NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR. NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Abdalla Juma Saadala "Mabodi" amezitaka jumuiya za Chama hich...
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Abdalla Juma Saadala
"Mabodi" amezitaka jumuiya za Chama hicho kutumia vizuri fursa ya
uchaguzi kuwapitisha viongozi wenye sifa na uwezo wa kukiletea ushindi
chama katika Uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Kauli hiyo ameitoa wakati akifungua mafunzo elekezi ya
kuwajengea uwezo viongozi wa majimbo Tisa (9) ya Chama na Jumuiya za
Mkoa wa Mjini juu ya mabadiliko ya Katiba ya CCM ya 1977 yaliyofanyika
hivi karibuni yaliyofanyika Katika ukumbi wa mkoa huo Aman Unguja.
Alisema
uchaguzi unaofanyika hivi sasa katika kwa ngazi mbali mbali za Chama
hicho ndio uwanja wa kuandaa jeshi kamili la kisiasa lililokamilika kila
idara na lenye ujuzi na mafunzo yote ya vita ya kisiasa litakaloweza
kupambana kwa ujasiri na kufanikisha ushindi katika uchaguzi mbali mbali
za Dola ili CCM iendelee kushinda na kutawala kupitia utaratibu wa
Kidemokrasia.
Aliwasihi washiriki wa mafunzo hayo kutumia vyema mafunzo
hayo ya siku moja ili waweze kuwa na uelewa mpana wa Mabadiliko kadhaa
yaliyofanyika ndani ya katiba ya CCM ili watekeleze kwa ufanisi majukumu
yao na kuwaelimisha wanachama wengine juu ya taaluma hiyo.
Dkt.Mabodi alieleza kwamba matarajio ya taasisi hiyo ya
kisiasa ni kuona kasi ya mabadiliko ya kiutendaji kwa haraka hasa kwa
viongozi na watumishi wa Chama na jumuiya zake.
Pia aliongeza kwamba mbali na matarajio hayo mafunzo hayo
yatamaliza mizozo na malalamiko yaliyokuwa yalisababisha kutokuwepo kwa
ufanisi mzuri wa kiutendaji kwa baadhi ya maeneo ndani ya Mkoa huo.
Naibu Katibu Mkuu huyo alisema hatovumilia tabia za
kupangwa safu za viongozi kwani kufanya hivyo ni kukiuka Kanuni za
maadili na miongozo ya uchaguzi huo.
" Tumekuwa tukisema siku zote kuwa CCM ndio mwalimu wa
Demokrasia yaani hivyo vyama vya upinzani demokrasia na ustaarabu wa
kisiasa tumewafunza sisi hivyo dhana hizo lazima tuzisimamie na
kuzitekeleza kwa vitendo kupitia uchaguzi unaoendelea ndani ya taasisi
yetu.", alisema Dkt.Mabodi na kuzitaka kamati za uchaguzi na maadili
kufuatilia kwa kina mwenendo wa uchaguzi na watakapobaini kasoro watoe
taarifa kwa ngazi husika ili zitafutiwe ufumbuzi wa haraka.
Alifafanua kwamba kupitia uchaguzi huo panatakiwa
kupatikana viongozi na watendaji watakaoendeleza siasa za upendo,
maendeleo, umoja pamoja na mshikamano unaojali misingi ya kidemokrasia
ndani na nje ya taasisi hiyo.
Hata hivyo alieleza dhamira ya chama hicho kupitia
mabadiliko yaliyofanyika katika Katiba ya Taasisi hiyo kuwa ni pamoja na
kila mwanachama kujipanga kisaikolojia kusaidia kuimarisha uchumi wa
CCM kupitia rasilimali zilizopo sambamba na kubuni miradi mingine ya
kimaendeleo.
Sambamba na hayo kupitia Mafunzo hayo Dkt.Mabodi
aliwakumbusha washiriki hao kwamba ili wafanikiwe katika utendaji wao ni
lazima watumie vizuri rasilimali watu ya wazee wa CCM pamoja na
wastaafu katika sekta za umma na binafsi kwani wana uwezo na uzoefu
mkubwa wa kushauri na kutoa maelekezo mazuri juu ya masuala mbali mbali
ya kiutendaji ndani ya Chama hicho.
Mapema akizungumza katika mafunzo hayo Mwenyekiti wa Mkoa
huo, Nd. Bora afya Juma Silima alisema Mkoa huo umejipanga kufanikisha
kwa ufanisi uchaguzi huo ili kulinda historia ya chama hicho katika
kufanikisha uchaguzi unaoheshimu misingi ya utawala bora na demokrasia
kwa wananchi wote.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wakisikiliza kwa makini Nasaha za Mgeni rasmi Dkt. Abdalla Juma Saadala huko ktk ukumbi wa Mkoa huo Aman Unguja. |
COMMENTS