F SKIMU 7 ZA UMWAGILIAJI WILAYANI MBARALI ZATOZWA FAINI KWAKUTO ZINGATIA SHERIA YA MAZINGIRA | RobertOkanda

Friday, April 28, 2017

SKIMU 7 ZA UMWAGILIAJI WILAYANI MBARALI ZATOZWA FAINI KWAKUTO ZINGATIA SHERIA YA MAZINGIRA


Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Richard Muyungi akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa Kikosi kazi cha kitaifa cha kutathmini  Ikolojia
ya Mto Ruaha Wilayani Mbarali Mkoani Mbeya.

Kikosi kazi cha kitaifa cha kutathmini  Ikolojia ya Mto Ruaha kikiwa katika moja ya skimu za umwagiliaji Wilayani Mbarali Mkoani Mbeya

Na Sarah Maganga (Afisa habari Mkoa wa Mbeya)Kikosi kazi cha kitaifa cha kutathmini  Ikolojia ya Mto Ruaha kimezitoza faini ya jumla ya shillingi 180,290,000 skimu 7 za umwagilija za  Iyala, Ukwavila- Nguvukazi, Madibira,
Mwendamtitu, Mbarali Estate, Kapunga na Kapunga Smallholders zilizopo Wilaya ya Mbarali kwa kutozingatia  sheria za Mazingira, Umwagiliaji  na kutumia maji
bila kupata kibali cha matumizi kutoka Mamlaka husika.
Akiongea kwa niaba ya Wajumbe wa Kikosi Kazi hicho Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Bwana Richard Muyungi amesema kuwa skimu hizo zimetozwa faini baada ya kugundua baadhi ya skimu zinatumia mifereji ya
matoleo ya maji na kuchepusha maji hayo kwenda kwenye mashamba bila utaratibu na kibali.

Muyungi amesema kuwa Skimu za Kapunga, Highland Estate na Madibira zimetozwa faini kwa kutozingatia sheria ya Mazingira, Maji na kutosafisha mifereji ya kuingiza na kutolea maji na kufanya maji mengi kutotiririka kuelea kwenye Mto Mbarali na Ndembela  na kusababisha mito hiyo kupungua maji.
Faini hizo zimetozwa kwa kufuata sheria za Mazingira, Maji
pamoja na Umwagiliaji kwa mchanganuo ufuatao kwa kila skimu ambapo Iyala wametozwa shilingi 2,200,000, Kapunga Farm shilingi 33,100,000, Mbarali Estate shilingi
33,000,000 Kapunga Small Holders shilingi 3,000,000 Madibira shilingi 33,000,000 Mwendamtitu shilingi 37,995,000 na Ukwavila- Nguvu Kazi shilingi 37,995,000.Aidha Mwenyekiti wa Kikosi Kazi hicho ambaye ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya Bibi Mariamu Mtunguja amesema kuwa faini hizo zinaenda sawa na maagizo waliyopewa skimu zote ya kufanya marekebisho ya miundombinu ya shamba ikiwa pamoja na kusafisha miundombinu hiyo na kuomba kibali cha matumizi ya
maji kwa kuzingatia taratibu na sheria.
Mtunguja amesema Kikosi kazi kimetoa muda wa mwezi mmoja na nusu kwa wakulima wanatumia maji bila kibali kuvuna mazao yao yaliopo shambani na baada ya hapo mashamba hayo yatafungiwa mpaka pale wakulima hao
watakapo pata kibali cha matumizi ya maji.
Naye Mwenyekiti wa muda wa Wakulima wa Kijiji cha Iyala Lenard Mwashikamile amekiri kuwa wakulima wa Kijiji hicho wanatumia maji kutoka kwenye mifereji ya matoleo ya mwekezaji bila kibali na kuomba wapewe muda wa
kumalizia msimu huu wa mavuno.


Mwashikamile amesema kuwa kutokana na uhaba wa mvua
msimu huu wamekuwa wakichepusha maji kutoka kwa mwekezaji kwa ajili ya matumizi ya umwagiliajia mashamba yao ya mpunga  pamoja na mifugo na wakijua kuwa ni kinyume cha taratibu na kuahidi kufunga miferji hiyo baada ya msimu huu wa kilimo.


Naye Afisa Uhusiano wa Mashamba ya Kapunga Bwana James Maliki ameshukuru Kikosi Kazi kwa kujionea maendeleo ya shamba la Kapunga na kuliweka
katika hali nzuri na kukiri kuwepo kwa wakulima jirani na mashamba hayo kuiba na kutumia maji bila Kibali na kuahidi kuanza kushughulikia suala hili kwa kuweka ulinzi wa kutosha na kuweka matuta kwenye mifereji ya matoleo.Kikosi Kazi cha kutathmini Ikolojia ya mto Ruaha kiliundwa na Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu kwa lengo la kupata maoni na changamoto za wadau kuhusu kupungua kwa maji katika Hifadhi ya Ruaha na mabwawa ya Kidatu na Mtera.

0 comments:

Post a Comment