Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Lephy Gembe (Kulia) akimsikiliza Mkurugenzi wa Mikopo na Biashara wa TADB, Robert Paschal (Kus...
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Lephy Gembe (Kulia) akimsikiliza Mkurugenzi wa Mikopo na Biashara wa TADB, Robert Paschal (Kushoto) wakati akitoa maelezo kuhusu Wajibu wa TADB katika kuendeleza kilimo nchini.
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Bw.
Lephy Gembe (Katikati) akizungumza na maafisa wa kutoka TADB wakati
walipomtembelea Ofisini kwake. Wanaomsikiliza ni Mkurugenzi wa Mikopo na
Biashara wa TADB, Bw. Robert Paschal (Wapili kushoto) na Meneja
wa Maendeleo ya Biashara wa TADB, Bw. Geofrey Mtawa (Kulia) na Afisa
Maendeleo ya Biashara Mwandamizi wa TADB, Bw. George Nyamrunda
(Kushoto).
Mkurugenzi wa Mikopo na Biashara wa TADB, Robert Paschal (Kushoto) akimsikiliza i Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Lephy Gembe (Kulia) walipomtembela Ofisini kwake.
Na Mwandishi wetu.
Benki mpya ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeaswa kutoa elimu kuhusu kilimo bora ili kuchagiza na kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Bw. Lephy Gembe wakati akiongea na Mkurugenzi wa Mikopo na Biashara wa TADB, Bw. Robert Paschal alipomtembelea Ofisini kwake.
Bw. Gembe alisema kuwa ili kuinua
uzalishaji wenye tija katika Sekta ya Kilimo kwa kuendeleza TADB ina
wajibu wa kutoa elimu ya kina kuhusu kilimo cha kisasa kwa kutilia mkazo
kuhusu miundombinu muhimu ya kilimo mathalani skimu za umwagiliaji za
kilimo ili kuongezea tija shughuli hizo za kilimo.
“TADB
muna wajibu wa kuhamasisha kilimo cha kisasa na cha kibiashara kwa
wakulima wadogo wadogo ili waweze kubadilisha fikra zao kutoka kilimo
cha mazoea na kufikiria kilimo cha kisasa chenye tija kitakachoongeza
kipato cha wakulima hao,” alisema Bw. Gembe.
Mkuu
huyo wa Wilaya ya Kilombero aliongeza kuwa TADB inapaswa kutekeleza kwa
vitendo juhudi za Serikali za kuinua ukuaji wa uchumi na kupunguza
umaskini nchini Tanzania kupitia kilimo ambacho kwa mujibu wa takwimu
kinaajiri zaidi ya asilimia 75 ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi
nchini na pia kutoa kiasi cha zaidi ya asilimia 65 cha mali ghafi kwa ajili ya viwanda vya nchi.
Bw. Gembe alisema kuwa ili kufikia malengo yake TADB inapaswa kuwa
na wataalamu wa utafiti na maendeleo ili waweze kuratibu taarifa za
utafiti na maendeleo ya Kilimo, hali ya hewa, udongo unaofaa kwa Kilimo,
pamoja na hatua nyingine za kuhuisha maendeleo kwenye Kilimo.
Akizungumza katika ziara hiyo Mkurugenzi wa Mikopo na Biashara wa TADB, Bw. Robert Paschal alisema kuwa TADB
imejipanga kutoa mikopo ya kilimo katika makundi matatu ambayo ni
Mikopo ya Muda Mfupi, Mikopo ya Muda wa Kati na Mikopo ya Muda Mrefu kwa
kutumia njia mbalimbali.
Akizitaja
njia ambazo TADB inatumia kutoa mikopo hiyo, zinajumuisha pamoja na
mambo mengine, mikopo ya moja kwa moja kwa vikundi vya wakulima wadogo
wadogo; kutoa mikopo
kwa njia ya marejesho taasisi zinazokopesha; utoaji wa mikopo kwa pamoja
na kushirikiana na taasisi/benki zingine; pamoja na mikopo ya
miundombinu inayolenga kupunguza mapengo ya upatikanaji wa fedha katika
minyororo ya ongezeko la thamani ya kipaumbele.
Bw.
Paschal aliongeza kuwa kwa kuanzia, TADB imelenga uwekezaji katika
maeneo nane (8) ya minyororo ya uongezaji wa thamani ambayo ni: nafaka,
kilimo cha mbogamboga, kilimo cha bidhaa za viwanda, mbegu za mafuta, ufugaji wa ng’ombe, ufugaji kuku, ufugaji wa samaki na bidhaa za misitu.
Aliongeza kuwa Benki pia inajitahidi kusimamia fedha kutoka kwa wafadhili wengine ambazo zimeelekzwa kwenye kuendeleza kilimo.
Mkurugenzi
huyo wa Mikopo alitumia fursa hiyo kumuomba ushirikiano Mhe. Gembe ili
kuhakikisha mikopo hiyo inarudishwa kwa wakati.
“Ili
kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, TADB inafanya kazi kwa karibu na
washirika mbalimbali wa kimkakati pamoja wadau wengine muhimu kutoka
ndani na nje ya nchi, hivyo ukiwa ni mdau muhimu, tunakuomba ushirikiano
katika kutimiza malengo ya kuanzishwa kwa TADB,” aliomba Bw. Paschal.
Kwa
mujibu wa Bw. Paschal wadau wengine wa TADB ni pamoja na Serikali,
Wizara na Wakala mbalimbali wa Serikali; Mashirika; Serikali za Mitaa,
Sekta Binafsi, benki na taasisi za fedha, Mashirika yasiyo ya
Kiserikali, Wafadhili wa ndani na wa Kimataifa, Taasisi za Utafiti na
Umma kwa ujumla.
COMMENTS