Frank Mvungi- Maelezo Serikali imetumia shilingi bilioni 16.9 kununua vifaa vya maabara na vile vya wanafunzi wenye mahitaji m...
Frank Mvungi- Maelezo
Serikali
imetumia shilingi bilioni 16.9 kununua vifaa vya maabara na vile vya
wanafunzi wenye mahitaji maalum vitakavyonufaisha shule za sekondari
1696 ambapo shule 1625 ni za Kata na 71 ni kongwe ambazo kwa sasa zipo
katika ukarabati.
Akihutubia
wakati wa hafla ya kuzindua mpango wa kusambaza vifaa vya maabara na
vifaa vya wanafunzi wenye mahitaji maalum leo Jijini Dar es Salaam,
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa
ambaye alikuwa mgeni rasmi, amesema dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano
ni kuhakikisha kuwa inaboresha sekta ya elimu ili azma ya ujenzi wa
Tanzania ya Viwanda itimie kwa kuwa Taifa litaweza kuzalisha wanasayansi
kulingana na mahitaji.
“Tunatoa
vifaa hivi kwa awamu ya kwanza kwa shule zilizokamilisha ujenzi wa
maabara, hivyo ni matumaini yangu kuwa wale ambao hawajakamilisha
watafanya hivyo ili awamu ijayo nao wapate vifaa hivi.” Alisisistiza
Majaliwa.
Aliongeza
kuwa dhamira ya serikali ni kuhakikisha zaidi ya shule 4,000 nchini
zinakuwa na vifaa vya maabara, walimu, vifaa vya kujifunzia na
kufundishia na mazingira rafiki ili kuwawezesha wanafunzi kupata elimu
bora itakayowasaidia kushiriki katika ujenzi wa Taifa.
Pia
Waziri Mkuu ameonya kuwa Serikali itachukua hatua kali dhidi ya mtu
yoyote atakaye sababisha mwanafunzi wa kike kupata ujauzito na kushindwa
kuendelea na masomo ambapo atakabiliwa na adhabu ya kwenda jela miaka
thelathini.
“Awe
baba au mama au mtu yoyote ambaye itathibitika kuwa amemsababishia
ujauzito mwanafunzi, adahabu yake ni kifungo cha miaka thelathini jela.”
Alisisitiza Majaliwa.
Kwa
upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce
Ndalichako amesema Serikali imetenga fedha katika bajeti ya mwaka
2017/2018 kwa ajili ya kuendelea kununua vifaa hivyo lengo likiwa
kuendelea kuinua kiwango cha elimu kwa kushirikisha wadau wa maendeleo.
“Vifaa
hivi vinakidhi mahitaji ya wanafunzi kuanzia kidato cha kwanza hadi cha
sita na upatikanaji wa vifaa hivi ni utekelezaji wa ahadi ya serikali
ya Awamu ya Tano kwa wananchi katika kuboresha sekta ya elimu na
vitawaongezea wanafunzi kasi ya kudadisi na kujifunza.” Alisisistiza
Prof. Ndalichako.
Akifafanua
kuhusu upatikanaji wa vifaa hivyo Prof. Ndalichako aliwashukuru wadau
wa Maendeleo ikiwemo Benki ya Dunia, Uingereza, Denmark na wengine kwa
kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuinua kiwango cha elimu nchini
ili kuchochea maendeleo kwa kuwa ufaulu wa masomo ya sayansi
utaongezeka.
Kwa
Upande wake Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein
Mwinyi amesema kuwa kazi ya kupokea vifaa hivyo imefanyika kwa ufanisi
na kuahidi kuwa watatekeleza jukumu la kusambaza vifaa hivyo kama
ilivyopangwa kupitia Jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Vifaa
hivyo vya maabara na vile vya wanafunzi wenye mahitaji maalum vyenye
thamani ya shilingi bilioni 16.9 vitasambzwa katika Kanda 11 na baadhi
ya mikoa itakayonufaika katika Kanda hizo ni Dar es Salaam, Katavi,
Kagera, Rukwa, Pwani, Tanga, Mwanza, Singida, Dodoma.
Waziri
Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa akizungumza na baadhi ya walimu na
wanafunzi wa shule za sekondari za mkoa wa Dar es Salaam (hawapo
pichani) wakati wa uzinduzi wa zoezi la usambazaji wa vifaa vya maabara
na vifaa vya wanafunzi wenye mahitaji maalum mapema hii leo katika
viwanja vya hospitali ya Jeshi Lugalo jijini Dar es Salaam.
Waziri
Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa (mwenye tai nyekundu) akipata maelekezo
toka kwa moja ya mwalimu wa masomo ya sayansi wakati wa uzinduzi wa
zoezi la usambazaji wa vifaa vya maabara na vifaa vya wanafunzi wenye
mahitaji maalum mapema hii leo katika viwanja vya hospitali ya Jeshi
Lugalo jijini Dar es Salaam.
Waziri
Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa (mwenye tai nyekundu) akikata utepe
kuashiria uzinduzi rasmi wa zoezi la usambazaji wa vifaa vya maabara na
vifaa vya wanafunzi wenye mahitaji maalum mapema hii leo katika viwanja
vya hospitali ya Jeshi Lugalo jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa (kulia) akikabidhi moja ya kifaa
cha kufundishia masomo ya sayansi kwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari
Juhudi wakati wa uzinduzi wa zoezi la usambazaji wa vifaa vya maabara
na vifaa vya wanafunzi wenye mahitaji maalum mapema hii leo katika
viwanja vya hospitali ya Jeshi Lugalo jijini Dar es Salaam.
Baadhi
ya walimu wa Mkoa wa Dar es Salaam wakimsikiliza Waziri Mkuu Majaliwa
Kassim Majaliwa (hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa zoezi la
usambazaji wa vifaa vya maabara na vifaa vya wanafunzi wenye mahitaji
maalum mapema hii leo katika viwanja vya hospitali ya Jeshi Lugalo
jijini Dar es Salaam.
Baadhi
ya wanafunzi wa shule za Mkoa wa Dar es Salaam wakimsikiliza Waziri
Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa (hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa
zoezi la usambazaji wa vifaa vya maabara na vifaa vya wanafunzi wenye
mahitaji maalum mapema hii leo katika viwanja vya hospitali ya Jeshi
Lugalo jijini Dar es Salaam.
(Picha na Eliphace Marwa - Maelezo)
COMMENTS