F HOJA/MTAZAMO- JAMII IENDELEE KUELIMISHWA KUHUSU UHIFADHI NA ULINZI WA MAENEO YA UOTO WA ASILI | RobertOkanda

Wednesday, April 26, 2017

HOJA/MTAZAMO- JAMII IENDELEE KUELIMISHWA KUHUSU UHIFADHI NA ULINZI WA MAENEO YA UOTO WA ASILIJAMII IENDELEE KUELIMISHWA KUHUSU UHIFADHI NA ULINZI WA MAENEO YA UOTO WA ASILI.
Na Ismail Ngayonga
MAELEZO
Dar es Salaam

TAARIFA ya Wizara ya Maliasili na Utalii inaonesha kuwa Tanzania inapoteza takribani hekta 372,000 za uoto wa asili kila mwaka kutokana na ukataji wa miti hovyo, kilimo kisicho endelevu, uchungaji holela wa mifugo, katika maeneo yaliyohifadhiwa.
Takwimu hizo zinaeleza kuwa maeneo yenye ukubwa wa takriban hekta milioni 48.1 yanayojumuisha Hifadhi za Misitu, Mapori ya Akiba, Mapori Tengefu na  Hifadhi za Taifa yanaelezwa yapo hatarini kupotea na kutishia uhifadhi endelevu nchini.

Aidha inaelezwa kuwa katika mapori mengi ya akiba nchini yamevamiwa na makundi ya ng’ombe yaliyochanganyika na wanyamapori jambo linalosababisha kutoweka kwa wanyamapori au kuhama katika makazi yao ya asili na kuvamia makazi ya wananchi.

Kutokana na uharibifu huo mkubwa wa maliasili unaoendelea katika hifadhi hizo, Serikali iliunda kikosi kazi chenye wajumbe kutoka Wizara sita zinazohusika moja kwa moja na changamoto mbalimbali za ardhi, kwa madhumuni mapana ya kufanya uchunguzi wa kina na kupitia sheria zote zinazohusika.

Miongoni mwa sheria hizo ni pamoja na Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori, Na. 5 ya mwaka 2009, Sheria ya Misitu, Na. 14 ya mwaka 2002, Sheria ya eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Sura 284, R.E 2002 na Sheria ya Hifadhi za Taifa, Sura 282, R.E 2002.

Kumekuwa na mazoezi yanayoendelea nchini yanayohusu utekelezaji wa sheria hizo ambapo Wakala wa Misitu Tanzania, Taasisi za hifadhi za Wanyamapori zimekuwa zikiendesha mazoezi kwa kushirikiana na Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya na Mikoa mbalimbali.

Akizungumza na Waandishi wa Habari hivi karibuni, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani anasema kasi hiyo ya kupotea kwa uoto wa asili iwapo itaachwa iendelee itaiacha Tanzania bila uoto wa asili baada ya miaka 129.

Anaongeza kuwa ni wajibu wa wananchi kutii sheria na kuepuka vitendo viovu vinavyosababisha kupotea kwa uoto wa asili na kuepuka tishio la Tanzania kugeuka Jangwa.

“Takwimu hizi zitabakia hivyo ikiwa idadi ya watu haitaongezeka, ukuaji wa shughuli za kibinadamu hautaongezeka na aina ya shughuli hizo haitabadilika, jambo ambalo
haliwezekani” anasema Mhandisi Makani.

Kwa mujibu wa Mhandisi Makani anasema kutokana na kuzingatia tishio hilo na umuhimu wa uhifadhi katika Taifa kiuchumi, kijamii na kiikolojia, Serikali ilitunga sera, sheria, kanuni na taratibu kwa madhumuni hayo.

Anaongeza kuwa kufuatia uzoefu katika utekelezaji wa sheria hizo na maoni mbalimbali kutoka kwa wananchi na wadau wengine, Serikali imekuwa ikitoa miongozo mbalimbali katika mazingira na nyakati tofauti kwa kuzingatia ongezeko
la idadi ya watu na milki zao dhidi ya ukubwa na ubora wa maeneo yaliyohifadhiwa.

Aidha Mhandisi Makani anasema katika kipindi hiki ambacho Serikali inaendelea kutafuta ufumbuzi wa kudumu na endelevu wa migogoro ya ardhi nchini, aliwataka  wafugaji kuondoa Mifugo yote iliyoko ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa kisheria iondolewe haraka kwa kuzingatia taratibu.   

Aidha Mhandisi Makani anasema Serikali inatarajia kuendelea kupata ushirikiano kutoka kwa wadau wote wa uhifadhi na wananchi kwa ujumla katika kutekeleza azma yake ya kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi duniani zinazoendana na Malengo ya Dunia ya Maendeleo Endelevu kupitia uhifadhi endelevu wa maliasili zake.

Wakati Serikali ikiendelea kutoa Elimu kwa njia mbalimbali na kufanya uhamasishaji, ni wajibu wa Wananchi kujenga na kuimarisha uelewa, utayari na kushiriki katika
jitihada hizo za Serikali.
0 comments:

Post a Comment