F SIKINDE KUIBUKA NA ALBAM MPYA YA JINAMIZI LA TALAKA 2014 | RobertOkanda

Saturday, March 1, 2014

SIKINDE KUIBUKA NA ALBAM MPYA YA JINAMIZI LA TALAKA 2014

SIKINDE KUIBUKA NA ALBAM MPYA YA JINAMIZI LA TALAKA 2014

Baada ya kimya kingi hatimaye bendi kongwe nchini iliyopata kutamba na kuwa bingwa katika mchuano na wapinzani wake wakubwa Msondo na kuibuka na ushindi na kuwa mabingwa wa muziki nchini mara mbili ambazo mashindano hayo yamepata kufanyika, bendi ya  Mlimani Park Orchestra “Sikinde Ngoma ya Ukae” imeanza kuipua nyimbo zake mpya zitakazokuwa katika album mpya ya “Jinamizi la Talaka”. 

Album hiyo itakayokuwa na jumla ya nyimbo 7, inatarajiwa kuzinduliwa mwaka huu 2014, ambapo mpaka sasa Sikinde wameshakamilisha jumla ya nyimbo tatu.

Miongoni mwa nyimbo zilizokamilika ni pamoja na,  Jinamizi la Talaka, itakayobeba albam hiyo, Za Mkwezi Mbili na Nikipata Nitalipa.

Kutokana na bendi hiyo kwenda kisasa zaidi imeamua kuziweka nyimbo hizo katika mtandao wao wa https://www.hulkshare.com/sikinde, ambapo unaweza kuzisikiliza Online na kutoa maoni ama ushauri ili kuboresha ama kufanyia marekebisho nyimbo hizo kabla ya kuzinduliwa rasmi.

Nyimbo nne nyingine zitakazokamilisha albam hiyo ni pamoja na Kibogoyo,  Dole Gumba, Ng'ombe Haelemewi na Nundu na  Tabasamu, ambazo nazo baada ya kukamilika zitawekwa kwenye mtandao huo ili kuwapa fursa mashabiki wa bendi hiyo kuzisikiliza kwa makini kabla ya kuzinduliwa rasmi.

Hii ni album ya kwanza kutolewa tokea mwaka 2009 iliporekodiwa album ya “Supu Umeitia Nazi” album iliyomfanya mwimbaji wake Karama Regesu kuchukua zawadi katika Tuzo za 'Kili Music Award' ya mwaka 2009 kwenye category ya “Mtunzi Bora wa Muziki”.
Rais Jakaya Kikwete, akizungumza na wanamuziki wa bendi ya Sikinde

0 comments:

Post a Comment