahi kupiga nae katika kundi la Makondeko na Bana Mwambe na wanamuziki wengine wachache wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Muziki John Kitime, Katibu Mkuu wa Chamudara Hassan Msumari. Serikali iliwakilishwa na Katibu Mtendaji wa BASATA. Katika jambo moja kubwa lililotokea
wakati wa kuaga mwili ni kujitokeza kwa balozi wa Msumbiiji Bi Monica Patricio
Clemente aliyefika Muhimbili kuaga mwili wa Tongolanga akiwa amesindikizwa na maafisa wengine, na pia Balozi huo alitoa
rambirambi zake kama Balozi na alitoa rambirambi kutoka kwa Waziri wa Ulinzi wa
Msumbiji. Hili lilikumbusha usemi wa wahenga ‘Nabii hathaminiwi kwao.’ Taarifa
zilizopatikana pale ni kuwa Tongolanga alikuwa mtu maarufu sana nchini
Msumbiji, na aliyekuwa ni msanii muhimu wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu nchini
humo.
Balozi wa Msumbiji Bi Monica Patricio Clemente akiaga sanduku lililokuwa na mwili wa Halila Tongolanga |
Nilipokutana
nae kwa mara ya mwisho akiwa kitandani Tongolanda kwa sauti ya uchovu alinambia
alikuwa na mengi ya kunambia, wakati tunasubiri taratib kukamilika za kuanza
kusafirisha mwili, Innocent Nganyagwa ambaye alikuwa mmoja ya wanamuziki
waliotengeneza kundi la Makondeko Six alinambia Tongolanga alikuwa amepanga
kufanya onyesho la ‘Usiku wa Makondeko’ na alikuwa na mipango mingine mikubwa
ya kufanya kupitia kipaji chake. Pengine ndiyo hayo aliyotaka kunambia Mungu
pekee anajua.
Shukrani za pekee zimfikie Mbunge wa Tandahimba Mheshimiwa Katani Ahmed Katani, kwani kwa juhudi zake Tongolanga alisafirishwa akiwa hai kutoka Ndanda hadi Dar es Salaam kwa matibabu, na pia ndie aliyeusafirisha mwili wa mwanamuziki huyu kwenda Mchichila kwa ajili ya mazishi.
Toka kushoto Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi Nyangamale, Balozi wa Msumbiji nchini, Katibu Mtendaji wa BASATA, Mbunge wa Tandahimba Mhe Katani Katani, afisa wa Ubalozi wa Msumbiji |
Tongolanga
anategemewa kuzikwa kijijini kwao Mchichila kesho Junanne 6 Juni 2017.
Mungu
Amlaze Pema Halila Tongolanga
Mpiga Kinanda Geophrey Kumburu, Katibu Mtendaji wa BASATA Godfrey Mngereza, Katibu Mkuu wa CHAMUDATA Hassan Msumari |
John Kitime, wanamuziki wa Makondeko Six, Mngereza, KumburuAdd caption |
Sanduku alilolazwa Halila Tongolanga likitayarishwa kuingizwa kwenye gari la kusafirisha kuelekea Mcjichila |
Sanduku likiingizwa kwenye gari |
Imetayarishwa na John Kitime wa www.tanzaniarhumba.blogspot.com
COMMENTS