F WABUNGE WAPAZA SAUTI KUHUSU UZAZI WA MPANGO, KUPUNGUZA VIFO VINAVYOTAKANA NA UZAZI NA KUPANGA MAENDELEO TAIFA | RobertOkanda

Wednesday, March 8, 2017

WABUNGE WAPAZA SAUTI KUHUSU UZAZI WA MPANGO, KUPUNGUZA VIFO VINAVYOTAKANA NA UZAZI NA KUPANGA MAENDELEO TAIFA
Asasi ya Kibunge inayojihusisha na masuala  ya
Idadi ya watu na maendeleo (TPAPD) imeelezea umuhimu wa kuweka kipaumbele
kwenye masuala ya uzazi wa mpango ili kukabiliana na ongezeko la kasi la idadi
ya watu  ambayo kwa sasa ni wa asilimia 2.7 kwa mwaka.

Tamko la TPAPD lilitolewa leo katika kuadhimisha siku ya
Kimataifa ya Wanawake Machi 8, limesema matumizi ya njia za uzazi wa mpango
yanaweza kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi (MMR) kwa asilimia 44, na
kupunguza vifo vya watoto kwa asilimia 35. Vifo vya wanawake katika uzazi
vimefikia 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2015 kutoka vifo 454 katika
kila vizazi hai mwaka 2010.


TPAPD chini ya Mwenyekiti wake Mhe Dkt Mary Mwanjelwa
iliamua kutoa tamko hili hivi karibuni katika kikao cha kamati tendaji mjini
Dar es Salaam kilichojadili umuhimu wa uzazi wa mpango katika harakati za
kujenga Tanzania ya uchumi wa kati na uchumi wa viwanda.

Tamko hilo lililotiwa saini na Mwenyekiti Dkt Mwanjelwa
limesema:

Uzazi wa mpango unahitajika katika kuiwezesha nchi
kukabiliana na ongezeko la kasi la idadi ya watu inayochangiwa na uzazi wa
kiwango cha wastani wa watoto sita kwa kila mwanamke aliye katika umri wa uzazi. Hali hii huchangia utegemezi pamoja na umaskini; na pia hudumaza juhudi za taifa za kufikia malengo ya maendeleo”.


“TPAPD inatambua na kuunga mkono kwa dhati kasi
ya  utekelezaji wa mpango Mkakati wa Taifa wa kuimarisha afya ya
uzazi, afya ya mama na mtoto, na vijana (RMNCAH II 2016-2020),” na inaahidi kuwa bega kwa bega  katika kufanikisha upatikanaji
wa  huduma bora za  uzazi wa mpango kwa wote hapa nchini”,
limesema Tamko hilo.


Mhe Mwanjelwa amesema TPAPD inatambua mafanikio
yaliyopatikana katika kulifanya suala la uzazi wa mpango kuwa  nguzo
muhimu katika mpango wa taifa wa RMNCAH ambao pia unajulikana kama One Plan II, unaolenga kuongeza matumizi uzazi wa mpango kila mwaka, kupunguza vifo vya wanawake na watoto, na kuimarisha afya ya uzazi kwa vijana. Ifikapo 2020,Tanzania imeweka lengo la kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kufikia 293 kwa
kila vizazi hai 100,000.


Ikitambua mchango wa wabunge wote katika kuweka mazingira
wezeshi ya kisera na kwa serikali kutenga bajeti ya uzazi wa mpango, TPAPD
imetaka jitihada za dhati ziendelee kufanyika kuhakikisha ununuzi na usambazaji wa taarifa sahihi, njia za uzazi wa mpango, na vifaa vya kuimarisha afya yauzazi kote nchini.

0 comments:

Post a Comment